Na Hassan Msellem, Pemba
WNAFAUNZI 96 wa Skuli ya Ufundi Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, wamelazimika kusitisha masomo kwa kipindi cha siku mbili.
Hii ni baada ya vyumba vitatu vya dahalia walivyokuwa wakivitumia kuungua moto na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwemo ndani ikiwemo nguo za wanafunzi hao, vitabu, madaftari pamoja na mabegi.
Ambapo jambo hilo limepelekea wanafunzi 44 kati hao ambao ni wanafunzi wa kike kuruhusiwa kurudi nyumbani kwa siku mbili, ili kuipisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar, kufikiria mbinu mbadala ya kukabiliana na athari zilizopatikana kutokana na tukio hilo la moto ili wanafunzi hao waweze kuendelea na masomo.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi Afisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, amesema kutokana na athari zilizopatikana kutokana na moto huo wizara imelazimika kutoa pendekezo la kuwataka wanafunzi wote wakike ambao wameathiriwa na moto huo kurudi nyumbani .
Alieleza kuwa watakwenda nyumbani kwa kipindi cha siku mbili, ili kuipisha Wizara kufanya tathmini ya namna ya kuandaa mazingira mbadala, ili wanafunzi hao waweze kuendelea na masomo kwa amani.
Nae kaimu Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Abdu Ali Haji, amesema tukio limewaathiri kwa kiasi kikubwa.
Alifahamisha kuwa, kwani wanafunzi walikuwa katika hali ya maandalizi ya mitahani yao ya kidato cha nne, ikizingatiwa kuwa Skuli ni miongoni mwa skuli za Serikali zinazoangaziwa kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Nao baadhi wanafunzi walioathirika na tukio hilo, wameiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine, kubuni njia za haraka za kuweza kuandaa mazingira rafiki ya kuendelea na masomo.
Walisema ili tukio hilo lisiwe ndio chanzo cha wanafunzi kufeli katika mitihani yao kikanda na kitaifa.
Tukio jengine la moto lilitokezea Mei 8, mwaka huu kwa bweni la wanaume la skuli ya Madungu kuungua moto kidogo, kama ilivyokuwa baina ya Machi 7 na 8 kuungua kwa bweni la skuli ya Utaani kisiwani humo
Mwisho.
Comments
Post a Comment