NA HAJI NASSOR, PEMBA
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii Tanzania
TASAF, kisiwani Pemba, umewashanufaisha walengwa wa mpango wa kunusuru kaya
maskini 14, 280 waliomo kwenye shehia 78 za kisiwani humo.
Walengwa hao
waliomo kwenye mpango huo, kuanzia mwaka 2014 hadi 2019, tayari TASAF
imeshatumia shilingi bilioni 14.4 kwa ajili ya kuwalipa ruzuku walengwa hao.
Mratibu wa
TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alisema fedha hizo ni pamoja na zile za msingi,
masharti pamoja na za kazi za muda kwa walengwa hao.
Alisema,
walengwa hao walitakiwa wanapopokea fedha hizo, wabuni mikakati ya kujiendeleza
ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya ushirika, iwe vya ufugaji, kilimo,
biashara au ujasiriamali.
Alieleza
kuwa, hilo limefanikiwa kwa kuwepo vikundi 942, ambavyo ndani yake vinajumuisha
walengwa 12,000 wastani wa walengwa 15 kwa kila kikundi kimoja.
Mratibu
Mussa, alisema kati ya vikundi hivyo 942, vikundi 700 vimeshasajiliwa na kupata
hati kwa mujibu wa shughuli zao, na vyengine vilivyobakia 242 vinaendelea na
taratibu.
‘’Fedha za
TASAF shilingi bilioni 14.4 zilizotumika kama ruzuku kwa walengwa wetu 14,280,
hazijapotea bure na sasa zinaendelea kuzaa matunda kwa wahusika,’’anasema.
Hata hivyo
Mratibu huyo, alisema pamoja na vikundi hivyo, walengwa hao waliibua miradi 146
mikubwa, ambayo inawanufaisha wananchi wote wa shehia husika.
Akatolea
mfano wa mradi huo, kuwa ni ujenzi wa matuta ya kuzuilia maji ya bahari, ambayo
sasa imesababisha wakulima zaidi ya 300 shehia za Ndagoni na Tumbe mashariki
kurudi.
‘’Lakini
hata mradi wa ufufuaji wa mto wa asili shehia ya Kiwani wilaya ya Mkoani, na
upandaji miti shehia ya Makangale wilaya Micheweni, ni miradi mengine ya
mfano,’’alieleza.
Mlengwa wa
mpango huo wa kunusuru kaya maskini shehia ya Ukunjwi Maryam Bakar Issa miaka
60, alisema baada ya kupokea ruzuku hiyo, alikusanya pole pole na mwaka 2020
amenunua mtumbwi kwa shilingi 300,000.
‘’Mtumbwi
huo nimemkabidhi mtoto wangu na anavua, kwa siku hujipatia kati ya shilingi
50,000 hadi shilingi 80,000 hutegemeana na hali ya upatikanaji samaki,’’alisema.
Nae Amina
Shaaban Shamte, wa shehia ya Mgogoni wilaya ya Wete, alisema kwa sasa
amefanikiwa kujenga nyumba ya vyumba vitatu, kununua Ng’ombe na kuendesha
biashara ya nguo za mitumba.
‘’Kwa sasa
ninamtaji wa zaidi ya shilingi milioni 6.5, ambazo zote hizo chanzo chake ni
fedha za ruzuku ninazo pokea kutoka TASAF,’’alieleza.
Mwenyekiti
wa ushirika wa mboga mboga uitwao ‘tushikamane’ wa shehia ya Chimba
wilaya ya Micheweni, Fatma Juma Salim, alisema wamepata mafanikio makubwa.
‘’Ushirika
huu tumeshawahi kugawana faida mara tatu kwa wastani wa shilingi 70,000 kwa
kila mwanachama, kati ya wanachama wetu wote saba,’’alisema.
Hata hivyo
ushirika huo, ambao asili yake ulitokana na uwepo wa mfuko wao wa kuweka na
kukopa, umezaa mradi mwengine wa ufugaji kuku wa kienyeji na utengenezaji wa
vipochi maalum.
Kwa sasa
TASAF, inaendelea na zoezi la uhakiki kwa wananchi wengine, ili nao kuingia
kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini.
MWISHO.
Comments
Post a Comment