NA
HAJI NASSOR, PEMBA
“KABLA
ya kuja kwa mpango wa kunusuru kaya maskini, hali yangu ya maisha ilikuwa ya
kubahatisha hasa kujipatia mlo walau wa siku, ilikua kazi,’’
Ni maneno ya mwanzo ya mlengwa huyo wa TASAF, Amina Shaaban Shamte, alipokuwa
akizungumza nami, kwenye eno lake la malisho ya wanyama kijijini kwake Mgogoni wilaya ya Wete Pemba.
Amina kabla ya kutuliwa na TASAF mikononi mwake, ilikuwa jambo la kawaida,
kutimiza siku tatu bila ya mlo hata ule wa kumuwezesha kuishi.
“Kwanza niwashukuru viongozi
ambao walileta huu mpango wa kaya maskini, mfumo huu umekuwa ni mkombozi mkubwa
kwetu sisi ambao tuna hali ngumu za maisha”,
anasema.
Bi Amina anasema, kabla ya kuja kwa mpango huo wa kunusuru kaya
maskini, hakuwa na shughuli yoyote ya kujipatia kipato lakini baada ya kufikiwa
na TASAF aliweza kujishuhulisha na biashara ya kuuza nazi na ndio safari yake
ya kuona mwanga ilianzia.
Katika kipindi hicho ambacho TASAF haijamfikia, watoto wake kwenye
suala la kusoma ilikua ni kwa njia ya kubahatisha, hali iliyopelekea siku moja
mtoto wake kusitishwa masomo kwa ukosefu wa ada.
Kumbe sababu ya tukio, hilo ni baada ya mtoto wake kutotoa ada ya
shilingi 10,000 ingawa kwa wakati huo nae ilimkwama kooni na kubakia nyumbani
“Kwa kipindi hicho kutokana na hali yangu ya kimaisha, shilingi 10,000
ilikua ni sawa na milioni moja, ingawa alirudi lakini baada ya dhiki na tabu iliyonitoa kijasho,’’anasema.
BAADA YA
TASAF
Kwa mara ya kwanza ulipoanza mpango huo wa kaya maskini hakuamini,
wakati sheha wake alipomwendea, kwa kuanza kumuandikisha jina kwa ajili ya kufanyiwa
usajili.
“Alikuja mwanamke ambae alitumwa na sheha akaniandika na kuniambia,
kwa sababu ya ujane na watoto nilionao, kushindwa kujihudumia,’’anaeleza.
Anakumbuka kama leo, kwa mara ya kwanza alipokea shilingi 32,000, na
alichukua hatua ya kuwanunulia watoto sare za skuli, mabuku na viatu.
Jengine alichokifanya ni kununua chakula pamoja na samaki mnene, na kwa
mara ya kwanza, alikula chakula cha mchana akiwa na furaha na watoto wake.
Kisha kwa miezi menngine mlengwa huyo wa kaya maskini, alifikiria
namna ya kuanzisha biashara ambayo ana hakika inaweza kumtoa kimaisha.
‘’Nilianza na ununuzi wa nazi za shilingi 20,000, ambapo kila nazi kwa
kipindi hicho nilinunua kwa shilingi 200 na baada ya kuuza kila moja kwa
shilingi 500 na kujipatia faida ya shilingi 30,000,’’anasimulia.
Biashara ya nazi, iliendelea kumnogesha na kumuingia moyoni maana,
kisha alijikuta na mtaji wa shilingi 150,000 unaotokana na biashara hiyo.
Baadae Amina, alifungua njia nyingine ya kujiongezea kipato, baada ya
kuingia kwenye ununuzi wa nguo za mitumba na hasa za kitoto.
“Niliagizia kutoka Unguja roba bota la nguo hizo kwa shilingi 150,000
na kisha baada ya kuziuza nilijipatia faida ya shilingi 50,000 nilinogewa na
kuendelea tena,’’anaeleza.
Maajabu na hamu ya kufanya
biashara hiyo hasa aliyaona kwenye awamu tatu, pale alipochomoa shilingi
300,000 kujitupa tena Unguja, na safari hii akiingiza faida ya shilingi 150,000.
Kumbe Amina, pamoja na biashara yake hiyo, kisha alizaa fikra na hamu
ya kununua mifugo, ili maisha yake ayatawale.
‘’Nilitumia shilingi 300,000 kununua
mtamba wa Ng’ombe ingawa baada ya muda alizaa na kujipatia dume, ingawa nalo
halikudumu nilimuuza baadae,’’anaeleza.
Hata mara ya pili, alibahatika Ng’ombe dume ingawa nilimuuza kwa
shilingi 500,000 na hapo sasa hatua iliyofuata ni kutaka kuanzisha ujenzi wa
nyumba ya kudumu.
Maana wakati huo anaendelea kupokea fedha za mpango wa kunusuru kaya
maskini, Amina alikuwa akiishi kwenye nyumba ya tope tena ya kuazimwa.
Kwa sasa akiwa anaishi kwenye nyumba yake ya tofali yenye vyumba
vitatu, kwa mchango wake wa hapa na pale, tayari ameshatumia shilingi milioni
5.
‘’TASAF imenitoa kwenye nyumba ya kuazimwa tena ya tope na makuti, na
sasa naishi kwenye nyumba ya kifahari iliyoezekwa bati,’’anafafanua.
Sasa anajisifia kuwa ana uhakika wa maisha, achia mbali mlo wa mara
tatu kwa siku, jambo ambalo anasema hakuwahi kuliota kwenye mbio zake za
maisha.
MPANGO WAKE WA BAADAE
Moja ni kumalizia kuizeka nyumba, na kutoa mlango maalum wa duka, ili
sasa ahamie kwenye biashara ya nguo mpya (special) huku akiendelea pia na nguo
za mtumba.
Alifahamisha, mpango wake mkubwa wa baadae ili kuona anaishi katika
mazingira bora ni kumaliza kujenga nyumba yake na kueka duka la nguo mpya.
Malengo haya anaweza kuyafikia, maana pamoja na biashara zake hizo
pamoja na ufugaji, Amina ni mwanachama wa ushirika unaojishughulisha na
ufugaji.
Ushirika huo, uitwao ‘nia njema’ kwake anauona kama
dhahabu, maana umekuwa sehemu ya kung’arisha maisha yake ya kila siku.
SHEHA
Sheha wa Shehia ya Mgogoni Said Hamad Khamis, anasema wakaazi wa
shehia hiyo ni 4,326 kati ya hao waliomo kwenye kaya maskini ni 143 tokea mwaka
2014 akiwemo Amina.
Anasema, mpango huo wa kunusuru kaya maskini, umeibua miradi kadhaa ya
maendeleo ndani ya shehia, ikiwemo ya ufugaji, ujasiriamali na kilimo cha mboga
mboga.
‘’Kwa mfano pia ipo miradi ya
jamii kama ule wa maji safi na salama unaowahudumia wananchi 4000 na uwepo wa
kinu cha kusagishia nafaka unaosimamiwa na watu wenye ulemavu,’’anaeleza.
Jambo la kujivunia katika shehia yao ni kuona baadhi ya wananchi
waliokuwemo kwenye mpango wa TASAF wamepiga hatua kimaendeleo kwa kujipatia
kipato chao wenyewe.
Anasema, changamoto kubwa ambayo imekuwa ikijitokeza wakati wa
upokeaji wa fedha za TASAF ni masafa marefu wanayotembea walengwa na
ukizingatia wengine ni watu wazima wasiojiweza.
TASAF.
Mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania ‘TASAF’ Pemba Mussa
Said Kisenge anasema, mpango wa kunusuru kaya maskini ni chachu ya kuleta
maendeleo kwa wananchi.
Anasema walengwa 14,280 ndio wanaendelea kunufaika kupitia mpango huo
wa kunusuru kaya maskini ata hivyo anasema, walengwa ambao wamefikiwa na mpango
huo kwa Pemba kuanzia mwaka 2014 hadi 2019 ni 14,280 kupitia shehia 78, hadi
sasa fedha zilizofikia mikononi mwa walengwa ni Billioni 14.4, ambapo kwa
wastani kila mlengwa amepata shilingi 2,380/=.
MWISHO.
Comments
Post a Comment