SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imepandisha bei ya karafuu kutoka shilingi 14000 hadi shilingi 15000 kwa kilo moja ya Daraja la Kwanza kwa mwaka 2023-2024.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na kufunguliwa kwa vituo vya kununulia karafuu kwa Unguja na Pemba katika ofisi za Wizara hiyo Kinazini.
Alisema Shirika la Biashara la Taifa litafungua vituo mbali mbali vya kuauzia karafuu kuanzia tarehe 3 mwezi huu Unguja na Pemba hivyo amewataka wananachi kuuza karafuu zote katika Shirika hilo la Biashara la Taifa ZSTC.
Alifahamisha kuwa kwa hatua ya awali shirika litaanza kufungua kituo cha Saateni kwa Unguja na kwa upande wa Pemba watatumia Kituo cha Mkoani,Madungu na Bandarini Wete kuuzia zao hilo na kauahidi kuongeza kufungua Vituo vyengine kulingana na mahitaji.
Akizungumzia suala la malipo kwa wakulima wazao hilo alisema shirika limejipanga kuwalipa wananchi hapohapo kwa mfumo wa Kielektroniki kupitia mifumo ya benki ,mitandao ya simu na fedha taslimu kwa kiwango kidogo cha karafuu.
Waziri Omar aliwataka wananchi kuwa na namba za simu zilizosajiliwa kwenye mifumo ya kupokea fedha pamoja na nambari za akaunti za benki zilizo hai ili kurahisisha malipo wakiwa vituoni .
Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya kupunguziwa kilo alisema shirika limejipanganga kununua mashine za kielektroniki za kupimia karafuu ili kuondosha malalamiko hayo na kuwataka Wananchi kuzingatia usafi wa karafuu kabla ya kuzipeleka Vituoni ili Kuepusha Usumbufu.
“Msipeleke karafuu zilizojaa mchanga, makonyo na takataka nyengine ili kupunguza muda wa kuzichekecha,hii itawarahisishia wahudumu wetu kufanya kazi mara moja endapo karafuu zitakua safi,” aliwasisitiza.
Hata hivyo Waziri Omar aliwaasa wananchi kuanika karafuu zao kwa kutumia majamvi ili kupata ubora na daraja la kwanza la karafuu.
Sambamba na hayo, alisema serikali itachukua hatua kali kwa wale wote watakaojihusisha na kuuza karafuu kwa njia ya magendo na kuitaka jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuzia biashara hiyo.
“Serikali imeongeza bei ya karafuu kusudi kuwaongezea kipato wananchi wetu,haitapendeza kuzichukua karafuu zetu na kuziuza nje ya Tanzania kimagendo kwa maslahi binafsi tuende kwenye vituo husika hii ni kwa faida ya mtu mmoja na taifa kwa jumla,”alisema.
Mbali na hayo, aliwataka wazazi na walezi kutokuwaruhusu watoto hasa wa kike kujishughulisha na uchumaji au uokotaji wa karafuu (mpeta) kwani kunaweza kusababisha vitendo vya udhalilishaji na kukosa muda wa kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Comments
Post a Comment