HABIBA ZARALI,
PEMBA
Ofisa Mdhmini
Wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilali Ali amewataka waandishi wa habari kuendelea
kuelimisha jamii ili wafahamu umuhimu wa afya ya uzazi.
Alisema, moja ya kipaombele cha Wizara
ya Afya ni kupunguza vifo vya mama na mtoto, hivyo endapo waandishi wa habari
watatumia nafasi yao kutoa elimu hiyo, hakuna shaka kwani lengo
litafikiwa.
Afisa Mdhamini aliyasema hayo wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya siku tatu
yanayohusiana na afya ya uzazi yaliyofanyika katika ofisi ya TAMWA
Mkanjuni Chake Chake.
Alisema, bado kuna uwelewa mdogo kwa jamii katika kutambua
afya ya uzazi, jambo ambalo linachangia kukosekana kwa afya bora kwa mama na
mtoto.
Alieleza kuwa, Wizara ya Afya inathamini sana mchango wa
waandishi wa habari katika kutoa taaluma mbali mbali na kuifanya jamii kuweza
kubadilika na hatimae kufikia malengo mazuri yaliyokusudiwa.
"Nyinyi waandishi ni kioo kwa jamii kwani munaonekana
na kusikika na hata kusomwa na watu wingi kwa wakati mfupi, hivyo taaluma hii
ipelekeni ili jamii ielewe na iondokane na changamoto kwenye afya ya uzazi
zinazowakabili", alisema.
Kwa upande wake Afisa Miradi na Tathmini kutoka Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) upande wa Zanzibar Mohammed Khatib Mohamed
alisema, mafunzo hayo yamejenga kuwaongezea uwelewa waandishi wa habari katika
kuandika habari zinazohusiana na afya ya uzazi.
"Bado changamoto za afya ya uzazi zimewekwa nyuma na
hazijapewa kipao mbele kuripotiwa na waandishi, hivyo jamii haijaona umuhimu wa
masuala ya afya ya uzazi", alisema.
Kwa upande wake mkufunzi kutoka Kitengo cha Afya Dk.
Rahila Salim Omar aliwashauri wananchi kutumia uzazi wa mpango katika
kuimarisha afya zao.
Alifahamisha kuwa, suala la afya ya uzazi linaonekana ni
la akina mama pekee, jambo ambalo sio sahihi na kuwaomba wanajamii kufika
hospitali na vituo vya afya mapema endapo watabaini mabadiliko katika miili
yao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment