Skip to main content

UFUGAJI MATANGO BAHARI AJIRA YENYE GHARAMA NAFUU, 'TUMUOMBE MOLA' MBIONI KUVUNA 20/=MILIONI

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

‘…….SEA Cucumbers’ ama matango bahari…...

Na wingine huliita jongoo la pwani, ama kiazi bahari.

Ni aina ya wanyama ama kiumbe, kinachoendesha maisha yake baharini.

Kitango bahari, kina ngozi ngumu kiasi na mwili mrefu ambapo muonekano na maumbile yake ni sawa na kitango kinacholiwa nchi kavu.

Kitango bahari, kinaendelea kufafanuliwa kwenye vitabu na mitandao kuwa, kina mwili mrefu wenye via vya uzazi, moja iliyo na matawi.

Wanyama hawa, wanapatikana kwenye sakafu za bahari duniani kote, wakiwa wamegawanyika kwenye spishi zaidi ya 1,717.

Ingawa nyingi zao, zinapatikana eneo la Asia-Pasifiki, ambapo kwa Zanzibar utafiti umeonesha zipo zaidi ya aina 35.

Vitango bahari, huishi kwa kutambaa kwenye sakafu ya bahari, na kuweka hifadhi na kujisitiri kwenye matumbawe.

 


Maisha ya viumbve hawa, waliokua hawakuwa na thamani kwa zaidi ya karne moja Zanzibar, maisha yao yana mchango mkubwa katika ikolojia ya bahari, hasa katika kuisafisha.

 

Tena imeonekana kuwa, na hili hutokea kipindi wanapokula mchanga, wenye mchanganyiko wa bakteria, mwani na viumbe vidogo vidogo na hatimaye kusafisha.

 

Vina mchango muhimu kwenye mfumo wa ekolojia wa bahari, kwa kusaidia kuzungusha virutubishi na kuvunja vunja mabaki na uchafu wa kioganiki, wa baharini.

KIPI CHAKULA KIKUU CHA VITANGO BAHARI?



Wataalamu mbali mbali wa ndani na wale wanaoandika tatifi, wanakubali kuwa, moja ya chakula kikuu cha vitango bahari, ni mabaki ya viumbe vidogo.

Aina nyingine ni viumbe vidogo vya baharini, kama planktoni na bakteria, ingawa hata chembe chembe za kikaboni, zilizochanganyika na mchanga wa baharini nazo hula.

AINA ZAKE

Tafiti zinaonesha duniani kuna aina nyingi za vitango bahari, ingawa kwa sasa, wanasayansi wamegundua na kuelezea zaidi ya aina 1,250 tofauti.

 Kwa mfano vipo aina ya ‘dendrochirotida’ nyenye umbo la miti, hutumia kukusanya chembe ndogo za chakula, ambao hupatikana katika kina kirefu cha bahari.

Aina ya ‘holothuriida’ ambapo huwa ni kundi kubwa lenye spishi nyingi, zinazojulikana kibiashara, ambapo hutambuliwa kwa mikia mirefu,

Kwa Zanzibar, wanasayansi na watafiti wamebaini kuwa kuna aina kadhaa za vitango bahari zinazopatikana, hasa katika maeneo ya pwani yenye miamba na mchanga.



Ingawa idadi kamili ya spishi zote, bado inachunguzwa, tafiti zinaonyesha kuwepo aina 30 hadi 40 zinazojulikana.

Na kati ya hizo, aina nane hadi 10, ndizo zinazovunwa au kufugwa hasa kwa soko la Asia.

ZANZIBAR NA MARUFUKU UVUVI WA VITANGO BAHARI

Marufuku ya uvunaji wa majongoo bahari Zanzibar ilianza kutekelezwa rasmi mwanzoni mwa miaka ya 2000, baada ya tafiti kuonyesha kupungua kwa kasi kwa spishi baharini, kutokana na uvunaji kupita kiasi.

Kwa wakati huo, serikali iliweka vizuizi vya uvunaji na biashara ya vitango bahari, ili kulinda rasilimali na kuhamasisha ufugaji, badala ya kuvua moja kwa moja.

Kwa sasa, juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye ufugaji wa vitango bahari, hasa aina ya holothuria scabra’ kupitia vituo vya kuzalisha vifaranga Unguja na Pemba.



Aina hiyo ni maarufu kwa sababu ya thamani yake, kwenye soko la kimataifa, hasa bara la Asia, ambako hutumika kama chakula, na kwa madhumuni ya tiba.

MAZINGIRA YA UFUGAJI WA VITANGO BAHARI

Kunahitaji mazingira maalum ya baharini, ili kukua vizuri na kwa haraka, ambapo kwa kawaida, wanakua kwenye maeneo yenye mchanga, miamba, au matumbawe kwenye kina kifupi cha maji.

Hivyo wataalam wanaekeleza mambo kadhaa ya kuzingatia, ikiwemo kiwango cha maji ya bahari, kwani hupenda kuishi kwenye kina kisichozidi mita 20, ingawa hukua vuzuri kina cha mita1 hadi 5.

Wanashauri kuwa, hali joto ya maji, hupendelea yenye halijoto kati ya nyuzi 25°C hadi 30°C, kwani chini ya hapo, inaweza kuathiri ukuaji wao au hata kifo.

Lakini hata suala la uchafu wa maji, hupendelea yalio safi na yasiyo na uchafu mwingi, ambapo wakulima husisitizwa kusafisa, shamba zao.



 WANAKIKUNDI CHA UFUGAJI

 Tumuombe mola’ ni wanakikundi cha wanawake na wanaume, kipo Makangaale wilaya ya Micheweni Pemba, wanatarajia kujipatia shilingi milioni 20 mwishoni mwa mwaka huu.

Wananchi hawa, sasa wamechangamkia ufugaji wa vitango bahari, na fedha hizo wataziingiza ikiwa watafanikiwa kuuza.

Hii ni baada ya kuekeza vifaranga vyenye thamani ya shilingi million 1.6 mwaka jana, wakisubiri muda mfupi sasa kuvuna.

Fedha hizo, ni uwekezaji wa vifaranga 3,300, walivyovinunua kwa shilingi milioni 1,650,000 wastani wa shilingi 500 kila kimoja.

Wanasema kati ya vifaranga hivyo, wanatarajia kuvuna vitango yaliokwisha komaa 2,500 na kisha kila moja kukiuza kwa bei ya shilingi 8,000 na kujipatia shilingi milioni 20.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Hator Hassan, anasema haiwezekani kuotesha vifaranga vya 3,300 kisha kuvuna kama vilivyo.

‘’Zipo changamoto kama za kufa na hasa wakati wa usafirishaji wa vifaranga kutoka eneo moja kwenda bwawani, wizi na wingine kufa kabla ya kufikia kukomaa,’’anafafanua.

Kumbe mara ya kwanza, wakati wanaanza kazi hiyo, walitumia shilingi milioni 1,000,000 kwa ununuzi wa vifaranga 1,000.

Ingawa hatimae, walivuna vitango 340 na kujipatia shilingi milioni 1.7, baada ya kuviuza vikiwa vibichi.

Hawakula hasara, ingawa hawakuvuuka lengo lao la kujipatia zaidi ya shilingi milioni 5, kama sio kujitokeza changamoto hizo.

‘’Kama sio changamoto ya vifaranga kufa au kuibiwa wakiwa ndani ya bwawa letu, hata ule mwaka 2021 wakati tunaanza, tungejipatia faida ya shilingi milioni 4,’’anafafanua.

Hata mwaka 2023, walitarajia kujipatia faida ya shilingi milioni 9, ingawa hatimae, walipata shilingi milioni 1.5.

Tayari wanakikundi hao, wameshafuga mara mbili, tokea waanze kazi hiyo mwaka 2021, na kutumia gharama ya shilingi milioni 3.1 kwa ununuzi wa vifaranga 4,000.

Kwa kwa sasa wanasubiria hadi mwishoni mwa mwaka huu, na ikiwa vifaranga walivyovitia ndani ya bwawa hilo, havitapata changamoto ya wizi na kufa, hawana wasiwasi wa kuvuna shilingi milioni 20.

Mwanachama Hamad Omar Hamad, anasema wamekua wakibadilisha maisha yao, kupitia kazi hiyo, ikiwemo kujihakikisha fedha za matumizi.

‘’Ni kweli kabla ya kuanza kazi hii ya ufugaji wa vitango bahari, sikuwa na uhakika wa wapi naweza kujipatia fedha za haraka, ingawa kwa sasa nnapo,’’anasema.

Akawageukia wafadhili, kuzitatua changamoto zao, ikiwemo kuwapatia boti dogo kwa ajili ya doria, viatu vya kuvulia, ili kuepusha hasara za miguuni.

Afisa Ustawi mkoa wa kaskazini Pemba Nassra Massoud Sanani, anakifahamu kikundi hicho, na amekuwa akiwaunganisha na wadau mbali mbali wakiwemo FAWE- Zanzibar.

FAWE wamekuwa wakifanyakazi na taasisi kadhaa za kimataifa kama UN-Women na wameshaanza kuwapatia mafunzo.

Afisa Miradi FAWE -ofisi ya Pemba Hija Hamad Issa, anasema hivi karibuni, walikuwa na mafunzo ya siku nne ya mnyororo wa biashara, ambapo mwakilishi wa kikundi hicho, alishiriki.

‘’FAWE unao mradi wa pamoja, ambao unawaangalia wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, majongoo bahari, migomba, ndizi na mihogo ili kuwa wabunifu,’’anafafanua.

Wamekuwa wakifanyakazi kwa karibu na UN-Women katika mradi huo, ambao wapo wajasiriamali 20 wa wilaya za Wete na Micheweni, wameshanufaika.

Mwakilishi wa shirika la kimataifa la UN-Women Tanzania Emile Kivugo Mwakafundu, anafafanua kua mradi huo, unawalenga wajasiriamali wa mazao ya baharini na nchi kavu.

Mradi huo wa miaka mitatu, utamalizika mwakani, ambao lengo ni kuona wajasiriamali hao, wanaziongezea thamani bidhaa zao.

Tena kupitia wadau wao FAWE- Zanzibar wanawafundisha namna ya kutoziuza bidhaa zao, kama walivyozivuna na badala yake, wazisarifu.

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, katika kuimarisha ufugaji wa zao hilo, kwa kushirikiana na Kampuni ya Zanzibar Marine Hatchery, ilizalisha vifaranga milioni 1.5.

Kati ya hivyo 80,000 vimegawiwa kwa wafugaji wa Unguja na Pemba na vyingine 70,000 kwa ajili ya biashara na uzalishaji.

Eneo jingine, sekta ya uvuvi imechangia katika pato la taifa, umeongezeka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 5.7 mwaka 2024, ambapo sekta hiyo imekua kwa asilimia 14.2 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2023.

Ambapo taarufa za wizara hiyo zinaeleza kuwa, ongezeko hilo linatokana na hatua mbalimbali za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi, kwa kuwawezesha wavuvi, wakulima wa mazao ya baharini, kwa kupatiwa zana za kisasa.

 

                       Mwisho

 

Comments