By
PEMBA TODAY
NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR
Katika harakati za uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, wanawake wamekuwa miongoni mwa vikosi vyenye ushawishi mkubwa katika kampeni.
Kutoka kuwa mashabiki wa pembeni hadi kuwa viongozi wa kampeni, wagombea, na waratibu wa mikutano, wanawake sasa wanathibitisha nafasi yao katika ujenzi wa demokrasia ya kisasa.
Vyama vya siasa vinatofautiana kwa kiasi kikubwa katika namna vinavyoshirikisha wanawake kwenye kampeni zao, lakini kwa ujumla, taswira ya mwaka huu inaonyesha mwelekeo chanya licha ya vikwazo lukuki.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza rasmi kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu Zanzibar tarehe 11 Septemba 2025 , Kampeni hizo zitaendelea hadi 27 Oktoba 2025 Zanzibar kabla ya siku ya kupiga kura.
Tume hiyo imekamilisha uteuzi wa wagombea kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ambapo Wagombea wa Urais wa Zanzibar 11, wagombea wa Baraza la wawakilishi 484 ,wagombea wa Udiwani 341.
Katika uzinduzi mkuu wa kampeni, chama Cha Mapinduzi CCM kilianza kufungua rasmi kampeni Zanzibar mnamo 13 Septemba 2025.
Katika harakati hizo mgombea wa urais kwa tiketi hiyo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa serikali yake itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi.
“Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu bila ushiriki sawa wa wanawake katika maamuzi ya kitaifa,” Amesema Dkt Hussein
Dk.Mwinyi amesema anatambua watu wengi wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi na kwamba awamu ijayo ataweka fungu kubwa zaidi ili kuhakikisha kila kundi linafikiwa.
"Tutawafikia wote katika uwezeshaji ninatoa ahaadi kwenu kuwa tutawafikia makundi yote kipindi kilichopita tulitoa sh.bilioni 96 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi tumefanya kwenye sekta ya uchumi wa buluu yaani wavuvi,wakulima wa mwani,wajasiriamali wadogowadogo , ,bodaboda,"Amesema Dk Mwinyi
Kampeni za mwaka huu zimeonyesha picha tofauti, wanawake wakiongoza misafara, wakizungumza majukwaani, na wakitumia mitandao ya kijamii kuwasilisha hoja kwa ufasaha. Ujasiri huu umevutia vijana wengi na kuleta hamasa mpya katika siasa za Zanzibar.
Huku wakiwa wameshika bendera zao, wamejivika ujasiri, na kuingia majukwaani, kwa ajili kuthibitisha kwa vitendo kuwa wakipewa nafasi, wanaweza kung’aa zaidi ya vile jamii ilivyowahi kufikiri hali hii ni tofauti na kampeni za miaka iliyopita.
Mwaka huu wanawake wamekuja na ajenda zenye mguso wa moja kwa moja kwa wananchi, elimu bora, afya kwa wote, usawa wa kiuchumi, uwezeshaji wa vijana, na ulinzi wa mazingira.
Wagombea kama Laila Rajab Khamis ambae anagombea nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha NCCR-Mageuzi , Chumu Juma mgombea makamu mwenyekiti taifa wa Chama Cha Alliance for African Federal Party (AAFP) na mgombea Ubunge wa Jimbo la Makunduchi kwa tiketi ya ya Chama Cha Mapinduzi CCM ,Wanu Hafidhi Ameir wamekuwa mstari wa mbele kutetea sera zinazolenga kujenga jamii yenye fursa sawa kwa wote.
Katika mikutano yao ya kampeni, wamekuwa wakisisitiza kuwa wanawake si wa kutazamwa tu kama wapiga kura, bali kama viongozi wanaoweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wa mgombea urais wa Zanzibar wa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi Laila Rajab Khamis katika kampeni zake amesema akipata ridhaa ya wananchi , ndani ya siku 100 za kwanza viwanda vitakuwa tayari kuanza kujengwa kwa ajili ya kuwapatia ajira vijana.
“Kama tutapata ridhaa ya wananchi , ndani ya siku 100 za kwanza viwanda vitakuwa tayari kuanza kujengwa. Tunataka vijana wa Zanzibar wawe na ajira za uhakika na wachangie maendeleo ya taifa leo”Amesema Laila akiwa kwenye kampeni katika kiwanja cha kibanda maiti.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Wanawake katika sheria na maendeleo Afrika (WiLDAF) Zanzibar, zaidi ya wanawake 300 wamepata mafunzo ya kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka huu, na wengi wao wamejipanga kushiriki kikamilifu katika kampeni za ngazi zote , kuanzia udiwani, ubunge hadi uwakilishi.
Kwa upande wa mgombea ubunge wa jimbo la makunduchi wa ticketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Wanu Hafidhi Ameir wakati wa kampeni amesema ,ameanzisha na kusimamia mafunzo kwa viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ngazi ya matawi, wadi, jimbo na wilaya ili kuwajengea uwezo viongozi wanawake kwa kujifunza kuongoza kampeni, kujitokeza kwa nafasi za uongozi, na kujua wajibu wao ndani ya chama.
" Kuhakikisha huduma za afya za wanawake kliniki za afya ya uzazi, huduma za mama mjamzito, uchunguzi wa saratani zipo karibu na rahisi kufikiwa jimboni Makunduchi." Amesema Wanu akiwa kwenye kampeni huko Makunduchi Septemba 29 2025
Na kwa upande wa mgombea uwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Asiata Said Abubakar kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) wakati akihutubia katika kiwanja cha mjeru kisiwani Unguja amesema ,watahakikisha wanaendeleza miradi ya kiuchumi kwa lengo la kuwafungulia fursa vijana.
“ Uchumi wa Zanzibar hauwezi kukua kama vijana wetu hawana nafasi ,tumechoka kuona vijana wakiwa watazamaji wa maendeleo”. Amesema Asiata
Wananchi nao hawakuwa nyuma katika kuwaunga mikono wagombea hao kwenye kampeni zao.
“ Tumezielewa ahadi za mgombea urais wa Zanzibar Laila kuhusiana na ujenzi wa viwanda na kuboresha huduma za afya , tumepata matumaini kuwa utekelezaji wa sera hizi utaongeza ajira kwa vijana “.Amesema Juma Mohameed wakati akisikiliza kampeni za mgombea laila huko kibandamaiti.
“ Wananchi wa jimbo la makunduchi, tumeonesha kuridhika na uteuzi wa Wanu Hafidh kama mgombea ubunge kwani yeye ni kiongozi mzoefu na mwenye ufanisi katika kuleta maendeleo kwenye jimbo letu.” Amesema khamis Ali wakati akisikiliza kampeni za mgombea Ubgunge Wanu huko Makunduchi.
“ Tunamkubali sana Asiata Said kwani yeye anajali masilahi ya wananchi wa jimbo la kikwajuni na anaweza kuleta mabadiliko katika sekta ya ajira.” Amesema Asha
Mashirika ya wanawake Zanzibar yamepongeza muamko huo ikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA- ZANZIBAR imetambua mchango wa wanawake 13 wanaotegemewa kugombea nafasi ya urais na umakamu wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 sawa na asilimia 36 ya wagombea wote 36 walioteuliwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) kwa ngazi hizo mbili.
Mashirika hayo yamekuwa kiungo muhimu katika kuongeza mwamko huu. Kupitia miradi kama SWIL ambao mradi wa kuimarisha wanawake katika uongozi na demokrasia (Strengthen Women in Leadership ,wanawake wengi wamepata mafunzo ya kampeni, ujasiri wa kuongea hadharani, matumizi ya mitandao ya kijamii, na uelewa wa sheria za uchaguzi.
“Tunaona huu ni wakati muhimu katika historia ya siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Idadi ya wanawake 13 kati ya wagombea 36 wa urais na umakamu wa rais ni matokeo ya kazi kubwa ya miaka mingi ya kuwawezesha wanawake kupitia miradi kama SWIL. Hii inaonyesha kwamba wanawake sasa hawako nyuma tena, wanajiamini na wako tayari kuongoza,” amesema Mkurugenzi wa TAMWA–Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps

Comments
Post a Comment