NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MGOMBEA Uwakilishi Jimbo la Mtambile kwa
tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi Wahid Khamis ‘Shoton’, amesema nia yake ni
kuziimarisha huduma za kijamii, ikiwemo maji safi na salama, kama akipata ridhaa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema
anachohitaji ni kupata ridhaa, kutoka kwa wananchi wa jimbo hilo, kwani nia
yake ni tbabiti.
Mgombea huyo alieleza kuwa, huduma ya maji safi na
salama, anaiona imekuwa ya kudorora kwa baadhi ya vijiji jimboni humo.
Alieleza kuwa, eneo ambalo anataka kuanza nalo ni
kijiji cha Kaani Kengeja, Majenzi, Muwanda
Mtambile ili kuona wananchi na hasa wanawake wanakuwa na muda wa kufanya kazi
nyingine, badala ya kushughulikia huduma hiyo.
‘’Nimechukua fomu ya kugombea nafasi ya Uwakilishi
jimbo la Mtambile, maana mimi ni mwanajamii, ninayeumwa na huduma za wananchi,’’alieleza.
Mgombea huyo alieleza kuwa, jingine ambalo anatamani
kuwafanyia wananchi wake, ni kuwawezesha kiuchumi vijana na wanawake, kwa njia ya
mikopo, isiyo na riba.
Alieleza kuwa, kwa aina ya mifumo ya wananchi wa
Jimbo la Mtambile, ili awasaidie ni kuwapatia mikopo isiyo na riba.
Aidha Mgombea huyo wa Uwakilishi wa Jimbo la Mtambile kwa chama cha NCCR-Mageuzi Wahid Khamis ‘Shoton’ alisema katika Ilani yao, kwanza Tanzania, itikadi ya chama baadae.
‘’NCCR-Mageuzi inaamini kuwa, Tanzania kwanza itikadi ya chama baadae, wakiamini kuwa bila ya Tanzania, vyama visingekuwepo,’’alifafanua.
Hata hivyo, alisema kama akipata tena ridhaa,
atashirikiana kwa karibu na wananchi, ili kuona Jimbo hilo linapiga hatua kubwa,
ya maendeleo.
Alifafanua kuwa, bado Jimbo hilo linahitaji mtu kama
yeye, ili kuyatafuta makundi kama ya watu wenye ulemavu, ili kuyawezesha
kiuchumi.
‘’Iwapo wananchi wa Jimbo la Mtambile, wataniona
ninafaa kushika nafasi hii, nikifanikiwa pia kundi la watu wenye ulemavu, nitahakikisha,
nalisaidia kiuchumi,’’alifafanua.
Hata hivyo, Mgombea huyo aliwataka wananchi wa jimbo
hilo, kuendelea kuilinda amani na utulivu uliopo, ili kura ifanyike kwa amani.
Alieleza kuwa, yapo mataifa kwa sababu ya vurugu ya
uchaguzi, sasa wananchi wenyewe hawayakai, hivyo kwa Tanzania hilo, aliomba
lisitokezee.
‘‘NCCR-Mageuzi inaamini, ili uchaguzi ufanyike kwa
amani, kila mwananchi ahakikishe hawi sehemu ya machafuko, kwani ikikosekana
hakuna linaloweza kufanyika,’’alifafanua.
Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Mtambile, walisema
wanaimani naye, na hasa kwa vile ni mgombea wanaeishi nae kila siku.
Mmoja kati ya wananchi hao Ali Mohamed Juma wa Mtambile,
alisema ni miongoni mwa wagombea ambao wanaishi ndani ya jimbo hilo.
‘’Mgombea wa NCCR-Mageuzi wa jimbo letu la Mtambile, kwa nafasi ya Uwakilishi, anafahamika kitabia, mwenendo, na yeye bahati nzuri, anaishi hapa hapa,’’alifafanua.
Nae Mwanaisha Haji Kassim wa Kengeja, alisema aina
ya mgombea ambae NCCR-Mageuzi wamemsimamisha, anazo sifa zote za kuwa kiongozi.
‘’Amekuwa akishirikiana nasi hata kabla ya kugombea nafasi
hii, tena ni mcheshi na tunamuona anafaa kuwa Mwakilishi wetu,’’alisema.
Kwa upande wake Aisha Omar Twaha, alifafanua hata
kama chama chao cha NCCR-Mageuzi hakionekani kuwa na wafusia wingi, lakini aliwaomba
kura wananchi wote.
Uchaguzi mkuu wa saba wa vyama vingi nchini,
unatarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, ni baada ya kuzinduliwa kwa kampeni
Septemba12.
Zanzibar yapo majimbo
50 ya uchaguzi ambapo kwa Pemba, yapo 18, likiwemo la Mtambile, Mkoani, Kiwani,
Chambani, Chonga, Ziwani, Wawi, Ole, Pandani, Micheweni, Wete, Mtambwe, Konde,
Gando, Kojani, Wingwi na mingine.
Mwisho





Comments
Post a Comment