NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
OKTOBA
29 mwaka huu, Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa saba wa vyama vingi tokea
kuasisiwa mwaka 1995.
Mpaka sasa matayarisho
mbali mbali yanaendelea kufanyika, kuanzia kwa wananchi, vyama vya siasa tume
ya uchaguzi pamoja na serikali kuu.
Kuelekea siku hiyo, wadau wa haki za
watu wenye ulemavu wanaendelea kulilia mazingira rafiki ya uchaguzi kwa watu
wenye ulemavu.
Kwani sensa ya watu na makazi ya mwaka
2022 imeweka wazi kuwa, Zanzibar ina takriban asilimia 11.4 ya kundi hilo.
Matokeo hayo ya sensa, yanafafanua kuwa
aina ya ulemavu unaoongoza ni wa uoni, ambao unachukuwa asilimia 3.6 ya jumla
ya watu wenye ulemavu.
Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema
jumla ya watu 717,557 wameidhinishwa kupiga kura mwaka huu, na kati yao 8,021
ni watu wenye ulemavu.
Hivyo ni muhimu kwao kuwekewa
miundombinu rafiki katika vituo vyote vya kupigia kura, ikijumuisha majengo
pamoja na vifaa.
Wenyewe wanasema, lazima mazingira hayo
yatiliwe maanani, kwa uhitaji wa aina zote za ulemavu, ili kuhakikisha watu
wote wanapata haki yao ya msingi ya kupiga kura.
WATU WENYE ULEMAVU
Said Saleh Sultan wa Mtambile Pemba
mwenye ulemavu wa viungo anasema, mazingira rafiki kwao katika uchaguzi ni kuhakikisha
vituo vya kupigia kura vinaweza kufikiwa.
Anaeleza ufikiwaji huo ni pamoja na
kuweka vituo kwenye sehemu ambazo hazina milima na zenye miundombinu jumuishi,
itakayo wawezesha wao kupata ushiriki mpana.
“Mazingira
rafiki kwetu ni kuwekewa vituo vya kupigia kura, katika sehemu zisizo na
milima, pamoja na zenye miundombinu jumuishi, tutakazoweza kufika tukiwa na
viti mwendo ” ,anasema.
Rehema Juma Makame wa Kukuu Kangani Pemba
mwenye ulemavu wa uoni anasema, miundombinu rafiki ya kupigia kura kwao, ni
kuwepo kwa karatasi za nukta nundu vituoni.
Adinan Khamis Juma wa Chake Chake mwenye
ulemavu wa uziwi anasema, ujumuishi wao katika uchaguzi ni kuwepo kwa wakalimani wa lugha ya alama
katika vituo vya upigaji kura.
Anaeleza kuwa, wakalimani hao
watarahisisha mawasiliano kwenye maeneo
ya kutoa huduma zinazo husu upigaji kura.
Saleh Khamis Khalfan wa Mtambile ambae
ana ulemavu wa ngozi anasema, mazingira
jumuishi kwa wenye ulemavu wa aina yake,
ni kuwepo foleni kwa ajili yao.
Anaeleza kuwa, utaratibu huo utasaidia
kupunguza muda wa kukaa foleni, ambazo mara nyingi hupangwa katika mazingira
hatarishi.
Anasema maumbile ya ngozi zao hayahimili
jua kali hasa kwa muda mrefu, ambalo linaathari kubwa kwao.
“Sisi wenye
ulemavu wa ngozi, mazingira rafiki kwetu katika upigaji kura ni kuwepo foleni
maalum kwa ajili yetu, ili kupunguza muda wa kusubiria juani”, anafafanua.
TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR
(ZEC)
Mkuu wa Mkurugenzi wa Elimu ya Wapiga
Kura na Mawasiliano kwa Umma wa ‘ZEC’ Juma S. Sheha anasema, wamejipanga
kuhakikisha watu wenye ulemavu na mahitaji maalum, wanashiriki ipasavyo katika uchaguzi
mkuu.
"ZEC imeandaa vitambulisho maalum kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo watu wenye ulemavu, ili kuwapa kipaumbele wanapofika katika vituo vya kupigia kura, "anaeleza.
Hatua hizo zilizochukuliwa hazikuja tu
kama ajali bali serikali, taasisi binafsi na wadau wingine wa kutetea haki za
watu wenye ulemavu, wamekuwa wakilipambania hili kwa namna tofauti.
MIKATABA
NA SHERIA INAELEKEZA NINI
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za
Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006, Ibara ya 29 inazitaka nchi wanachama, kuweka
mazingira rafiki ya watu wenye ulemavu kushiriki katika mchakato wote wa kisiasa.
“Nchi zihakikishe utaratibu wa kupiga
kura, vifaa na nyenzo ni sadifu, vinafikika, vinaeleweka na kutumika kwa
urahisi,” imeeleza sehemu ya ibara hiyo.
TUME
YA HAKI ZA BINAADAMU
Afisa Mfawidhi wa Tume ya haki za binaadamu
na utawala bora Pemba, Suleiman Salim Ahmad anasema, ili kuhakikisha
miundombinu rafiki kwa watu wenyeulemavu wa aina zote, tume hufuatilia mwenendo
mzima wa uchaguzi.
“Sisi
tunafuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi kisha tunatoa mapendekezo kwa tume ya
uchaguzi nini kifanyike ili watu wenye ulemavu wa aina zote wawe katika
mazingira jumuishi,’’ anasema.
JUMUIYA
YA WATU WENYE ULEMAVU
Maryam Mohamed Salum Afisa watu wenye
ulemavu kutoka Jumuiya ya watu wenye ulemavu Pemba anasema, unapokaribia
uchaguzi, jumuiya hutoa mapendekezo kwa
tume ya uchaguzi ili kuhakikisha unakuwa
jumuishi.
Mratibu Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu
Pemba, Mashavu Juma Mabrouk anasema, baraza hukutana na jumuiya za watu wenye
ulemavu na kukusanya maoni yao.
Anasema baada ya kupata maoni hayo, huweka
mapendekezo na ushauri kwa tume ya
uchaguzi, juu ya kuimarisha mazingira, vituo vya kupigia kura.
TAMWA
ZANZIBAR INAFANYA NINI ?
Meneja programu kutoka Chama cha waandishi
wa habari Tanzania TAMWA-Zanzibar Khairat Haji anasema, TAMWA inatoa mafunzo kwa waandishi wa habari, kuhusu
uandishi jumuishi.
Anaeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni
kuhakikisha waandishi wanatambua na kutetea haki za watu wenye ulemavu, katika
nyanja zote.
“Tumetoa mafunzo
ya uandishi jumuishi kwa waandishi wa habari, ili waweze kutetea haki za watu
wenye ulemavu, ikiwemo hii ya mazingira rafiki katika vituo vya kupigia kura,’’
anaeleza.
MWISHO



Comments
Post a Comment