ZANZIBAR
ipo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mashariki mwa Afrika.
Ni miongoni
mwa nchi zinazopata viongozi wake kupitia mchakato wa upigaji kura.
Ambapo kila
baada ya miaka mitano wananchi wake, wenye sifa zilizotajwa kikatiba, hupiga
kura ili kuchagua kiongozi wamtakae.
Mchakato huo
humjumuisha kila mtu, ilimradi awe ametimia miaka 18 na asiwe mwenye changamoto
ya ufahamu ama akili.
Izingatiwe
kwamba, upigaji kura ni haki ya kikatiba ya kila Mzanzibari, kwani katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 7(1) kimetoa haki hiyo.
Kwamba ‘’Mzanzibari
alietimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi
unaofanywa Zanzibar,’’kimefafanua.
Kwa
kulizingatia hilo, Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC, imeidhinisha jumla ya wazanzibari
717, 557 kushiriki katika uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu.
Huku taarifa
kutoka tume hiyo zikieleza kwamba, kati ya hao
watu wenye ulemavu 8,021 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo hapa Zanzibar.
Watu wenye
ulemavu wa uziwi wakiwa ni miongoni mwa wapiga kura hao, wanahaki ya kupata
sera wakati wa kampeni kutoka katika vyama vyao.
WENYEWE
WANASEMAJE?
Fatma Kombo
Omar wa Kengeja Pemba ni mmoja wa watu wenye ulemavu wa uziwi, akiwa na
mkalimani wake anasema, ingawa vyama vyote viko katika mchakato wa kunadi sera,
hadi sasa ni sera za chama kimoja tu, ndio zilizomfikia.
Kumbe vyama
vyingine vilivyo bakia, hupokea sera zao kutoka kwa watu wanaomzunguka na si
kutoka kwa wagombea wenyewe.
“Ingawa
kushiriki katika kampeni ni haki ya kila mmoja, lakini mazingira sio rafiki
kwetu, na hadi sasa ni sera za chama kimoja tu ndio zilizonifikia,’’anaeleza.
Anaona bado
ni vigumu kwao kupata sera za wagombea wote, kama ilivyo kwa watu wingine wasio
na ulemavu wa uziwi.
Adinan
Khamis Juma wa Chake Chake Pemba ni mtu mwenye ulemavu wa uziwi anasema, pamoja
na kuwepo kwa mikataba, sheria na kanuni zinazotaka ujumuishi, ikiwemo siasa,
bado hali si shwari kwao.
Anafafanua kua, amekua akishiriki katika
mikutano hayo, ingawa hakuna anachoelewa na hurudi akiwa hana alichofahamu,
kwani hakuna mkalimani wa lugha za alama.
Hata Zuhura
Haji Mohamed wa Mtambile, anasema wapo wagombea wanao watumia watu wa karibu
wawafikishie sera zao, lakini bado
haitoshi.
“Bado
ujumuishi wetu katika kampeni ni chanagamoto, na baadhi ya wagombea hutumia
watu wetu wa karibu watufikishie sera zao, lakini hatupati ujumbe kamili,”anaeleza.
JAMII
INASEMAJE?
Asia Shaib
Saleh wa Mjimbini Pemba, anasema ujumuishi
kwa viziwi katika kampeni, bado ni changamoto na wanawachagua wagombea
sio kwa kulewa na sera zao.
Anaeleza
kua, jamii ndio inayofanya kazi kuwaeleza sera za vyama tofauti, kazi ambayo ilipaswa kufanywa na wenyewe
wanasiasa.
Saleh Bakkar
wa Kengeja anasema, mara nyingi watu wenye ulemavu wa uziwi, hukataa kushiriki
katika mikutano ya siasa, kwa vile hakuna mazingira rafiki kwao.
“Wenzetu
wenye ulemavu wa uziwi, mara nyingi hawashiriki ipasavyo mikutano ya kampeni,
kwa kukosekana kwa mazingira rafiki kwao, ikiwemo wakalimani wa lugha ya alama,’’anasema.
VYAMA VYA SIASA VINASEMAJE?
Katibu wake
wa CCM mkoa wa kusini Pemba Kajoro Vyohoroko anasema, katika kampeni za mwaka
huu, mikutano yao ya hadhara ya wagombea urais, wameweka wakalimani wa lugha ya
alama, ili kuhakikisha ujumuishi.
‘’Kwa miaka
iliopita, kundi hili hatukulizingatia ipasavyo, ingawa mwaka huu mikutano yote
ya kampeni za wagombea wa urais wa Tanzania na Zanzibar, tumeweka wakalimani wa
lugha ya alama,’’anafafanua.
Mohamed
Abdallah ni Mwenyekiti wa chama cha ACT –Wazalendo mkoa wa kusini Pemba
anasema, hadi sasa chama hicho hutumia watu wa karibu, na watu wenye ulemavu wa
uziwi katika kufikisha sera.
‘’Kwasasa chama hakina mazingira rafiki kwa
watu wenye ulemavu wa uziwi, katika kuhakikisha wanapata sera za chama, na
badala yake tunawatumia watu wao wa karibu,’’ anaeleza.
MIKATABA/SHERIA
NA SERA
Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa watu wenye uleamu (CRPD,2006) Ibara ya 9, inazitaka nchi wanachama, zihakikishe zimeweka
utaratibu wa watu wenye ulemavu, kufikia huduma zote pamoja na mawasiliano na
teknolojia.
Malengo 17
ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya mwaka 2020/2030 yenye shabaha 169, shabaha 11
inagusia watu wenye ulemavu wa aina zote.
Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 12 (1) kimeweka wazi kua, watu wote
ni sawa mbele ya sheria.
Huku mabano (4)
na (5) vikieleza kua, hakuna mtu yeyote atakae baguliwa kwa utaifa wake,
kabila, jinsia, ulemavu, pahala alipotokea, muelekeo wa kisiasa, rangi au dini.
Ndio maana Sheria
ya watu wenye ulemavu nambari 8 ya Zanzibar ya mwaka 2022, kifungu chake cha 29
kinaeleza umuhimu wa watu wenye ulemavu, kufikia miundombinu pamoja na taarifa,
mawasiliano na haki zote za msingi.
NINI ATHARI
YAKE?
Zainab
Mohamed Ali wa Chake Chake, mwenye ulemavu wa uziwi anasema, moja ya athari
zinazojitokeza ni kutowachagua viongozi wawatakao.
Afisa Mfawidhi
Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Pemba Suleiman Salim Ahmad anasema,
ni watu hao kukosa haki yao ya kikatiba
ya kupiga kura.
NINI
KIFANYIKE?
Yumna
Mbarouk Yussuf na Mbarouk Ali Juma wa Pemba wanasema, yvama vyote vya siasa
viandae mazingira rafki kwa kuweka wakalimani wa lugha ya alama katika mikutano
yote.
Katibu Mkuu
wa Chama cha Viziwi Zanzibar ‘CHAVIZA’ Yahya Hamed Seif anasema, ili
kuhakikisha ujumuishi wao katika kampeni za vyama vya siasa, vyama vibuni njia
za kuwajumuisha.
Kaimu
Mratibu wa chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA-Zanzibar Ofisi za Pemba
Amina Ahmed Mohamed anasema, ni vyema vyama vyote vya siasa kuweka wakalimani
wa lugha ya alama.
Jingine, ni
kwa wadau wa haki za watu wenye ulemavu, kuendelea kupaza sauti, ili sheria ya
uchaguzi na ile ya vyama vya siasa iwe na kifungu lazimishi juu ya kuwatumia
wakalimani.
MWISHO


Comments
Post a Comment