HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
SARATANI ya matiti (breast
cancer) inaendelea kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha
vifo vya wanawake duniani kote.
Hali hii ni ya
kutia wasiwasi zaidi katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo, ambapo idadi
kubwa ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa
huo.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kuchelewa kupata huduma za
uchunguzi na tiba kunachangia, kwa kiwango kikubwa vifo vinavyotokana na
ugonjwa huu.
Takwimu za
kimataifa za mwaka 2022 zilizotolewa na Global Cancer Observatory
(GLOBOCAN), na ile ya wizara ya Afya ya mwaka 2024 zinaonyesha kuwa,
saratani ya matiti ni ya pili kwa wanawake baada ya saratani ya shingo ya
kizazi.
Takribani asilimia
14.4 ya wagonjwa wapya wa saratani nchini, ni wa saratani ya matiti, hali
inayoifanya kuwa moja ya magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo.
Shirika la Afya
Duniani (WHO), linasema takribani wanawake milioni 2.3 waligundulika
kuwa na saratani ya matiti mwaka 2020, na kati ya hao zaidi ya 685,000 walifariki
dunia.
Hii inafanya
saratani ya matiti kuwa aina ya saratani inayoathiri wanawake kwa kiwango
kikubwa zaidi duniani.
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Tanzania ya mwaka 2023, inaonesha kuwa
zaidi ya wanawake 3,500 waligunduliwa na saratani hiyo.
Asilimia 70 ya
wagonjwa hao walifika hospitalini wakiwa katika hatua ya tatu au ya nne ya
ugonjwa, hatua ambazo nafasi ya kupona huwa ndogo.
WATAALAMU WA AFYA
Mratibu wa vituo vinavyotowa huduma ya kinga Pemba, dk.
Rahila Salim Omar anasema wanawake wengi hufika hospitali wakiwa
tayari katika hatua za juu za ugonjwa.
Anasema saratani ya matiti imeendelea kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoongoza
kusababisha vifo kwa wanawake duniani.
Na Zanzibar kama
sehemu ya dunia na inayokaliwa na wanawake, wala haijasalia nyuma katika
changamoto hiyo.
Anabainisha kuwa, ongezeko
la visa vya ugonjwa huo linaashiria haja ya kuchukua hatua madhubuti za kinga,
uchunguzi wa mapema, na elimu endelevu kwa jamii.
Ongezeko hilo linahusishwa na mabadiliko ya maisha, lishe
duni, na kuchelewa kufika hospitalini kwa uchunguzi.
Daktari wa masuala ya akina mama hospitali ya Chakechake Dk. Rahila
Salim Omar anasema wanawake wasiopenda kunyonyesha wako hatarini kupata
saratani ya matiti.
Anaelezea kesi nyingi zinazoripotiwa ni hatua (stage) ya
pili, jambo ambalo linachangia ugumu wa matibabu.
“Ni vyema unapojigunduwa na maumivu ya ziwa, maboje ukimbilie
spitali kwani tatizo linapoonekana mapema hutibika,’’anafafanua.
Fatma Hassan Khamis
msimamizi wa vituo vya huduma rafiki kwa vijana Pemba, anasema saratani ya
matiti ni ugonjwa unaoweza kutibika endapo utagundulika mapema.
Huku akitaja
changamoto ya uchelewaji wa huduma inayosababisha idadi kubwa ya vifo, inaweza
kuzuilika.
“Ushirikiano kati
ya serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, na jamii kwa ujumla,
unahitajika ili kuweka mazingira bora ya uchunguzi,’’anasema.
SABABU NA
HATARI YA SARATANI
Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2023, lilianisha kuwa, moja ya sababu
kuu za saratani ya matiti ni pamoja na urithi wa vinasaba.
Nyingine ni,
matumizi ya homoni kwa muda mrefu, unene kupita kiasi, na mtindo wa maisha
usiofaa.
Kadhalika, wanawake wanaopata hedhi mapema au kukoma hedhi kwa kuchelewa, kutonyonyesha,
na kutumia pombe mara kwa mara, wako hatarini.
“Utafiti unaonesha wanawake wanaonyonyesha kwa muda mrefu,
wanapunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya kupata saratani ya matiti,”
anafafanua dk. Hidaya Omar, mtaalamu wa afya ya jamii wizara ya Afya Zanzibar.
Daktari wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Abdalla Mzee Pemba Mohamed
Omar, anashauri wanawake kuwa makini na mabadiliko yoyote katika matiti yao.
Akitaja mabadiliko hayo anasema ni pamoja na uvimbe usioumiza,
ngozi kubadilika rangi, chuchu kutoa majimaji yasiyo ya kawaida na maumivu
yasiyo ya kawaida.
“Dalili hizi hazimaanishi kila mara kuwa ni saratani, lakini ni muhimu kumuona
daktari mapema,” anashauri.
MASHUHUDA WA UGONJWA
Massoud Ali Massoud wa Chakechake anasema sababu ya mama
yake mzazi kuumwa na ziwa, hadi hatua ya kukatwa na kupoteza maisha ni
kuchelewa kufanya vipimo.
“Naamini mama angewahi mapema kufika hospitali angepona talianza
kuumwa mwaka 2005 hadi 2008, ndipo alipofanyiwa matibabu baada ya kugundulikana
kuwa ana saratani ya matiti,”anambuka.
Asha Mohamed Kombo wa Mkanyageni Mkoani, anasema baada ya
kuona ziwa lake limefanya ugumu (maboje) kwa ndani na mtoto wake hataki kunyonya,
aliwahi hospitali kwa uchunguzi.
“Kumbe ilikuwa ni saratani, ingawa nilikuwa na hofu baada ya
kumsikia daktari kuwa awahiwe haraka isijeikafikia hatuwa ya kukatwa ziwa lote,’’anasema.
Aziza Juma wa Machomane nae anasema, alifanyiwa upasuaji wa ziwa
katika hospitali ya Chake chake, baada ya kuwa na boje, ingawa hakuwa na
maumivu.
Fatma Sharif wa Kengeja, anasimulia mwaka mmoja uliopita,
aliumwa na ziwa ila hakukaa nyumbani, badala yake alikimbilia kupata matibabu.
Mume wa Fatma anasema, hajawahi kumsikia mke wake kulalamikia
kuumwa na ziwa hapo kabla, ingawa mara tu baada ya kujifungua hali hiyo ikaanza
kujitokeza.
Akisimulia hali iliyomfika mke wa rafiki yake Abdalla Saidi wa
Wawi, baada ya kuumwa ziwa alifanya woga kukimbilia hospitali ziwa lilikatwa.
JAMII INASEMAJE
Rehema Kassim wa Kiwani anasema aliwahi kusimuliwa na bibi yake
mwaka 1998, kuwa mama asiponyonyesha mtoto wake inavyotakiwa ni rahisi kuumwa
na ziwa.
Ali Juma anasema wanawake wengi huathiriwa na saratani ya matiti,
ila huwa hawajui.
NINI KWANI SARATANI YA MATITI?
Ni mabadiliko ya chembechembe hai, zilizopo kwenye matiti,
saratani hii kwa kawaida, haina dalili katika hatua ya mwanzo.
Uchunguzi wa awali ndio utakaowezesha kugundua ugonjwa, katika
hatua ya mabadiliko yaletwayo na saratani.
Kuvimba katika titi au kwenye makwapa, mabadiliko ya umbo na
ukubwa wa titi, kutokwa na majimaji au damu katika chuchu.
MAMBO YA KUZINGATIA WANAWAKE
Wanapaswa kuvunja ukimya, kuondoa aibu, na kuelimishana kuhusu umuhimu wa
uchunguzi mapema.
Wanawake kuwa na utamaduni wa kujikagua matiti kila mwezi, siku chache
baada ya heidhi kumalizika, na kufika hospitalini mara, wanapobaini mabadiliko
yoyote.
Jingine ni jamii kutokuwa na imani potofu ya kutumia dawa za
kienyeji badala ya kwenda hospitali, ambako ndiko unakojulikana tatizo na
hatimae kupata matibabu.
MIKAKATI YA SERIKALI NA WADAU
Wizara ya Afya, imeanzisha programu maalum za uchunguzi wa saratani za
wanawake, ikiwemo kampeni ya “Afya ya Mama, Tumaini la Taifa”.
Kampeni hizi, zinayolenga kuwafikia wanawake katika shehia zote
za Unguja na Pemba na popote walipo.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui anasema, serikali imeimarisha vifaa
vya uchunguzi wa saratani, katika hospitali za Mnazi Mmoja kwa Unguja na
Abdalla Mzee Pemba.
Jingine ni kutoa mafunzo kwa wauguzi na madaktari, kuhusu
utambuzi wa mapema.
“Tunasisitiza wanawake wajitokeze kufanya uchunguzi wa matiti, angalau
mara moja kila mwaka,’’anasisitiza.
Mashirika kama Zanzibar Cancer Foundation (ZCF) na Taasisi ya
Saratani Ocean Road (ORCI), yanaendelea kutoa elimu na huduma za uchunguzi,
bila malipo katika kampeni za kijamii.
Na hili hasa wakati wa mwezi wa Oktoba wa uhamasishaji wa
saratani ya matiti duniani (Breast Cancer Awareness Month).
WHO, linaripoti kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa
wanaopatikana katika hatua za mwanzo, hupata nafuu kamili baada ya matibabu.
MWISHO
Comments
Post a Comment