NA ARAFA MAKAME, PEMBA@@@@
HAPA ni Kiuyu Minyungwini, wilaya ni ya
Wete, mkoa wa kaskazini Pemba, na mbele yangu namuomba mjasiriamali, bila shaka
ni mtu mwenye ulemavu wa viungo.
Niliharakia, kutaka kumjua ni
nani, nilipomkaribia ana nadisha haya kangaa…kangaaa…na wale wa wapenzi wa madira na
vipodozi nipooo.... njooo ujichagulie.
Kauli hizo, zilinifanya nisimame
pembeni kidogo mwa nyumba ya Asha Haji Makame wa Kiuyu, nae mjasiriamali huyo, aligeuka
nyuma ghafla, kwa hamu ya kutafuta wateja na alinifuata.
…..assalama alyekum, baada ya
kuitikia mjasiriamali huyo, alimuuliza bi Asha kua amepata mgeni, na kumjibu ni
mgeni wako.
‘’Au ndio huyo mwandishi wa habari
aliyenipigia simu, juzi kuniambia anakuja, nilijua utachelewa kidogo ndio
maana, nimeanza kutembeza biashara yangu,’’alisema.
‘’Kwani wewe ndio Katija Mbarouk Ali,
nilikua nawasiliana na wewe bila ya kukufahamu, ndio nimekuja kukuhoji,’’alidakiza mwandishi.
Ghafla, baada ya kutua mzigo wa kanga,
madira na vipodozi, kumbe anapokaa Katija ni nyumba moja tu, na kumvuta
mwandishi pembezoni.
MAZUNGUMZO
‘’Mimi ndie Katija Mbarouk Ali, nilienza
kuipenda siasa tokea, mwaka 2016, kwa hamu tu ya kutaka kuwatetea wenzangu.
Akamueleza mwandishi wa kua, safari
yake ya siasa iling’oa nanga miaka tisa iliyopita, baada ya hamu yake ya kutaka
kutimiza ndoto za kuwahudumia wanawake na watu wenye ulemavu.
‘’Ni kweli mwandishi huu ulemavu wangu
sikutaka kuufanya mtaji, wa kuwaomba omba, mtegemezi wa familia na kuonekana
mazigo,’’anasema.
Katija ni mchesi, mchangamfu na
mwenye ulemavu wa viungo, ni mweusi wa wastani, na uso wake saa 24 huwa ni wenye
bashasha.
Hadi sasa anaamini, iko siku atakuwa
mtetezi wa kweli kwa wanawake, jamii na kundi la wenzake wenye ulemavu, akiwa
ndani ya chombo cha kutunga sheria.
Kumbe anaumia ndani ya moyo, kuona
kundi la wanawake na watu wenye ulemavu, kudhalilika kwa kukosa mitaji ya
kujiendesha.
‘’Unajua mwandishi, mimi na uongozi,
mimi na sisasa sasa ni watoto pacha, na tunaorithi pamoja, na sifanyi haya kwa
ajili ya tumbo langu, lahashaa,’’anasimulia.
KATIJA NA UONGOZI
Kumbe, baada ya kuiva akitokea mjumbe
wa mkutano wa wadi wa tawi la Kiuyu Minungwini, sasa ikwa ni mwendo wa kugombea.
Maana kuanzia mwaka 2017 hadi 2019,
aliwahi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa tawi la CCM Kiuyu Minungwini, inagawa
kwa mshangao alikabidhiwa nafasi ya ujumbe.
‘’Hapo nilianza kuulizwa maswali, na
wasionitakia mema wala chama changu, eti wapi na wapi mlemavu kugombea,’’walihoji
watu.
Katija, ambae familia inamuita shujaa
asiyekumbuka kovu za kukatishwa tamaa, kudharauliwa, aligombea tena nafasi ya Mwenyekiti
wa tawi.
‘’Mara iliyofuata mwaka 2017,
niligombea Mwenyekiti tena wa tawi la CCM Kiuyu Minguwini, ingawa nilipewa
nafasi zile tano za kupitia wilaya,’’anasema.
Walishasema wahenga kuwa, zimwi likujualo
halikuli likakumaliza, ndivyo ulivyosadifu msemo huu kwa shujaa Katija.
Ilipofika mwaka 2020, aliibuka tena
kiana na kumuliika bahati yake kwenye viti maalum, tena kwa watu wenye ulemavu.
‘’Hapa tulikuwa wanawake wanne (4),
ingawa pia haikuwa bahati yangu, lakini sikununa wala sikumlau mtu,’’anasema.
Maisha ya Katija na kuusaka uongozi,
ili kuwatumikia wananchi, uliamka tena mwaka 2025.
Si unajua kwa anapoishi Katija, jimbo
lake ni Kojani, hapo dada huyo alijichanga kwa miaka mitano, na kufundika
shilingi 500,000 kibindoni.
Anamueleza mwandishi wa makala, kuwa,
siku ilipofika aliianga familia yake, na kutaka dua na ridhaa hadi wilaya ya
Wete, yalipo makao makuu ya CCM.
‘’Nilizitoa shilingi 500,000 kuchukua
fomu ya kugombea Uwakilishi wa Jimbo la Kojani, huku nikiangalia huruma za
wajumbe,’’anasema.
Hapa alipambana na watia nia 23, wakiwemo
wanawake wanne, ingawa mwenye ulemavu alikuwa peke yake.
Kwa hakika, msuguano wa kukutana na
wajumbe, kwa Katija hakukutana nao, akiamini kama sehemu ya njama ya kumkosesha
nafasi.
Aliona madudu kadhaa, kuanzia kwa
wanachama wa kawaida, wagombea wenzake na watu wingine wa karibu, wakiashiria
maumivu kwake.
‘’Wapo walioniita mlemvau sio kiongozi,
mbona umeacha nafasi za watu wenye ulemavu umekuja jimboni, pesa zako hazina
kazi,’’nadio maneno aliyokumbana nayo.
Anasema akikumbuka tokea, alipokuwa
akiomba nafasi za kugombea Mwenyekiti wa tawi, zaidi ya miaka 10 na haya ya mwaka
2025, hakutetereka.
‘’Unajua ukishatafunwa na simba,
mbwa, kima, paka na kuku, huwa ni jambo la kawaida,’’anasema.
Kwenye kinyang’anyiro hicho, mtia nia
Katija, alifanikiwa kupenya, kuanzia ngazi ya jimbo, wilaya, mkoa na taifa.
‘’Kama binaadamu na mwanamke mwenye
ulemavu, kwa hakika nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Kojani, nilishaanza
kuifikiria,’’anasema.
‘’Siogopi kupambana na wanaume kwenye
kupiga kura, naopa kwenye riadha, kuvuta kamba, kutupa mkuki ama kucheza mpira,
kwa sababu ya ulemavu wangu tu,’’anasema.
Kumbe jasiri huyo anaetamani kuingia
tena jimboni mwaka 2030, kwa nafasi ya ubunge, anachojenga hofu ni kubezwa na
kudhalilishwa kwa maneno.
Mana anasema, baada ya watia 23, na
kisha vikao vya chama taifa kuwarejesha saba, na akiwa mwanamke pekee, anasema
huo ulikuwa mtihani kwa wajumbe.
‘’Tunasema kila siku mwanamke mbele
na hasa mwenye ulemavu, lakini duuuu….wajumbe hawakuliona hilo na leo hii
sikufanikiwa kuwa mwakilishi mteule Kojani,’’anasema.
AKIWA NJE YA SIASA
Katija, ni mjasiriamali wa kutembeza
bidhaa kama kanga, madira na manukato mingine katika shehia ya Kiuyu Minungwini
na vijiji jirani.
Anasema, hapendi hata kidogo kuonekana
mzingo kwa wazazi wake, ingawa hajabahatika ndoa, lakini ndio msaada mkubwa kwa
familia yake kwa sasa.
Alishaanzisha vikundi kadhaa vya wajasiriamali
vya watu wenye ulemavu, ingawa bado hajafanikiwa kutoboa kimaisha.
‘’Unajua, katika kutafuta fursa,
inafika wakati nasema kama vile kushirikiana na watu, ni mbaya maana nia zetu
hazifanani,’’anasema.
Kumbe anakumbuka machungu, baada ya
kuwezeshwa kwa cherhani zaidi ya sita, na aliyekuwa Mwakilishi wa watu wenye ulemavu
Raya Suleiman, ingawa kwa utunzaji mbovu wamerudi tena kwenye umaskini.
Anasema, kama wengikuwa na moyo
unaofanana na tamaa ya kutafuta maisha, leo hii wengekusha kuwa wameshaajiri
wenzao.
FAMILIA YA KATIJA
Mwanache Mkadamu Juma ni mama mzazi
wa Katija, anasema juhudi za kutafuta fursa za uongozi kwa mtoo wake, zimezungurukwa
na changamoto za kiroho.
‘’Hata mimi hufuatwa na kupewa lugha
za kumvunja moyo, mara…..ooooni mlemavu, mara oooo…ataka poteza pesa zake,’’anaelezea
anavyovunjwa moyo mtoto wake.
Anasema, anapokaa au wakati mwingine
kusikilzia redio, hulalamika na kuguna, jinsi wanawake na watu wenye ulemavu,
wanavyoishi kwenye changamoto za kimaisha.
‘’Utaskia, nikipata nafasi ya kuwa Mwakilishi
wa jimbo au viti maalum, ntahakikisha napunguza changamoto za watu wenye
ulemavu,’’anasema.
Fatma Mbarouk Ali ni ndugu wa Katija,
anasema dada yake, anasema bado hapati usingizi wa fofo, hasa anapoona watu
wenye ulemavu wanadhalilishwa.
Ukikakaa nae hadithi zake ni kuwasaidia
wanawake, watu wenye ulemavu na wale maskini, akisema kuwa, inawezekanaje mtoto
kushindwa kwenda skuli, kwa kukosa kiti mwendo.
Anasema, wakati mwingine anaporudi
kwenye mikutano, huandika orodha ya watu wenye ulemavu, ukimuuliza, anasema ana
mpango mkakati.
CCM JIMBO LA KOJANI
Tamimu Omar ni Katibu wa CCM jimbo la
Kojani, anasema, juhudi za kumuunga mkono na kumpa moyo, zinafanyika kila
wakati.
‘’Kwa mfano, tunamuelekeza njia za
kufanya, ili afanikiwe, na kwa hakika ni mwanachama anayepitia changamoto na
hasa akionesha nia tu ya kugombea,’’anasema.
Hilo anasema huchangiwa na mambo
kadhaa, maana Katija ni kijana wa misimamo, hayumbishwi na visenti na ana
maadili ya kijamii na kichama.
Akigusia juu ya watu wenye ulemavu,
anasema CCM katika kuwajali, imeanzisha viti maalum, kwa ajili yao.
‘’Fursa iliyopo, anaweza kugombea,
jimbo, vitu vyao maalum au nafasi ya wanawake au nafasi ya vijana, hayo ndio
mahaba ya CCM kwa makundi ya jamii,’’anafafanua.
WANAHARAKATI
Hidaya Mjaka Ali ni Makamu Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’, anasema bado watu
wenye ulemavu wanakabiliwa na vikwazo kadhaa ushiriki katika uongozi.
Anasema, jamii haijawaamini hata
chembe, kama wanaweza kuwa watetezi wao, maana kama hivyo sivyo, Katija kwa
mwaka huu engefanikiwa.
Amina Ahmed Mohamed ni Kaimu Mratibu
wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania- TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba,
anasema kazi yao ni kuwawezesha wanawake kugombea.
Kwa mfano tulikuwa na mradi maalum wa
kuwawezesha kushika nafasi, na huyo Katija alikuwa mshiriki, lakini bado jamii
haijawaamini.
‘’Na tulianzisha kamati maalum na
wanaume wa mabadiliko, na ilipita vijijini na vitongoji vyote vya Pemba, lakini
bado mfupa ni mgumu,’’anasema.
Kwenye majimbo ambayo tulitarajia CCM
wengemsimamisha mwanake mwenye ulemavu kwa nafasi ya Uwakilishi, tulihisi ni
Kojani, lakini imekuwa tofauti.
Ijapokuwa wapo wanawake kadhaa kwa
sasa waliopitishwa na vyama vyao kugombea nafasi za majimbo kama Wawi, Chake
chake, Chambani, Wete, Konde, Gando bado takwimu ni ndogo.
‘’Maana Pemba, tu tunayomajimbo 18,
ambapo ni sawa na wagombea 36, kwa kila jimbo kwa nafasi ya ubunge na
uwakilishi, takwimu bado haziridhishi kwa wanawake,’’anasema.
Ijapokuwa taarifa za Tume ya Uchaguzi
Zanzibar ZEC, imabainisha, kuwa, wapo wapiga kura wenye ulemavu mchanganyiko 8,021
bado wanaowania majimbo hawajapewa kipaumbele.
JAMII NA WAPIGA KURA
Omar Haji Msanifu wa Kojani, anasema
ngarambe ya kulipata jimbo, bado mazingira yanatawaliwa na mambo kadhaa,
ikiwemo rushwa na umaarufu.
Mwanaisha Hilali Khamis, anasema wanawake
wenyewe, hutengenezwa kuwa maadui kwa wanawake wenzao, na kusabisha ugumu
kufingia jimboni.
NYARAKA ZINASEMA JE HAKI YA KISIASA
Hadithi ya kusikitisha ya Katija, haibebwi
na Sheria ya watu wenye Ulemavu nambari 8 ya mwaka 2022, maana kifungu cha 28 (1)
(e) chenyewe kimetamka haki ya kushiriki, katika shughuli za kijamii, ikiwemo
siasa.
Hata Mkataba wa kimataifa wa haki za
watu wenye ulemavu mwaka 2006, Ibara ya 29 (b) (i), kwamba watu wenye ulemavu,
wana haki ya kujumuishwa kisiasa.
‘’Kushiriki katika asasi za kiraia na zile
zinazojihusisha na masuala ya umma na siasa za nchi, na katika shughuli na
uongozi wa vyama vya siasa, ni haki kwa watu wenye ulemavu,’’umefafanua mkataba.
Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na
kisiasa wa mwaka 1976, ukitaja moja ya haki za kila mmoja ni kushiriki, siasa
bila ya ubaguzi.
Tena hata mkataba wa kimataifa
wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake ‘CEDW’ wa mwaka 1979, ukasisitiza
Ibara ya 7, kwamba lazima hatua
zichukuliwe, kuhakikisha wanawake wanakuwa na ushiriki sawa kwenye ulingo wa siasa.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 21(1), kinasisitiza
kuwa, watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi, kupata
haki mbele ya sheria.
Katija Mbarouk Ali, ambae hayuko kwenye
ndoa ni mkaazi wa shehia ya Kiuyu Minungwini yenye wakaazi 60,23 wanaume
29,14 wanawake 31,09.
Akiwa ni mtoto wa tatu kuzaliwa,
katika familia ya Mbarouk Ali Suleiman yenye watoto wanne, ameshatimiza miaka 35,
tokea alipofika hapa ulimwenguni.
Mwisho


Comments
Post a Comment