Na Mwandishi Wetu, Zanzibar@@@
SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO), imezindua rasmi Muongozo wa Mawasiliano
kati ya Mzazi na Mtoto kuhusu Haki ya Afya ya Uzazi (PCC Toolkit),
unaolenga kuimarisha malezi, mawasiliano, ulinzi na ustawi wa watoto na vijana.
Uzinduzi wa muongozo huo
umefanyika jana katika Hoteli ya Verde na kuzinduliwa na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zawadi Amour Nassor, kwa niaba ya
Waziri wa Wizara hiyo, Anna Athanas Paul.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Zawadi alisema wazazi na walezi wanapaswa kuvunja ukimya katika kujadili
masuala ya afya ya uzazi na watoto wao kwa kutumia lugha sahihi, yenye heshima
na inayozingatia umri wa mtoto.
Alisema watoto na vijana
wanahitaji kupata taarifa sahihi zinazolingana na umri wao ili kuwasaidia
kuelewa mabadiliko wanayopitia, kutambua hatari, kujilinda dhidi ya ukatili na
kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao.
“Tunapozungumzia afya ya
uzazi, hatuzungumzi tu masuala ya kibaolojia, bali pia malezi, maadili,
mahusiano yenye heshima, usalama wa mtoto na uwezo wa kusema ‘hapana’ pale
inapohitajika,” alisema.
“Ukimya hauondoi changamoto, bali huacha nafasi kwa upotoshaji,” alisema, akibainisha kuwa PCC Toolkit itawasaidia wazazi kuzungumza na watoto wao kwa uwazi, kusikiliza bila kutoa hukumu na kujenga mazingira ya kuaminiana.
Aidha, alisema
utekelezaji wa muongozo huo unahitaji ushirikiano wa Serikali, UNESCO,
mashirika ya kiraia, wazazi, walimu, viongozi wa dini na vijana wenyewe, huku
akiipongeza UNESCO na wadau mbalimbali, wakiwemo Katibu Mkuu Abeda Rashid
Abdallah, Mkurugenzi na Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Watoto Mohamed Jabir,
kwa kuchangia maandalizi ya muongozo huo.
Kwa Upande wa Umoja wa
Mataifa kanda ya Zanzibar akizungumza
Naibu Katibu na Mratibu Dorothy Temu Usiri amesema Muongozo huo umezingatia maadili hivyo
wamaimani kwamba Muungozo huyo utawazaidia wazazi kuwa na Malezi bora ya Watoto
hali ambayo itawasaidia watoto kujielewa na kujifahamu mapema.
Akimuakilisha Mwakilishi
Mkaazi wa UNESCO Matias Luhanya amesema Shirika litaendelea kushirikiana na
Serikali kwa ajili ya kutoa elimu na kuleta mabadiko katika Sekta ya Elimu
Zanzibar kwani umepatikana muongozo wa kuwasaidia wazai.
Akizungumza moja kati ya
wazazi Bahati Issa kutoka Kikungwi, Unguja ameishukuru Shirika la UNESCO kwa
kundaa Muongozo huo. Pia ameiomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto kuendelea kutoa elimu dhidi ya muogozo huo kwa kila shehia ili kila
mtu imfikie elimu ya Mawasiliano kati ya Mzazi na Mtoto kuhusu Haki ya Afya ya
Uzazi.
MWISHO

Comments
Post a Comment