WAZIRI ANNA PAUL AZIFARIJI FAMILIA ZILIZOPOTEZA WATOTO MBUZINI, ATOA WITO WA KUIMARISHA ULINZI WA WATOTO
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Paul, leo amewatembelea na kuwapa mkono wa pole familia zilizopoteza watoto watatu kufuatia tukio la kusikitisha la kuzama kwenye bwawa la maji katika eneo la Mbuzini, Wilaya ya Magharibi A, Unguja.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo ya kuwafariji wafiwa, amesema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watoto hao na
inaungana na familia zilizopoteza Watoto wao wapendwa pamoja na wananchi wote
wa Mbuzini katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Amesema
tukio hilo ni pigo kubwa kwa Taifa na limetoa funzo kwa jamii kuhusu wajibu wa
pamoja wa kulinda usalama wa Watoto ni wajibu wa kila mtu katika jamii na sio
wazazipekee.
“ Tukio
hili ni pigo kubwa kwa taifa na linatoa funzo kwa jamii, kuhusu wajibu wa
kumlinda mtoto si la Serikali pekee bali kila mmoja wetu anawajibu wa kumlinda
mtoto kwa kuzuia kila tukio hatarishi” Amesema Waziri Anna.
Aidha
Waziri ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwaelimisha watoto kuhusu maeneo
hatarishi, kufuatilia mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha yao na kutoa
taarifa mapema kwa mamlaka husika pindi wanapobaini uwepo wa hatari, ili kuzuia
matukio kama hayo yasijirudie.
Pia
amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya usalama kwa watoto na kuchukua
tahadhari stahiki katika maeneo yenye hatari, akieleza kuwa watoto ni rasilimali
muhimu ya Taifa inayopaswa kulindwa kwa nguvu zote.
Naye Diwani
wa Wadi ya Bububu ndugu Ramadhani Juma Mkanga amesema tukio la watoto watatu
kuzama na kufariki dunia lilitokea juzi majira ya jioni katika bwawa la Mwanamanja ambapo
Watoto wao walikuwa wakikamata ndege wanopita juu ya maji.
Diwani huyo
aliwataja Watoto waliyofariki akiwemo mtoto Ibrahim Makame Haji (14), Ahmed
Ramadhani Issa (14) na Abdullatif Ame Ussi (12) wote ni wakaazi wa Mbuzi.
Kwa upande
wa wazazi wa Marehemu Akizungumza Malaki Mzee Salum mzazi wa marehemu
AbdullLatifu Ame Ussi (12) ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kuwafariji na kushiriki nao katika majonzi yao. Wamesema ujio wa viongozi hao
umewapa faraja na kuwatia moyo katika kipindi kigumu wanachokipitia, huku
wakieleza matumaini yao kuwa hatua za kuimarisha usalama katika maeneo
hatarishi zitachukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.
Katika
ziara hiyo, Waziri Anna aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Lela
Burhani Ngozi, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Bw. Makame Khatib
Makame. Viongozi hao kwa pamoja walitoa pole kwa familia zilizofiwa na
kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwa karibu nao katika kipindi chote
cha maombolezo.
Comments
Post a Comment