NA ZUHURA JABIR, ZANZIBAR@@@@
"Uongozi
hauanzi unapopewa cheo; huanza pale unapokuwa tayari kuwahudumia wengine,’’ kauli
hii inaelezea kwa ukamilifu safari ya Nadya Juma Idrissa, kijana ambaye
ameonyesha kuwa uongozi wa kweli hujengwa kwa kujituma, nidhamu na huduma kwa
jamii.
Katika kipindi ambacho vijana wengi bado
husita kushiriki katika masuala ya uongozi, Nadya, aliamua kuchukua hatua
mapema.
Alianza kama mwanachama wa kawaida wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), lakini leo ni Katibu wa Hamasa wa Tawi la ‘UVCCM’ katika
Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).
Safari yake ni ushahidi kwamba mafanikio
hayaji kwa bahati, bali hujengwa hatua kwa hatua.
MWANZO WA SAFARI YA UONGOZI
Nadya anasimulia kuwa, safari yake
ilianza akiwa bado mwanafunzi, alipokuwa akishiriki kwa hiari, katika shughuli
mbalimbali za CCM kwenye tawi la eneo analoishi.
Hakuwa na cheo wala mamlaka, lakini
alijitokeza kila mara, kushiriki shughuli za chama, mikutano na kazi za
kujitolea.
Kupitia uzoefu huo, alijifunza thamani
ya uwajibikaji, nidhamu, ushirikiano na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa
jamii.
Kwa mtazamo wake, kuwa mwanachama wa
kawaida kulimjengea msingi imara wa kuelewa kwamba uongozi ni huduma, si
mamlaka.
Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha
Zanzibar (ZU), hakubadili mwelekeo wake, kwani aliendelea kushiriki kikamilifu
katika shughuli za ‘UVCCM’, akihudhuria mikutano, semina, kampeni za
uhamasishaji.
ALIVYOPATA IMANI YA WANACHAMA
Bidii yake haikubaki bila kuonekana,
kwani wanachama wenzake walimuamini na kumchagua kuwa, Katibu wa Hamasa wa Tawi
la UVCCM katika Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Kwa hakika nafasi hiyo iliyompa jukumu
la kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuimarisha
mshikamano ndani ya chama.
"Sikuwahi kufikiria kwamba
ningepewa nafasi ya uongozi mapema kiasi hicho, nilichokifanya ni kujituma,
kuheshimu watu na kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu," anasema.
Kupitia nafasi hiyo, Nadya alipata
uzoefu wa kupanga shughuli za chama, kuzungumza mbele ya hadhara, kushirikiana
na viongozi wa ngazi mbalimbali na kujenga uwezo wa kuongoza makundi yenye
mitazamo tofauti.
UONGOZI ULIBADILI MAISHA YAKE
Kwa Nadya, uongozi haukumletea uzoefu wa
kisiasa pekee, bali ulimjengea kujiamini, kumpa uwezo wa kufanya maamuzi kwa
haraka na yenye busara.
Anasema nafasi
alizopata zimemfungulia milango ya fursa nyingi, zimemsaidia kujenga mtandao
mpana wa watu na kumwandaa kwa majukumu makubwa zaidi.
"Nimejifunza kuwa mafanikio hayaji
kwa bahati pekee, bali yanahitaji nidhamu, uvumilivu, kujifunza kila siku na
kuheshimu watu unaofanya nao kazi," anasimulia.
CHANGAMOTO HAZIKUKOSEKANA
Kama ilivyo kwa safari nyingi za
mafanikio, njia yake haikuwa rahisi.
Changamoto kubwa ilikuwa kusawazisha
masomo na majukumu ya uongozi, wakati mwingine alilazimika kusafiri kwa ajili
ya shughuli za chama, katika kipindi ambacho masomo yalikuwa yanaendelea.
Anasema kulikuwa na nyakati ambazo,
alikosa kuhudhuria vipindi kwa takribani wiki mbili kutokana na majukumu ya
kichama.
Hata hivyo, hakuruhusu changamoto hizo
zimrudishe nyuma, ikiwemo kukatisha masomo au kukubali kuwa pocho darasani.
"Niliona changamoto hizo kama
sehemu ya kujifunza, zilinifundisha kupanga muda, kuwajibika na kufanya maamuzi
kwa haraka,"anasema.
Kwa upande wake, Afisa Programu na
Mawasiliano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar
(TAMWA-Zanzibar) Khairat Ali, amesema lengo
la mafunzo wanayoyatoa ni kuwajengea uwezo waandishi kuhusu masuala ya
wanawake na uongozi.
Akiamini kuwa, hatua hiyo itasaidia
kuibua changamoto za wanawake na jamii kwa ujumla, ili zipatiwe ufumbuzi kutoka
kwa mamlaka husika.
MAMA YAKE ANASEMAJE ?
Mama yake mzazi, Fatma Haji Khatib, anasema
ameshuhudia mabadiliko makubwa tangu mtoto wake, aanze kushiriki katika
shughuli za uongozi.
Anaona sasa, uongozi umemjengea Nadya
kujiamini, uwezo wa kushirikiana na watu na kufungua milango ya fursa
mbalimbali za maendeleo.
"Nina imani naye sana, nitaendelea
kumuunga mkono katika kila hatua ya safari yake, kwa sababu naamini ana uwezo
wa kuitumikia jamii kwa uadilifu na kujituma,"anasimulia mama yake.
Hajra Ramadhan Juma, ninayo heshima
kubwa kutoa shuhuda yangu kuhusu kiongozi huyu ambaye nimepata fursa ya
kumfahamu katika safari yake ya uongozi ndani ya chama.
Katika kipindi chote nilichomfahamu,
ameonyesha uadilifu, uwazi na kujituma kwa hali ya juu, huku, akitanguliza
maslahi ya wanachama na maendeleo ya chama.
Aanasema amekuwa mstari wa mbele
kusikiliza maoni ya wanachama, kutatua changamoto na kuimarisha mshikamano.
Kama wahenga walivyosema, "Umoja ni
nguvu, utengano ni udhaifu," na hilo amelidhihirisha kupitia uongozi wake,
unaojenga ushirikiano na kuleta matokeo chanya.
Kwa kuzingatia uwezo wake wa kuongoza na
maono yake, ana imani ataendelea kukipeleka chama mbele, na wameahidi kuendelea
kumuunga mkono kwa dhati, ili afikie ndoto zao.
Nadya mwenyewe anaamini wanawake
wameendelea kuthibitisha uwezo wao katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa sasa wanashiriki kikamilifu katika
kuhamasisha wananchi, kupanga shughuli za maendeleo na kushiriki katika maamuzi
yanayoathiri maisha ya jamii.
Hata hivyo, anaona bado zipo changamoto
zinazowazuia wanawake wengi kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.
Anataja hofu ya unyanyasaji wa kisiasa,
ukosefu wa mafunzo ya uongozi na siasa, changamoto za kiuchumi pamoja na
mitazamo hasi ya kijamii kama baadhi ya vikwazo vinavyopunguza ushiriki wao.
SHERIA ZINASEMAJE?
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, zinatambua usawa wa wananchi
na kupinga ubaguzi.
Aidha, Tanzania imeridhia Mkataba wa
CEDAW pamoja na Itifaki ya Maputo ya Umoja wa Afrika, ambazo zinahimiza
wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi ya umma.
Aidha lengo la Tano la Malengo ya
Maendeleo Endelevu (SDG 5) linahimiza usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa
wanawake katika nafasi za maamuzi.
Hii inaonyesha kuwa, ushiriki wa
wanawake katika uongozi si suala la hiari pekee, bali ni sehemu muhimu ya
utekelezaji wa haki za msingi na maendeleo jumuishi.
WANAUME/SERUKALI INASEMAJE
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi,
akizungumza mjini Wete Pemba, kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi,
aliahidi kuongeza nafasi za uteuzi kwa wanawake.
‘’Wanawake wamekuwa wakichapakazi bila
ya kusita, hivyo kila ninapofanya teuzi, ntahakikisha nao wanakuwemo, maana ni
wachapakazi,’’alisisitiza.
Ali Khamis Makame wa Mikunguni, anasema
wanawake, wanayohaki sawa na wanaume katika kushika hatamu za nchi.
‘’Maana mikataba, sera, sheria, katiba
na miongozo mbalimbali ya kikanda, Afrika na ulimwenguni haijambagua
mwanamke,’’anaeleza.
Katibu mkuu wizara ya Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo Zanzibar Matar Zahor Massoud, aliwahi kusema kuwa,
wanawake hawajawahi kupewa nafasi wakaharibu za uongozi.
Omar Juma Hassan wa Tunguu, alisema
jamii isipowaamini wanawake kwenye uongozi, wasitarajie mabadiliko ya
kimaendeleo.
Ofisa Mdhamini wizara ya Elim una
Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salum, moja ya juhudi wanazozifanya ni
kuweka serikali za wanafunzi, ambapo wanafunzi wa kike wanapata kujifunza.
Akizungumza kwenye hafla ya kutoa zawadi
kwa waandishi wa habari za takwimu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar
Dk. Hamad Omar Bakar, alisema wanawake kupewa uongozi sio hidaya, bali ni
sheria na kanuni zinaagiza hivyo.
USHAURI WAKE KWA WANAWAKE VIJANA
Nadya anawahimiza wanawake vijana
kuamini uwezo wao na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto.
Anasema mwanamke anayetamani kuwa
kiongozi anapaswa kutafuta elimu, kujifunza mbinu za uongozi, kujenga mtandao
wa watu wanaomuunga mkono.
"Usisubiri kupewa nafasi;
jitengenezee mazingira yatakayokufanya uaminiwe. Uongozi hujengwa kwa tabia,
maadili na utendaji mzuri." anasema.
Safari ya Nadya Juma Idrissa ni zaidi ya
simulizi ya mafanikio binafsi; ni somo linaloonyesha kwamba uongozi hujengwa
kwa hatua ndogo ndogo, kwa kujituma, kujifunza na kuhudumia wengine.
Kutoka kuwa mwanachama wa kawaida hadi
kuwa kiongozi wa UVCCM, ameonyesha kuwa bidii, nidhamu na uadilifu vinaweza
kufungua milango ya mafanikio.
Kwa wanawake na vijana wanaoota kuingia
katika uongozi, simulizi yake ni ukumbusho kwamba changamoto ni sehemu ya
safari, si mwisho wa ndoto.
Kwa kutumia fursa zilizopo, kuendelea
kujifunza na kuzingatia maadili, kizazi cha leo kina nafasi ya kuwa nguvu kubwa
katika kujenga Tanzania yenye usawa, uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Mwisho

Comments
Post a Comment