NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa Halmashauri ya wilaya ya
Micheweni Pemba, wametakiwa kurejea utamaduni wao wa kuweka mazingira yao safi
na salama, ili kujikinga na magonjwa ya kuharisha, ambayo chanzo chake kikuu ni
uchafu.
Ushauri huo umetolewa jana na Mwanasheria wa Halmashauri
hiyo, Rukia Khamis Haji, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii,
kufuatia uwepo wa tishio la matumbo ya kuharisha, katika baadhi ya maeneo
kisiwani Pemba.
Alisema, suala la usafi haipendezi kuona wananchi wanalifanya
kwa shindikizo la Halmshauri, bali wenyewe waamue kujielekeza kwenye usafi, ili
kujihakikisha usalama wao.
Alieleza kuwa, utamaduni wa kuweka mazingira safi na
salama, ni vyema kwa wananchi wa Halmashauri hiyo, ikawa ndio utamaduni wao
endelevu, kwani kinyume chake ni kujiangamiza.
‘’Hichi ni kipindi cha mvua na kinakuwa na changamoto
zake, ikiwemo kusambaa kwa uchafu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hivyo
suala la usafi lazima liwe kipaumbele chetu,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mwanasheria huyo wa
Halmashauri ya wilaya ya Micheweni Rukia Khamis Haji, amewakumbusha
wafanyabiashara nao kuzihifadhi vyema biashara zao, ili zisishambuliwe na
wadudu.
‘’Tunajua kuwa, biashara kama mandazi, visheti,
mikate, samaki wa kukaanga na matunda, huwa ni rahisi kuingiliwa na nzi, ambao
kwa njia moja ama nyingine, hubeba vimelea vya magonjwa,’’alifafanua.
Hata hivyo, amewakumbusha wafanyabishara hao,
kuendelea kulipa kodi zao kwa wakati, ili kuiwezesha Halmashauri hiyo na
serikali kuu, kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Micheweni, akiwemo
Huda Hamad Simba, alisema bado wapo baadhi ya wananchi, ambao wamekuwa
wakitiririsha maji taka ovyo.
‘’Watu bado elimu haijawafikia na wingine ni wakaidi
wa kuchimba mashimo maalum ya kuhifadhia maji taka, kwani yakitiririka huwa
chanzo cha magonjwa kusambaa,’’alifafanua.
Aisha Omar Mjaka, alisema ni vyema kukaandaliwa
adhabu na faini nyingine, pindi akijitokeza wananchi wenzao, kukaidi amri ya kufanya
usafi.
Hidaya Haji Khamis na mwenzake Mwamize Kombo Juma,
walisema usafi katika baadhi ya shehia zao, umekuwa ukisua sua, kwakule wananchi
kukosa usimamizi.
Juzi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Chake chake Shida Kombo
Mohamed, alifanya ziara ya kushtukia katika viwanjwa vya sikukuu na kupiga
marufuku uuzaji wa juisi.
Hata hivyo, aliwahimiza wafanyabiashara hao, kuzihifadhi
vyema biashara zao, kwa kuzitia kwenye masunduku ya vioo, ili kuwakinga wateja
wao na uwezekano wa kupata magonjwa.
Afisa Mdhamini wziara ya Afya Khamis Bilali Ali,
aliwakumbusha wananchi, kuyasafisha mazingira waliyoyazunguruka, sambamba na
kuchemsha maji ya kunywa.
Mwisho
Comments
Post a Comment