NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
WANANCHI shehia ya Mjimbini wilaya ya Mkoani
Pemba, wameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kwa
upatikanaji wa maji safi na salama shehiani mwao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Juni 20, 2025 mwananchi Saumu Issa Mohamed alisema, huduma ya
upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapo, kwa sasa ni yauhakika jambo
linalotoa faraja kwao.
Alisema mafanikio hayo ni muhimu kwao, kutokana na
umuhimu wa huduma hiyo katika maisha yao ya kila siku, hivyo wameipongeza
serikali kwa kuwahakikishia upatikanaji
wa huduma hio saa ishirini na nne.
Mwananchi Suleiman Muhammed Makame kutoka shehiani hapo
alisema, kwa miaka zaidi ya saba iliopita,
iliwalazimu kutumia maji ya mito na visima ambayo hayakua safi na salama,
kwa matumizi ya binaadamu, hivyo upatikanaji wa huduma hiyo imekua suluhu ya
tatizo hilo.
Nao Zahra Hafidh Juma na Hafidh Khatib Faki, walisema,
upatikanaji wa huduma hio ni utekelezaji wa ahadi ya serikali ya awamu ya nane,
ya kuwasogezea karibu wananchi wake huduma zote muhimu za kijamii, ikiwemo ya
maji safi na salama.
Hivyo waliongeza kwamba ili kuungamkono jitihada hizo
watahakikisha wanatunza miundombinu hio kwa maslahi ya sasa na baadae.
"Serikali imefanya jitihada ya kutatua changamoto ya
ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, iliokua ikitukabili, na kwa sasa tunapata ipasavyo, hivyo tutahakikisha tunatunza miundo mbinu hii kwa
matumizi ya sasa na baadae," walisema.
Kwa upande wake sheha wa Mjimbini wilayani humo, Faida
Haji Khatib, alisema serkali imekua ikichukua jitihada mbalimbali, ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za kijamii.
Alieleza kuwa, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuungamkono
jitihada hizo, ili kufikia lengo la serikali na wananchi kupata huduma za
kuendesha maisha yao.
Alisema kua, niwajibu wa wananchi wa kijiji hicho kutumia
maji kwa uangalifu, kwa kuepuka kuyamwaga ovyo, pamoja na kuchangia kwa wakati,
ili kuiwezesha huduma hio kudumu kwa mda mrefu.
Hata hivyo aliwaomba viongozi wa jimbo hilo, pamoja na wadau wingine wa maendeleo, kuwapatia tanki
lenye uwezo wa kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji, ili kujihakikishia zaidi
huduma hiyo hata kipindi ya umeme unapokazimika.
" Kwasasa tunakisima chenye maji mengi, ambayo ni
toshelevu kwa shehia yetu, ingawa bado
kuna hofu kwa wananchi,
kutokana na kutokua na tenki la kuhifadhia maji,’’alifafanua.
Nae Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji ZAWA Pemba Suleiman
Anas Massoud alisema, hatua hiyo ni
miongoni mwa mikakati ya serikali, ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na
salama kwa wananchi wote.
Shehia ya Mjimbini inawakaazi 3,210 wanaume wakiwa na 1,558
na wanawake 1,652 ikiwa na zaidi ya vitongoji vinne, na ni miongoni mwa shehia
zilizonufaika na mradi mkubwa wa uchimbaji wa visima, kupitia mradi wa COVID 19.
MWISHO
Comments
Post a Comment