Akizungumza na blog ya pemba today juzi, Afisa Miradi wa ‘ZLSC’ Beny Louis Mlingi, alisema wengi wao ni wale waliolalamikia ukosefu wa vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa, vitambulisho vya ukaazi pamoja na migogoro ya ardhi.
Alieleza kuwa, kwa sasa wamepanga kulifuatilia hilo, ili kuona wanawasaidia wananchi hao, ili kupata nyaraka hizo muhimu kwa ajili ya shughuli nyingine.
‘’Ni kweli hapa Uwandani wananchi wameitikia wito wa kufika kwenye kambi yetu ya siku tatu, na tumegundua shida zipo za wananchi kulalamikia ukosefu wa nyaraka muhimu,’’alifafanua.
Mapema Mwenyekiti wa Kituo hicho Pfrofesa: Chriss Maina Peter, alisema wanakusudia kukutana na watendaji wakuu wa serikali, ili kuona wananchi hoa wasiokuwa na uwezo wanaondoshewa ada ya vyeti vya kuzaliwa.
Alisema, wapo wananchi hadi wenye miaka 50 na 70 wakilalamikia ada kubwa ya malipo ya upatikanaji wa vyeti, jambo ambalo, kwa hali zao linaingia akili.
‘’Baada ya kuona hali hii, sasa sisi ‘ZLSC’ ni kuangalia uwezekanao wa kuzungumza na serikali kuu, kwamba wale wasiokuwa na uwezo, sasa wanapewa nyaraka za vyeti bila ya malipo,’’alifafanua.
Kwa upande wake Afisa Sheria wa ‘ZLSC’ Asha Maulid Khamis, aliwataka wananchi, ambao wanachangamoto nyingine za kisheria, wasisite kuwatumia wasaidizi wa sheria waliomo katika maeneo yao.
Sheha wa Uwandani Ali Hamad Mussa, alisema ujio wa watendaji hao wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, imesaidia kwa wananchi wake, kupata uwelewa wa masuala ya kisheria.
Hata hivyo, alisema katika shehia yake, hakuna mwananchi anayemkosesha nyaraka kama za cheti cha kuzaliwa, vitambulisho, ingawa wapo wanaoshindwa kulipa ada.
‘’Wapo wananchi hali zao ni za kimaskini, na ndio maana hufuatilia hadi mwisho, lakini hushindwa ada kwa hali zao zilivyo,’’alifafanua.
Mwananchi Mohamed Issa Ali, alisema ujio wa watendnaji hao, kumesaidia kupatikana kwa njia rahisi ya kudai nyaraka hizo muhimu.
Nae Asha Haji Mohamed, alisema amepewa njia ya kufuatilia kesi ya mtoto wake, iliyokwama kituo cha Polisi Chake chake kwa muda wa mwaka mmoja sasa.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, kimeasisiwa mwaka 1992, kwa kutoa huduma za maktaba, kuwasomesha wasaidizi wa sheria na kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria kwa wananchi bila ya malipo, ambapo kama hiyo inaendelea wilaya ya Wete.
Mwisho
Comments
Post a Comment