HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
NI majira ya saa 4:00 asubuhi, nilipofika katika bonde la Kigawani kijiji cha Chwale Wilaya ya Wete Pemba, nikitokea Mkoani.
Katika safari hiyo niliyochukuwa muda usiopunguwa saa 1:30 kwa usafiri wa umma, nikiwa na lengo la kutaka kujuwa changamoto na maendeleo ya kilimo msitu ambacho kinalimwa shehiani humo.
Ilikuwa ni safari yenye kheri kubwa, kwani kukutana na wakulima wa kilimo msitu, ambao wameamuwa kujikita na kilimo hicho wakiwa na malengo ya kujikwamua kimaisha.
Pamoja na wakulima wengine kuzungumza nao nilipata hamu na shauku kubwa ya kuzungumza na mkulima Naomba Shaaban Mbarouk, baada ya kumsikia kuwa alikotokea hakuwa na hamu ya kujiingiza katika kilimo hicho.
Wala sikufanya ajizi nilimvuta pembeni, chini ya muembe huku upepo ukitupepea taratibu akiielezea makala haya, kinaga ubaga kuhusu kilimo hicho kilichomvutia hadi kujiingiza.
Alijiingiza katika kilimo hicho, baada ya kupata mafunzo kutoka jumuiya ya uhifadhi wa misitu, yaliyomuonesha njia na kumpa uhakika wa kuendesha maisha.
Anasema ni faraja kubwa aliyonayo kwa kuweza kuingia katika kilimo msitu, kwani ana uhakika wa kuendesha maisha yake, na kuacha utegemezi.
"Huko nilikotokea sikuwa nikilima na hata lengo la kuanza kulima sikuwa nalo, ila sasa siwezi kukiacha.
Anasema na TAMWA – Zanzibar nao walimzidisha hamasa ya kujikita na kilimo hicho, baada ya kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Anasema TAMWA imefanya jambo moja zuri, kuwapa wakulima elimu na kuwawezesha kuzungumza na vyombo vya habari, kwani sasa wataweza kutowa changamoto na mategemeo yao.
Kumbe Naomna kabla ya kuingia katika kilimo hicho, maisha yake yalikuwa magumu, ila baada ya kuanza kilimo na kujivunia matunda mengine kula na mengine kuuza kupata pesa za kujikimu anafurahia maisha.
"Nilipojuwa umuhimu wa kilimo msitu, kinavoweza kuniinuwa kimaisha sikujibweteka niliingia shambani na kuanza kufanya kazi za kilimo hichi,"anasimulia.
HATUA ALIZOCHUKUWA KUIMRISHA KILIMO HICHO
Baada baada ya kuingia kwenye kilimo hicho, alishirikiana na wenzake wakachimba mashimo, kwa ajili ya kupata maji na wakafanikiwa na wakawa wanamwagilia vizuri na kilimo chao kilinawiri.
Hali hiyo iliendelea akaendeleza kilimo hicho ingawa kila siku zinapoendelea hali ya juwa kali inaendelea na kukiifanya kilimo hicho kudhoofika na kisha kufa.
"Pamoja na faida zinazopatikana kupitia kilimo msitu, lakini, kuna changamoto zinazokikabili kilimo hicho,,"anasema.
Anasimulia moja ya changamoto ni ukosefu wa maji kwa kuwepo kwa jua kali linalosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Hali hiyo, imeathiri kilimo hicho na kufanya baadhi ya miche kukosa afya na mingine kufa kabisa, kilichosababisha kufa kwa baadhi ya miche.
Kilimo msitu ni chenye kukomboa maisha ya waliowengi kwani ni mchanganyiko wa miti na matunda hivyo ndani ya miezi mitatu unavuna na kula ama kuuza.
Mimi nimepanda migomba, minanasi, miparachichi miembe, midimu, mikungu India, kunde, njugu na mchicha.
KITAMSAIDIAJE
Naomba anasema kwa vile kilimo hicho ni cha mchanaganyiko kati ya miti na matunda na hakichukuwi muda mkubwa, kati ya kupanda na kuvuna kitawasaidia kuondokana na njaa na kukuza uchumi.
Akizungumza kwa furaha anasema kilimo msitu kinampa uhakika wa kuyamudu maisha yake na kujisikia furaha kila siku ziendapo.
Kumbe hapo awali, hakuwa na uhakika hata wa shilingi 5000 kwa mwezi, maana hakuwa mwenye kujishughulisha na kazi yoyote, alikuwa ni wa kukaa ndani na kusubiria kuletewa tu.
Shughuli za kilimo cha mihogo na mpunga ambacho alikuwa analima mwenza wake hakikumtosheleza hata kidogo yeye na familia yake.
Ndani ya shamba lake la kilimo msitu, Naomba sasa atakuwa na uhakika wa chakula kwa muda wakati, kwa kuvuna minanasi miezi sita ijayo.
Wakati anavuna manasi kwa ajili ya chakukala na biashara fedha, zitamuwezesha kuanzisha miradi mingine aliyokwishaibuni ikiwemo wa kuuza sabuni.
‘’Hivi sasa nimeanza kuona mwanga, maana nna uhakika wa kuingiza lakini 300,000 hadi shilingi 500,000 kwa mwezi, ntakapovuna mananasi ndani ya miezi sita ingawa nimo mbioni kupanda mabamia na matango,’’anasema.
MATARAJIO YAKE
Ni kuwa mkulima mkubwam kujiendeleza kimaisha na kufikia kwenye uchumi mkubwa wenye manufaa na kuongeza pato lake.
Ingawa matarajio mengine ni kuwapa wenzake elimu upandaji, kama alivyoipata yeye pamoja na kutowa elimu kwa jamii iliyomzunguka.
“Nataka niwe mkulima mkubwa katika kilimo hichi na niwafikie wengine wote wenye hamu ya kulima kilimo hichi,”anafafanua.
WATU WA KARIBU WA NAOMBA
Bikombo Khamis Hamad ni mmoja wa wakulima wenzake amabao wanalima kilimo msitu katika bonde la Chwale, anasema wamefurahia baada ya kumuona Naomba, amejiongeza na amejikita na kilimo hicho.
Anasema alikuwa ni mmoja amabae hataki kujishirikisha na kilimo hicho, lakini kwa sasa amekuwa wa kwanza kushajihisha wenzake.
“Ama kweli mafunzo yanamtowa mtu sehemu moja kumpeleka kwengine, kwani mwenzetu huyu baada ya kupata mafunzo ameshajihika kweli na kilimo hichi”,alisema.
Khatib Juma Mbarouk ni mume wa Naomba, anasema hapo awali, hakuwa tayari mkewake kutoka toka na kujishirikisha na kilimo, ingawa kwa sasa amebadilika.
Anasema hali ya maisha kuwa ngumu na kuona faida wanayoipata wanawake wengine ikiwemo kujihudumia angalau kwa baadhi ya mahitaji na watoto ndio akaona, amruhusu.
“Faida ya kilimo msitu ipo kwa sababu tumekuwa tofauti baada ya kujiingiza na kilimo hichi tunapata mazao ya kula na kuuza pia”,anasema.
Saada Hamad Alawi ni mama wa Naomba anasema alichukuwa jitihada kubwa ya kumshajihisha mwanawe kuhusu kujiingiza na kilimo mtoto wake, ingawa hakuwa tayari.
“Baada ya kupata mafunzo ya umuhimu wa kilimo sasa ameridhia na anaiona faida, kwani hataki tena kukiacha kilimo hichi,”anaeleza.
Mkuu wa Mawasiliano na Habari chama cha waandishi wa Habari Tanzania TAMWA Zanzibar Safia Ngalapi akawataka wakulima hao akiwemo Naomba, wasikate tamaa na wasikae kimya badala yake wazisemee chanagamoto zinazowakwaza.
Akawanasihi kuwa pamoja na misaada kuelekezwa katika mambo mengine ikiwemo mipira, badala yake itazamwe na kwa wakulima ili nao waweze kujikomboa katika kilimo chao.
Ili wakulima waweze kuendeleza kilimo chao na kuondokana na changamoto zinzowakumba, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anatupia nguvu zake, katika kutowa msaada wa hali na mali.
Mwisho
Comments
Post a Comment