HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
‘UKIMUELIMISHA mwanamke umeielimisha jamii nzima'
Kutokana na msemo huo, inadhihirika kuwa mwanamke ni muhimili mkubwa, katika dunia hasa pale anapoonekana kuwa na nafasi kubwa ya ulezi ndani ya familia.
Ingawa haimaanishi kwamba, baba si muhimu hapana nae ana umuhimu wake mkubwa tu, lakini kwa upande wa mama anaechukuwa nafasi ya ulezi wa familia ni jambo kubwa.
Na ndio maana, inafahamika kuwa dunia isingeweza kuendelea mbele bila ya uwepo wa wanawake, kwani kuwekeza kwa wanawake na wasichana kunaleta matokeo makubwa.
Wanawake wanahitaji kuwa na nyenzo madhubuti zitakazowawezesha kuyamudu maisha yao na kuondokana na utegemezi, ambao unaweza kuwa kikwazo katika kuendeleza mbele maisha yao.
Pamoja na kuwepo mafanikio na juhudi za wanawake katika sehemu mbalimbali ikiwemo za kiuchumi, na kijamii bado inaonekana suala la mabadiliko ya tabianchi, linaendelea kuwa na madhara makubwa kwa wanawake.
Wanawake wanazidi kuonekana kama watu walio katika hatari zaidi ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi, kuliko wanaume, kwani wengi wao ndio wategemezi.
Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), wanawake pia ni watu wa kwanza kuhisi madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mathalan nchini Kenya, baadhi ya wanawakewanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 10, kutafuta kile wanachohitaji, ili kulisha familia zao pamoja na kutafuta maji.
Matumaini ya wanawake wa kisiwa cha Pemba shehia ya Chwale Wilaya ya Wete ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, kwa kujikita katika kilimo msitu.
Wanawake hawa, wameweka matumaini makubwa juu ya umuhimu wa kilimo msitu huku wakiamini ndio mkombozi mkubwa wa maisha yao.
Ingawa wanawake hao ni wale waliomo kwenye mradi unaoendeshwa na Jumuiya ya Uhifadhi wa misitu Pemba ‘CFI’ na ‘CFP’ wanaofanyakazi kwa karibu na TAMWA Zanzibar, na hasa baada ya serikali ya Canada kutoa fedha na Serikali ya Zanzibar kuridhia.
Pamoja na kwamba mradi huo imeanza kwa shehia nane kwa Unguja na Pemba, ikiwemo wanawake wa shehia za Mchanga mdogo, Kambini, Kiuyu minungwini na Chwale kwa Pemba.
Sasa wanawake wa maeneo hayo wameshaamka na kujikita katika harakati za kilimo hicho, ambacho wanasema iwapo watakiendeleza watakuwa na uhakika wa kuyamudu maisha yao.
Kilimo msitu amabacho ni mchanaganyiko wa mazao mbalimbali kama migomba, minanasi, mbazi, michikichi, njugu, mahindi na miembe.
WANAWAKE WANUFAIKA
Rehema Salim Issa wa Chwale Weete anasema, kilimo msitu kinawapa uhakika wa chakula katika maisha yake.
Ingawa kilimo hicho kimekabiliwa na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi bado wanaendelea nacho.
Anaona pamoja na kuonesha juhudi, kubwa katika kilimo hicho bado mabadiliko ya tabianchi yanawaathiri, ikiwemo jua kali na kupelekea kilimo chao kuharibika.
Anasema suala la jua kali limechangia kutokuwa na maji na vipando kupotea kwa haraka, jambo ambalo hukabiliwa na ongezeko la umaskini.
"Kilimo hichi tunakitegemea kujikwamua na umaskini kwani tunapata chakula, ila jua kali limetukosesha kupata maji na imechangiwa miti kufa,’’anasema.
Mkulima kiongozi Hadia Omar Haji wa kijijini hapo, anasema kilimo hicho kinawanufaisha kwa muda tofauti ikiwemo muda mfupi, kati na mrefu.
Kumbe, ili waweze kunufaika kama ilivyo maumbile ya kilimo hicho, huduma ya maji ya kumwagilia ni muhimu.
“Kusema kweli tatizo la mabadiliko ya tabianchi yanatuweka katika hali ngumu, kwani sasa ni jua hatujui ikija mvua itakuwaje,’’anaeleza.
Kwa vile wanawake ndio wakaaji wa nyumbani kuliko wanaume, hutumia muda mkubwa kuwashughulikia watoto kwenye mambo mengi, ikiwemo kula.
"Wenzetu wanaume si sana kuteswa na njaa kwani wao si wakaaji wa nyumbani, kama tulivyo wanawake na watoto wetu yeye akitoka hupata cha kujitafunia,"anasema.
Bikombo Khamis Hamad anasema kuwekeza kwa wanawake na wasichana, kunaleta matokeo makubwa ambayo yanaigusa jamii, na maarifa waliyonayo wanawake yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine.
FAIDA YA KILIMO MSITU
Kilimo msitu ni mfumo wa kilimo unaohusisha upandaji wa miti , mazao na wanyama, kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo.
Pamoja na kuwa rafiki kwa kupata chakula, kuzuwia ukame kilimo hichi pia kinaleta kivuli na kuzuwia upepo makali.
Mkulima anaweza kunufaika na kilimo msitu kwa kumpatia mahitaji yake ya msingi kama vile kuni, matunda, kurutubisha udongo malisho ya mifugo, dawa za asili.
Nyingine ni usindikaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu kama vile juisi, jamu na asali.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya uhifadhi wa misitu Pemba Mbarouk Mussa, anasema kutopatikana kwa mvua, kukata miti ni jambo jingine linaloendelea kuathiri.
Anasema athari mbalimbali za ukataji wa miti kwa shughuli za kijamii, zimekuwa zikijitokeza katika maeneo tofauti, huku jumuiya hiyo ikiendelea kutoa elimu.
Afisa kilimo kutoka CFP Saada Juma, anasema kupitia mradi huo haujabaguwa, ingawa lengo ni kuwainuwa wanawake katika shughuli za kujitafutia kipato.
Afisa mdhamini Wizara ya kilimo, umwagiliaji Maliasili na Mifugo Muhandisi Idriss Hassan Abdulla, anafafanuwa kuwa, wameandaa mpango maalum wa kuhakikisha wanazalisha kupitia kilimo msitu.
WANAUME WANASEMAJE
Hamad Ali Suleiman, anasema wanatambua mchango mkubwa wa wanawake, katika kukiendesha kilimo msitu kwani hawako nyuma katika kuhakikisha kinaendelea.
Rubea Mwadin, anawashauri wanaume kuwaruhusu wanawake, kujiingiza katika kilimo hicho na ili waweze kujikwamua na maisha.
TAMWA ZANZIBAR
Chama cha waandishi wa Habari wanawake TAMWA Zanzibar, nao husimamia kidete haki za upatikanaji wa usawa wa kijinsia na kuwashirikisha wanawake.
Mkuu wa mawasiliano na Habari TAMWA Sofia Ngalapi anawataka wakulima hao, wasikae kimya, katika kueleza changamoto zinazowakwaza katika kilimo chao.
KumbeTAMWA imewapa elimu ya kuzungumza na waandishi wa habari, sasa wawatumie hapo ndio yatakaposikika .
“Tunapaswa kufahamu kwamba kuwekeza kwa wanawake na wasichana kunaleta matokeo makubwa ambayo yanaigusa jamii, na maarifa waliyonayo wanawake yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine,”anasema.
Katika mwaka wa 2013 Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ilifanya marekebisho ya sera ya mazingira ya mwaka 1992 na kuingiza katika sera hiyo mpya, masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Sera hiyo ya mwaka 2013, imetoa muongozo juu ya usimamizi wa masuala ya kimazingira, lengo ikiwa ni kuweka rasilimali za mazingira za Zanzibar, kwa maendeleo endelevu na usimamizi bora wa mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa mujibu wa utafiti mdogo uliofaywa mwaka 2013/2014, mkuu wa Kitengo cha Tabianchi katika Idara ya Mazingira Pemba, Ali Abdi Mohamed anasema kuna maeneo 123 ya mashamba yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi wa kupambana na mabadiliko tabia nchi umetowa miche 178,268 ya aina mbalimbali ikiwemo migomba 7,000, minanasi 117,054.
Miti ingine ambayo imetolewa kwa mfumo wa miche kwa walengwa hao wa mradi ni midalasini 39,968, miparachichi 5,950, miembe 3,682, midimu 523, michungwa 534.
Mradi wa ZANADAPT unaoendeshwa na jumuiya ya uhifadhi wa misitu wenye lengo la kuwafikia wajasiriamali 4,000 amabao asilimia 80 wakiwa ni wanawake amabao utasaidia uzalisahi wa chakula na mazao pamoja na kupunguza umasikini wa kipato.
Mwisho
Comments
Post a Comment