NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Uwandani wilaya ya Chake chake, wamesema kambi ya siku tatu ya kutoa ushauri na msaada wa kisheria, inayoendeshwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, imezaa matunda kwao, kwa kupata ufumbuzi baadhi ya changamoto za kisheria, ikiwemo mirathi.
Wakizungumza na blog ya Pemba today, leo April 14, 2025 kwenye kambi hiyo skuli ya Uwandani, walisema wamepata ufumbuzi mkubwa, ambao baadhi yao walishakata tamaa.
Mmoja wa wananchi hao, aliyekataa kutaja jina lake, alisema tatizo lake la mirathi wa mali kadhaa, umepatiwa ufumbuzi wa haraka, baada ya kuitwa upande anaoulalamikia.
Nae Riziki Abdalla Suleiman (29), ambae alilalamikia kukosa vitambulisho vya mkaazi, cha taifa na cheti cha kuzaliwa, sasa amepata muelekeo.
‘’Nilishahangaika kwa zaidia ya miaka 19, lakini sijafanikiwa, ingawa kupitia ushauri wa kisheria uliotolewa na ZLSC, sasa nimeondoka na furaha,’’alieleza.
Kwa upande wake Mwana Said Khamis (30), alieleza kuwa, kilichomfikisha mbele ya wanasheria hao kutoka ‘ZLSC’, ni kulalamikia matunzo ya watoto.
Nae mwananchi Halima Yussuf Khamis (70), alisema anafuatilia cheti chake cha kuzaliwa, ingwa changamoto ni malipo ya fedha kwa taasisi husika.
‘’Mimi ujio wangu hapa, nikupata ufumbuzi wa kisheria namna ya kupata msamaha wa ada, kwa aina ya umri wangu, na cheti cha kuzaliwa ninachokihitaji, gharama sizimudu,’’alieleza.
Mapema Vakili kutoka ‘ZLSC’ Saleh Daud Othman, alisema zoezi hilo linakwenda vizuri, na wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi, kufikisha changamoto zao kisheria.
Nae Mwenyekiti wa bodi ya ZLSC Professa: Chriss Maina Peter, alisema elimu zaidi inahitajika kwa jamii ya Uwandani, ili wananchi kujua haki zao.
Kambi hiyo ya siku tatu, iliyoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ ilianza jana, April 13 na inatarajiwa kumalizika kesho April 15, ambapo wanatoa msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, kimeasisiwa mwaka 1992, kwa kutoa huduma za maktaba za kisheria, kuwasomesha wasaidizi wa sheria na kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria, kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Mwisho
Comments
Post a Comment