NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Wingwi Mjananza wilaya ya Wete Pemba, wamekishauri Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kuhamishia ofisi kwenye shehia yao, ili kila wanapokuwa na changamoto zao za kisheria wawe karibu nao.
Walisema, huduma walizopewa za ushauri wa kisheria bila ya malipo, zimewavutia na kuona ipo haja kwa sasa, kwa kituo hicho kujenga ofisi shehiani mwao.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi leo April 18, 2025 mara baada ya kufungwa kwa kambi ya siku tatu ya utoaji elimu, ushauri na msaada wa kisheria, walisema wanatamani ZLSC ijenga ofisini eneo la Mjananza.
Walisema kuwa, wengi wao walikuwa hawana uwelewa wa utaratibu wa kufuatilia nyaraka kama za vyeti vya ndoa, talaka, vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho jambao ambalo wamelipata ndani ya kambi hiyo.
Mwananchi Salim Hamad Faki, alishauri kuwa, ni vyema kwa ZLSC ikawa na ofisini ngazi ya shehia, ili kupunguzia dhiki za wananchi kuwafuata mjini wanasheria, wanapokuwa na changamoto za kisheria.
Nae Fatma Mussa Iddi, alisema kama ikiwezekana ni vyema kituo cha Huduma za sheria, kikajenga ofisi shehia ya Mjananza, hasa kutokana na aina yake ya huduma inayotoa.
‘’Kwa mfano mimi nilifuata kupata utaratibu wa kupata chti cha ndoa, maana nimeolewa huu sasa ni mwaka wa nane, lakini sijapata cheti,’’alifafanua.
Nae Mwajuma Himid Mjaka, alisema kupitia kambi hiyo ya siku tatu, amepata mwelekeo wa kwenda kuwashawishi kaka zake, kuharakisha mirathi.
Akizungumza katika ufungaji wa kambi hiyo, skuli ya Msingi Mjananza, Afisa Miradi wa ‘ZLSC’ Beny Louis Mlingi, alisema walifanikiwa kuwapata wananchi 304, wakiwemo wanawake 295 na wanaume tisa (9).
Alisema wingi wa wananchi waliowapokea walikuwa wakilalamikia ukosefu wa gharama za vyeti vya kuzaliwa, na baadhi yao wakikosa vyeti vya ndoa kwa zaidi ya miaka 25 sasa.
‘’Kwanza niwashukuru wananchi wa shehi ya Mjananza kwa kufuata wito wetu, na tumeona ipo shida kwa wananchi, ingawa wengi wao wanaliwa na umaskini wa kipato,’’alifafanua..
Nae Afisa Sheria wa ‘ZLSC’ Asha Maulid Khamis, alisema muitikio mkubwa wa wananchi, ni ishara kuwa msaada wa kisheria unahitajika kwa jamii.
‘’Kwa vile kila jimbo na baadhi ya shehia wapo wasaidizi wa sheria, ni dalilili kuwa waongeze kasi ya kuwafikia wananchi, maana bado wanakabiliwa na changamaoto za elimu, ushauri na msaada wa kisheria,’’alifafanua.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, kimeasisiwa mwaka 1992, kwa kutoa huduma za maktaba, kuwasomesha wasaidizi wa sheria na kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria kwa wananchi bila ya malipo.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, kimemaliza kambi ya siku sita kwa shehia za Uwandani wilaya ya Chake chake na Mjananza wilaya ya Wete, na kuwafikia wananchi 416.
Mwisho
Comments
Post a Comment