NA HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
‘TULIANZISHA mchezo huu tukiwa tunajiamini huku tukijuwa kuwa na sisi wanawake tuna haki ya kujishirikisha katika michezo ya aina mbali mbali’.
Hayo ni maneno ya kocha wa mpira wa pete timu ya Mchanaga mdogo Center Bimkubwa Maulid Othman, aliyezungumza na makala haya.
Kocha Bimkubwa aliyasema maneno hayo huko katika maeneo ya skuli ya Mchangamdogo Wilaya ya Wete Kisiwani Pemba, ambapo ndipo wanapofanyia mazoezi.
Akinisimulia miongoni mwa sababu ya kuanzisha mchezo huo, ni pamoja na kuwa michezo ni ajira, afya na kupata kujuwana na watu.
Ingawa anasema alianza kuupenda mchezo huo tokea akiwa mwanafunzi na alikushaanza kuucheza ila kuna kipindi, alisita japo kama ndoto yake ni kuwa mwanamichezo.
Anasema kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo jamii kuwadharau na kuwaona hawafanyi kitu cha maana, na kudai michezo si kwa wananwake, ilibidi avunjike moyo na kukaa tu.
“Tokea tuanzishe mchezo huu hali zetu kiafya zimeimarika kwani tunafanya mazoezi kila siku jambo ambalo kwetu ni faraja”, anasema.
Akitaja muonekano kwa jamii baada ya kuanzisha mchezo huo, anasema jamii iliwachukulia kuwa ni wahuni, lakini bado wanaendelea na hawajavunjika moyo.
Anasema vikwazo vingi ambavyo wanavipata katika jamii ikiwemo kupewa majina tofauti kama vile ‘madume dume’ ila bado wanasonga mbele.
Akiendelea kusimulia kocha Bimkubwa anasema alianza kufundisha vijana mchezo huo wakiwa katika mazingira magumu, huku jamii ikiwapa maneno ya kejeli ingawa hawakurudi nyuma.
“Lakini hatuwa ya mwanzo nilifundisha tukiwa hatuna vifaa vyovyote , hatuna uwanja ni wa kutengeneza wenyewe, mipira hatuna ni ya kubaka baka tu ,hakuna hata wadhamini,”anasema.
Pamoja na mazingira magumu ya mchezo huo, lakini waliendelea na kufundisha vijana kucheza akiwa na kocha mwalimu Mohamed, ambae kwa sasa ni mwenyekiti wa chaneza Pemba.
Anazidi kusimulia wakati wakiendelea na mchezo huo , vikwazo kwenye familia na kwenye ndoa pia, huku jamii iliyowazunguka, ikitowa maneno kadhaa kuwa mpira huo kwa wanawake ni haramu.
“Ingawa nilipambana nayo na sikukatisha njiani kwani, nilikuwa nashajiihisha vijana na mimi sikuvunjika moyo niliendelea nao taratibu hadi sasa wanaweza kucheza.
Akitaja faraja yake kubwa ni baada ya kupata mafunzo ya michezo kwa maendeleo kutoka TAMWA -Zanzibar, kwani nae aliweza kumuelimisha mwenza wake na akakubali.
Anasema ni jambo la faraja, kuona mwenza wake nae anaelimisha familia na hata jamii kuhusiana na umuhimu wa michezo kwa wanawake.
Anasema suala la mavazi, kuchanganyika kwa wanawake na wanaume, ndilo kubwa linalosemewa na jamii.
Anasema ni jambo linalohuzunisha kwa sasa, kuona timu hiyo inasuasua kwa namna moja ama nyingine na ndio maana hutowa fedha zake na wachezaji kuhakikisha timu inasonga mbele.
“Tatizo hatuna ligi hapa mpaka tuanzishe wenyewe katika shehia, lakini shida hatuna hata mdhamini huyo Mwakilishi na Mbunge hawatuanagalii haswa,”anasema.
Akitaja mafanikio anasema ni pamoja na kutambua kwa jamii ya Mchangamdogo, kuwa timu ya mpira wa pete ipo na kuwa na uelewa japo si kwa kiasi kikubwa.
Anasema jingine ni kutowa vijana nje ya Pemba hadi kisiwa cha Unguja, kwa ajili ya kushiriki na kucheza.
Mafanikio mingine ni vijana kupata umaarufu wa kujuwana na vijana wenzao kutoka maeneo tofauti Unguja na Pemba.
Kocha Bimkubwa aliwahi kupata mafunzo mbali mbali ya ukocha, kupitia mwalimu wake Ali Khamis wa Mchangamdogo na kupitia chama cha mpira wa pete CHANEZA.
“Nilitamani niwe kama kocha mwalimu Mohamed Mwenyekiti wa Chaneza Pemba, kutokana na utendaji wake mzuri na ufuatiliaji wa mchezo huu,”anasema.
Anataja changamoto na kusema kwenye mchezo huo hakuna wafadhili , ukosefu wa ligi, ukosefu wa kiwanja, ukosefu wa vifaa na uhaba wa timu za mpira wa pete za wanawake hasa kisiwani Pemba.
Uhaba wa mashindano ya mara kwa mara na mabonanza , umasikini wa familia ambapo hushindwa kupata fedha za kushiriki mechi japo za shehia kwa kuwa hulazimika kujichangachanga wenyewe kifedha.
“Nafasi alizonazo kwa sasa ni ukocha wa timu , katibu na keptain wa timu amabapo bado anaendelea na vijana katika kuhakikisha timu hiyo inaendelea mbele,’’anaeleza.
Jambo ambalo hatolisahau ni kule kuanzisha mpira huo Mchangamdogo na ukaweza kujulikana na kukubalika japo kwa asilimia ndogo.
Endapo atapata ufadhili ni kuuimarisha timu hiyo kwa kucheza ligi na timu tofauti kisiwani Pemba sambamba na kuanzisha timu nyengine ya watoto wadogo ili kuwekeza.
Akitowa ushauri wake anaiomba serikali kuongeza mkazo zaidi kuwaendeleza vijana wa kike hasa Pemba, katika mchezo wa pete kwani vipo vipaji vingi.
Kocha Bimkubwa alizaliwa mwaka 1995 ni mtoto wa tatu kwa mama Fatma Ali Hassan na kwa baba Maulid Othman Hamad.
Akimzungumzia Kocha Bimkubwa ,mmoja wa wachezaji wa timu hiyo Amina Kudra Ali anasema ni mwanamke anaejitolea kwa hali na mali kuhakikisha mpira wa pete unasonga mbele.
Anasema anashajihisha wachezaji kuhakikisha wanaendelea kuwa na hamu ya kuupenda mchezo huo.
Kocha Bimkubwa anaonesha kuukubali mchezo huo kwani hutowa cha kwake mfukoni , alimradi mchezo huo uendelee.
“Mimi namuona kocha Bimkubwa hakati tamaa kwani anatutia moyo mpaka tunajikuta nasisi kwenye mchezo huu hatuwezi kuukosa.
Ali Khamis ni mmoja wa waalimu waliomfundisha kocha Bimkubwa anasema miongoni mwa wanafunzi wake, lakini ni mmoja wa wanafunzi bora mwenye bidii hadi leo hii.
Anasema wanajivunia kuwa Mchangamdogo pamoja na changamoto ya mchezo huo, lakini wanajulikana kupitia mchezo huo chini ya kocha Bimkubwa.
Anasema ni vyema makocha wakatambulika na wapatiwe nafasi za kusoma ukocha , hasa kwa wale wenye malengo ya kuendeleza mchezo.
Makamu Mwenyekiti chama cha mpira wa pete ‘CHANEZA ‘ Wilaya ya wete Idrissa Maulid Othman, anasema sifa ya Bimkubwa si mtu wa kukata tamaa, aliweza kujitia moyo na kuukubali mchezo wa mpira wa pete tokea akiwa mwanafunzi hadi akiwa kocha wa kuaminika.
Anasema ni mwanamke anaejitolea kwa hali na mali kuhakikisha mpira wa pete unaendelea.
Kai Bakar Ali ni mume wa kocha Bimkubwa anasema hapo awali, hakuwa tayari mke wake kushiriki katika michezo kutokana na mazowea ambayo jamii ilikuwa nayo ya kuwa mwanamke, hafai kushiriki michezo.
Anasema pamoja na kuwa jamii, ilikuwa na muono huo wa kuwa mwanamke si wa kushiriki michezo lakini kwa sasa yuko tofauti.
“Kilichonifanya nikubali mke wangu kushiriki katika michezo ni baada ya kupata elimu kutoka TAMWA-Zanzibar na mimi akanielimisha na nikaona kama kuna umuhimu mkubwa, kwa mwanamke kushiriki michezo”,anasema.
Afisa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi kwenye michezo unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la kimataifa la Ujerumani Khairat Haji anasema, kila mtu anayo haki ya kushiriki michezo na hakuna sababu ya wanawake kubakia nyuma.
Ndio maana anasema kupitia mradi huo TAMWA Zanzibar, itahakikisha usawa wa kijinsia unapatikana katika michezo ya aina mbali mbali.
Pamoja na kuwa wanawake wako nyuma katika ushiriki wa michezo, aliwataka wasirudi nyuma na washiriki kwa hali ya kuridhisha.
“Katika program hii tunamshirikisha mtoto wa kike kwenye michezo kutowa maoni yao kupitia changamoto wanazokutana nazo.
Sera ya michezo ya mwaka 2018 imeelezea utaratibu na uendeshaji wa michezo mbalimbali katika makundi tofauti ikiwemo michezo na mazoezi kwa wanawake.
Iliendelea mbele sera hiyo kuhusu juhudi zitakazofanyika ni pamoja na kuandaa na kufanya kampeni za kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo.
Katika ujenzi wa viwanja sera inasema Serikali katika ngazi zake zote kwa kushirikiana na wananchi itahakikisha kwamba vinakuwepo viwanja bora na vya kutosha na yatatengwa maneno maalum kwa ajili ya viwanja vya michezo na kambi mbalimbali.
Waziri wa habari, vijana, utamadini na michezo Tabia Maulid Mwita anasema katika harakati za kimichezo nchini wizara imeweza kufunga mkataba na shirika la kimataifa la Ujerumani (GIZ) wanaofadhili ujenzi wa viwanja vinne vya michezo midogo midogo (6 in 1 ) Unguja na Pemba.
Maneno yatakayojengwa viwanja hivyo ni pamoja na mkokotoni na mnazimmoja kwa Unguja na Mchangamdogo na Kangani kwa Pemba.
Hayo yamebainika wakati Waziri wa habari, vijana utamadini na michezo Tabia Maulid Mwita akisoma bajet ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Akasema maandaliziya ujenzi wa viwanja hivyo tayari tokea mwezi mei 2023 .
Ili vijana wa kike waweze kushiriki katika michezo ipasavyo na waweze kupata faida zitokanazo na michezo ni jukumu la kila mmoja kupitia nafasi yake kuhakikisha watoto wa kike wanaungwa mkono ili kuweza kukuza vipaji vyao vya michezo.
mwisho
|
Comments
Post a Comment