Na Salma Lusangi
WAZIRI wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaibu Hassan Kaduara ameagiza
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuwatafuta na kuwachukulia hatua mafundi wa
maji wa mitaani ambao wanaunga maji kwa wananchi kinyume na Sheria zilizoekwa
na Wizara yake.
Akizungumza katika kikao na uongozi pamoja na wafanyakazi wa ZAWA huko
Gombani, Pemba mwishoni mwa wiki aliwataka watendaji hao kuwatambua wateja wao pamoja na kuwasaka mafundi wa maji
wa mitaani ambao wanaunga maji kwa watu kinyume na Sheria.
Alisema Wizara ya Maji, Nishati na Madini kupitia taasisi yake ZAWA
imeshatoa muongozo kwamba watu wanaohitaji kuungiwa maji wafike katika ofisi
hiyo kwaajili ya kujisajili.
“ ZAWA hamuwajui wateja wenu, hamuwatambui mafundi wa mitaani! Mapato ya
maji yanapotea kwasababu hamjawajibika ipasavyo. ZAWA watambueni wateja wenu,
mafundi wa mitaani wanaowaungia watu maji kinyume na sheria ”. Alisema kaduara
Pia alisisitiza umuhimu wa ZAWA kujipanga katika kukusanya mapato ya
maji. Alisema endapo taasisi hiyo itajipanga vizuri katika ukusanyaji wa mapato
basi wataweza kujilipa mishara mizuri sana na fedha zingine zitabakia.
“Mkisimamia mapato vizuri basi mnaweza kujilipa mishara na pesa ya
chenji zitabaki, simamieni mapato vizuri, kwani siku za nyuma makusanyo yalikua
yanaenda vizuri, Mji wa Wete tu, mkisimamia vizuri basi mapato yataongezeka”
Alielezea Kaduara.
Aidha Waziri huyo alikemea tatizo la uwepo wa makundi ndani ya ofisi,
ununuzi wa vifaa ambavyo sio sahihi kwa maana ya kutokua na vigezo
vinavyotakiwa. Pamoja na kuwataka watendaji hao kusameheana endapo mtu
amekwanzana na mtumishi mwenzake. Alisema kwani bila ya kusameheana watendaji
hao hawataweza kufanya kazi kwa pamoja na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo
Joseph Kilangi aliwakumbusha watendaji hao nidhamu ya kazi, lugha nzuri kwa
wateja wao, umuhimu wa kusimamia
matumizi sahihi ya fedha kwa kufuata mfumo uliyowekwa na Serikali, pamoja na kuwahimiza kujibu hoja za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) haraka.
Aidha aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu wa kubuni miradi ya maendeleo
ambayo italeta tija kwa Serikali na wananchi. Alielezea kwamba kuna baadhi ya Idara/Taasisi
hazina miradi.
Aidha Katibu Mkuu huyo aliwataka mafundi wa ZAWA wasifunge mota za maji
bila ya kushirikiana na wataalamu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa
sababu mota zinaungua, hivyo Serikali inapata hasara zaidi ya milioni mia tano.
“Wizara yetu inamgusa kila mtu tujitahidi kuzuia malalamiko na kuzuia malalamiko
hayo ni kuwajibika, nidhamu, sisi
tuliyopo ofisini tunatakiwa tutowe ripoti ya miaka miwili ya uongozi wa Rais
Zanzibar Dk. Hussein kwa kuangalia ilani, hivyo timu iliyopo chini ya Afisa
Mdhamini Pemba itekeleze wajibu wao” Alisema Kilangi.
Mwisho
Comments
Post a Comment