NA HAJI NASSOR, PEMBA
KILA ifika Oktoba 1 ya kila mwaka, dunia huadhimisha
siku ya wazee.
Siku
hii kihistoria, iliaanzishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ‘UN’ kuanzia Disemba
14, ya mwaka 1990.
Ambapo
maadhimisho haya, ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Vienna wa mwaka
1982, kwa ajili ya wazee duniani,“The
Vienna International Plan of Action on Ageing”.
Ulioboreshwa
tena na Mkakati wa Madrid, Hispania wa mwaka 2002, ili kuweza kupambana na
changamoto za wazee katika karne ya 21, na kuendelea mchakato wa maendeleo
fungamani ya binadamu kwa ajili ya wote.
MWELEKEO NA HISTORIA
Maadhimisho
ya siku ya wazee duniani, ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa ‘UN’ katika kutambua na kuihamasisha jamii, kuwalinda na kutetea haki zao
msingi za wazee duniani kote.
Kwa
maadhimisho ya mwaka 2021, yalinogeshwa na kauli mbiu “Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa Ustawi wa Rika Zote.”
Inatambuliwa kuwa, takriban
watu milioni 700 kwa sasa, wamepindukia umri wa miaka 60, na ifikapo mwaka 2050,
watu bilioni 2, ambayo ni zaidi ya asilimia 20 ya idadi jumla ya watu duniani,
watafikisha umri wa miaka 60 au zaidi.
Kuongezeka kwa idadi ya
wazee duniani, litakuwa jambo kubwa na litakalokwenda haraka zaidi katika dunia
ya sasa, inayoendelea huku bara la Asia, likiwa na idadi kubwa ya wazee na
Afrika nayo ikifuata kuwa na idadi hiyo kubwa ya wazee.
Kwa kuzingatia hayo, wazee
wanamahitaji makubwa na kuzeeka au kuwa mkongwe hakuondowi utu na haki zao za
msingi za mwanadamu, kama inavyosema ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya
kuadhimisha siku kimataifa ya wazee duniani.
Umoja huo ulianzisha siku
hii, kwa lengo la kutoa ulinzi kwenye masuala ya uhuru, ushiriki, huduma,
heshima na utu wao.
Ingawa ripoti za utafiti za
hivi karibuni zinaonesha kwamba, wanawake na wazee hawapati nafasi sawa wanapohusika
masuala ya kidijitali.
Kwa sasa watu milioni 125
ni wazee, kuanzia umri wa miaka 80 kwenda juu, na serikali zikiendelea
kujipanga, ili kuhakikisha wazee wanaishi maisha mazuri na ya amani.
Katika hilo, Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, anasema wazee ni lazima wapewe kipaumbe
katika kukabiliana na ugonjwa, kama vile ukoma, corona, ukimwi na kifua kikuu.
Amesema ni lazima watu
waangalie namna wanavyowashughulikia wazee, katika maisha yao, ili wabaki
salama na kuishi kwa amani kama yalivyomakundi mengine.
‘’Kila
mkongwe (mzee) anahitaji heshima, na kutambuliwa utu na mchango wake kwa jamii
yake na taifa, ili kufikia malengo yake,’’anasema.
Kwa upande wa Tanzania
bara, Serikali ipo katika hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Taifa
ya Wazee ya mwaka 2003, kwa kushirikiana na wadau na imeendelea kutekeleza afua
mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wazee.
Hayo aliyasema waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima,
alipotembelea makazi ya wazee wasiojiweza ya Sukamahela kuelekea siku ya wazee duniani.
ZANZIBAR
Wakati dunia ikiadhimisha
siku ya wazee hapo Oktoba 1 hapa Zanzibar, ambapo rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akitarajiwa kuwa mgeni
rasmi, wazee wanakumbukwa mno.
Kwa Zanzibar, serikali
iliamua wazee kuanzia miaka 70, walipwe pencheni jamii ya shilingi 20, 000 kila
mwezi, hata kama wazee hao, hawakuwa watumishi wa umma.
Amekuwa akirejea kauli yake
kuwa, azma ya kupunguza umri huo ili kuangalia uwezekano wa miaka 65 walipwe
pencheni jamii, linafanyiwa kazi kwa haraka.
‘’Wazee wetu fedha
mnazopata za shilingi 20,000 kwa kila aliyefikisha umri wa miaka 70, ni ndogo
na tunajua kuwa maisha yamepanda, lakini tunangalia uwezekano wa kuongeza fedha
hizo na kupunguza umri,’’alieleza.
KAULI YA WAZEE KUELEKEA SIKU YAO
Ali Haji Ali wa Pujini,
anasema yapo mambo mazuri ya kujivunia, ambayo, yanatokana na matayarisho na
kuweka mazingira rafiki na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
‘’Hata kupewa pencheni
jamii za shilingi 20,000 ni eneo moja, lakini hata kuwepo kwa madirisha maalum
ya kutokewa dawa kwenye hospitali za serikali, nalo ni zuri,’’anasema.
Mwanajuma Issa Haji ‘Mwaju’ anasema, wazee wote
wanakabiliwa na changamoto, ingawa wanawake ndio wanaongoza kwa kutelekezwa.
‘’Wazee tunakabiliwa na
changamoto za kutelekezwa na familia na wakati mwengine huwa tunajiingiza
kwenye omba omba bila ya kupenda, jambao ambalo sio zuri,’’anasema.
Mussa Iddi Mussa wa Wawi,
anasema wakati umefika sasa kwa jamii, kuungana pamoja katika kuwalinda wazee,
ili nao waishi kwa salama na amani.
VIONGOZI WA SERIKALI
Mkuu wa mkoa wa kusini
Pemba Mattar Zahor Massoud, anasema kila mmoja, kwa wakati huu awatendee mema
na mazuri wazee, maana uzee ni njia kila mmoja atapita.
‘’Kama kuna sheria ambayo
inakandamiza kundi la wazee, muda ndio huu kwa vijana wa leo, kuzirekebisha ili
kesho na keshokutwa ziwafae na wao,’’anashauri.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani
Khatib Juma Mjaja, anasema hakuna namna ya wala mbadala, juu ya kuwatunza na
kuwaenzi wazee, maana ndio wazazi wa vijana wa leo.
Anasema, wakati huu
Zanzibar ikitarajiwa kuungana na dunia katika maadhimsho ya siku ya wazee hapo Oktoba
1, kila mmoja na kwa nafasi yake, awatunze wazee.
‘’Angalia eneo la kazi
ulipo, kama ni hospitalini, dereva, kiongozi sehemu za kazi, mwanasheria na
mwengine atumie nafasi yake kuwasaidia wazee,’’anasema.
Aliyekuwa Afisa mdhamini
wizara ya Afya Pemba dokta Yakoub Mohamed Shoka, aliwahi kusema kuwa, suala la
kuwa mzee na kubezwa kwa haki zao halihusiani.
WADAU WA HAKI ZA BINADAMU
Mratibu wa Kituo cha Huduma
za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Zanzibar ofisi ya Pemba Safia Saleh Sultan, anaona moja
ya jukumu la kisheria kwa jamii, ni kuwatunza wazee.
Mwanasheria wa kujitegemea
Mohamed Hassan, anasema haipendezi kwa familia, kuacha kumlea mzee wao na
kumkabidhi serikalini.
‘’Matunzo ya wazee walioko
serikalini, huwa mara nyingi ni wale waliokosa watunzaji madhubuti, na hivyo ni
vyema kuhakikisha familia inawalea wazee,’’anaeleza.
Aliyewahi kuwa mjumbe wa
jumuiya ya wazee na wastaafu Zanzibar kwa upande wa Pemba Sifuni Ali Haji,
anasema licha ya serikali kuweka mazingira rafiki kwa wazee, lakini utekelezaji
bado hafifu.
‘’Siku ya wazee duniani ni
jukwaa kwa wazee na watetezi wa haki zao, kujadili changamoto na mafanikio yao,
ili kuona mwelekeo wa baadae,’’anasema.
VIJANA
Mratibu wa vijana Pemba Ali
Mussa, anasema kama vijana wa leo, wanaelewa iko siku atakuwa mzee wa nchi hii,
ahakikishe sasa wanatengeneza mazingira imara kwa wazee.
Kijana Kheir Juma Mrisho,
anasema haipendezi kuona vijana wanawadhalilisha wazee, kwa sababu ya kukosa
uwezo wa kimwili na fedha, maana uzee ni kama barabara.
‘’Vijana wa leo, lazima
tukumbuke kuwa kesho sisi ndio wazee, hivyo maslahi yao na haki zao zitunzwe,
ili hapo baadae zetu iwe rahisi,’’anasema.
Siku ya wazee duniani,
huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 1 ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu, rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Katika maadhimisho, Dk.
Mwinyi anatarajiwa kuwakabidhi wazee 689 wa mkoa wa mjini wa Magharibi Unguja,
vitambulisho maalum, ambavyo watavitumia katika maeneo mbali mbali.
Kwa mujibu wa waziri wa
wizara ya Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Riziki Pemba
Juma, anasema, vitambulisho vyengine 24,000 vinaendekea kuvitengeneza na baadae,
vitasambaazwa kwa wazee wengine ambapo Zanzibar ikikadiriwa kuwa na wazee
28,706.
Mwisho
Comments
Post a Comment