Na Salma Lusangi
WAZIRI wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaibu Hassan Kaduara, ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kufikisha huduma ya umeme haraka sehemu ambazo wananchi wameekeza kilimo ili waweze kuzalisha kwa gharama ndogo na nafuu.
Aliyasema hayo leo wakati akizungumza watendaji wa shirika hilo Tibirizi Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Alisema mkulima yeyeto akifikishiwa huduma ya umeme ataweza kuzalisha mazao kwa gharama ndogo hali hiyo itapelekea bidhaa kuuzwa kwa bei ndogo kwasababu alizalisha kwa gharama ndogo.
Alifahamishwa kwamba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameshatoa agizo nguzo za umeme zitolewe bure kwa wananchi, hivyo ZECO harakisheni kuwafikishia wananchi nguzo za umeme hasa kwa wanaodhalisha mazao mbali mbali ili wapate urahisi wa kuzalisha bidhaa zao.
“ZECO kwanini mnachelewesha kufikisha nguzo za umeme kwa watu wanaozalisha, acheni kuzipigia hesabu gharama za nguzo, hizo peza sio za mtu binafisi ni za serikali,'alieleza.
Pia Waziri huyo amewataka watendaji wa ZECO kuwajibika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi wanaohitaji kufungiwa mita za umeme majumbani mwao wakati wameshalipa gharama zote za fedha zilizohitajika.
Alisema hali halisi ya ZECO ilivyo kwa sasa sio ya kusemwa vibaya lakini bado watendaji wa ZECO hawajawajibika ipasavyo hivyo endapo ataendele kupata malalamiko ya wateja kwamba wameshalipa lakini ZECO hawajatimiza wajibu wao wa kuwafungia mita wateja ameahidi atawafukuza kazi baadhi wa watendaji wa Shirika hilo kwa kutokuwajibika.
“ Siko tayari kutolewa madarakani kwasababu ya wafanyakazi wa ZECO kutokuwajibika, nitawafukuza wafanyakazi hata mia (100), kama mtu hana uwajibikaji kwanini aendelee kubaki katika Shirika! Mnafanyakazi kwa uzembe. Mtu akiniharibia tutaharibiana, ukinizingua tutazinguana.Wajibikeni kwanza na baadae mdai haki zenu.Waziri huo alieleza kwamba anafahamu wafanyakazi wa ZECO wanadai mishahara yao hivyo ameagiza Utawala wa ZECO kuhakikisha kila mtu anapata haki yake anayodai pamoja na kupewa muongozo wa majukumu yake ya kila siku (Job Descriptions) kwamujibu wa sheria na kanuni za Utumishi.
Aidha aliwataka watendaji wa ZECO kusimamia mapato ya huduma ya umeme na kujiepusha na vitendo vya kuhujumu uchumi, kwani katika zoezi la kuwafungia watu mita na kuwasaka watu wanaojiungia umeme kinyume na sharia (Kadua Operesheni) aliwakamata watu sita ambao wanahujumu uchumi.
Naye katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph Kilangi aliwataka watendaji wa Shirika hilo kutumia vizuri vifaa vya Serikali, kufuata taratibu za manunuzi pamoja na kuongeza mashirikiano baina yao ili kuleta ufanisi katika majukumu yao.
Pia aliwasisitiza wafanyakazi hao kujiepusha na kosa la utoro kazini pamoja na kutekeleza maagizo yote yalitolewa katika kikao hicho yatekelezwe kwa wakati ikiwemo kuwafungia wateja mita, nguzo za umeme kufikisha maeneo ya wakulima kwa wakati. Alisema anahitaji kupata ripoti nzuri.
Kwa upande wao wafanyakazi wa ZECO waliomba kupatiwa mafunzo ya fani tofauti, pamoja na vitendea kazi ikiwemo gari, viatu pamoja na kulipwa maposho yao ya kufanyakaza kwa zaidi ya saa za kazi zilizoekwa kisheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment