NA HAJI NASSOR, PEMBA
SHEHIA ya Tumbe Mashariki wilaya ya
Micheweni Pemba, inawakaazi 7,675 kati ya hao, ni wananchi 225 wanaoendelea
kupokea rukuzu kutoka TASAF.
Kati hao,
wapo wananchi 20 kutoka ndani ya mpango huo sasa, wameamua kujiajiri na
kuendesha maisha yao, kwa kuanzisha miradi kama vile biashara na kilimo cha mboga
mboga.
Shehia ya
Tumbe iliyoko wilaya ya Micheweni Pemba, ni kati ya zile shehia 78 zinazoendelea
kuhudumiwa na TASAF, kwa wananchi wake kuendelea kupokea rukuzu.
Maana TASAF,
inao walengwa 14, 280 kwa wilaya zote nne za Pemba, ambao hao wapo walioanzisha
vikundi vya ushirika iwe ni utengenezaji sabuni, mboga mboga, ufugaji ama
biashara.
Katibu wa
sheha wa shehia ya Tumbe Mashariki, Makame Hassan Makame, anasema moja ya
shehia ambazo TASAF imeacha alama ya mafanikio, ni yao kwao.
‘’Wapo walengwa
wa kunusuru kaya maskini 20, hawa sasa hatuwatarajii kurudi tena kwenye
umaskini wa kipato, kama ilivyokuwa kabla ya ujio wa TASAF,’’anaamini.
Pamoja na hao mmoja mmoja, lakini wapo
walioanzisha ushirika wa biashara kilimo cha mboga, ufugaji na hata vikundi vya
kuweka na kukopa.
Hapa
akatolea mfano ushirika wa ‘kiumbe mzito’ ambao umekusanya wanawake 20, na sasa
wameshaanza kufikia pahala pazuri kimaisha.
‘’Ushirika
huu ni wale walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini, na waliamua
kujikusanya kwenye kuweka na kukopa na sasa wameanzisha ushirika wa duka la nguo
na vipodozi,’’anaeleza.
Katibu
anasema, mfano wa vikundi kama hivi shehiani mwake, vipo wengine wanaotengeneza
sabuni, kilimo na ufugaji wa kuku.
USHIRIKA WA ‘KIUMBE MZITO’ ULIANZAJE?
Ushirika huu,
ni zao la mpango na mikakati ya TASAF ambapo ilikuwa ikiwataka walengwao hao,
kuhakikisha ruzuku wanayoipata inazaa matunda.
Hapa Mratibu
wa TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, anasema pamoja na uwepo wa vikundi 942,
lakini ushirika wa kiumbe mzito ni mfano mzuri ndani ya TASAF.
Maryam Haji
Khatib ni Mwenyekiti wa ushirika huo, anasema baada ya kupokea ruzuku kutoka
TASAF na wakiwa kwenye ushirika wa kuweka na kukopa, walizaa wazo la kuanzisha ushirika
huo wa duka.
Ijapokuwa,
wapo waliotamani kuanzisha duka la chakula, lakini kwa wakati huo, waliafikiana
kuanzisha duka la kivazi, kama nguo za kike na viatu.
Kwenye
ushirika huu, ambao unawanachama 18, kila mmoja kwa kuanzia alichanga shilingi
5,000 na kwa hatua za mwanzo wakajipatia shilingi 90,000.
Kisha
waliendelea na mchango kwa miezi minne, na wakajitilia kibindoni shilingi
700,000 kwa dhamira ya kuanzisha ushirika huo wa duka la viatu na nguo.
‘’Kwa hatua
za mwanzo tulinunua nguo za watoto, viatua aina ya yebo yebo, vishungi, kanga,
mahafu, sidiria, shati, suruali na badhi ya vipodozi,’’anasema Mwenyekiti.
Ushirika huo ambao uliasisiwa mwaka 2019, hauwajahi kugawa faida, ingawa hadi mwishoni mwa mwaka 2021, baada ya kufanya hesabu, walijikuta na mtaji wa shilingi milioni 1.
Ambapo baada ya kutoa mtaji wa shilingi 90, 000 wamejikuja na faida ya shilingi milioni 1 na elfu kumi.
Fatma Hamad
Mkandi, ni Katibu wa ushirika huo wa ‘Kiumbe Mzito’ anasema hawajagawa
faida, kutokana na kuwa na ushirika wa kuweka na kukopa.
Anasema,
wote waliomo kwenye ushirika wa duka, wanakutana kwenye ushirika wa kujiwekea
fedha na kukopa, ambako wanachama hukopeshwa.
‘’Jinsi
ushirika wetu unavyokwenda kwa sasa hata akitokea mfadhili akitukopesha
shilingi milioni 200 tunajiamini kuzichukuwa na kurejesha taratibu.
‘’Kama
tukikopeshwa fedha hizo, kwanza tutanunua mashine za kukobolea nafaka, mashine
ya kutengenezea sabuni, masheni ya kutotolea vifaranga na kujenga ofisi
yetu,’’anaelezea ndoto zao.
Katibu anasema
malengo yao ya baadae, ni kuona kila mwanachama kati ya wale 18, awe anajitegemea
katika kuendeleza maisha yake.
''Tunatamani iwe suala la shilingi 100,000 hadi shilingi 500,000 kwa mwanachama anapohitaji kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake,''anasema.
Kwa sasa,
hali ya maisha kwa wanachama wao, imebadilika hasa baada ya kuwa na sehemu ya
uhakika wa maisha ‘kukopa’ ambapo hapo kabla hawakuwa na pakwenda.
Yupo
mwanachama ambae aliwahi kupata msiba kisiwani Unguja, na alifika kwenye
ushirika na kikundi, na kukopeshwa shilingi 100,000.
‘’Hata mimi
niliwahi kukopa shilingi 200,000 kwa ajili ya matibabu ya mtoto wangu na yupo
mwengine alikopa hadi shilingi milioni 1, na baada ya miezi sita
alirejesha,’’anasema.
Hapa mshika
fedha wa ushirika huo Awena Shavuu Abdalla, anasema kwa siku msimu kama wa sikukuu, huuza kati ya shilingi 80,000 hadi shilingi 100,000.
Anasema kwa
sasa, wanaendelea kuutumia mlango wa kuazimwa, ingawa wanatarajia kuona
wanakuwa na wao ili kupunguza gharama.
KABLA YA TASAF
Kwanza
hawakufikiria kuanzisha ushirika wa duka wala mpango wa kuweka na kukopa,
kutokana na kukosa chanzo cha kuyafanya hayo.
Asiya Faki
Suleiman, ambae ni mwanachama, anasema hali ya ukosefu wa kipato kwake ilikuwa
ya kawaida, na hakuja wapi aende.
‘’Hata
ukibahatika kumpata mtu, lakini sio kumuazima fedha, labda nguo ama chakula,
maana kila mmoja kwa hapa kijijini kwetu, fedha ilikuwa ngumu,’’anasema.
Anakumbuka vyema,
hakuwa mtu wa kutoa mchango wa harusi, ugonjwa wala matanga katika familia
yake, kutokana na kukosa shughuli ya kufanya ya kujiingizia kipato.
Fatma Hamad
Mkandi, anasema kipato kwake kilikuwa kizito, hadi anapoamua kwenda kwenye
kilimo cha mwani, ambako fedha yake haina haraka.
‘’Utegemee
mwani mpaka ukauke, na kisha waje wanunuzi kwa siku watakazo, na hapo ukimaliza
kuuza ni kulipa deni, ambalo umekopa,’’anasema.
TASAF
Mratibu wa
TASAF Pemba Mussa Said, anasema wapo walengwa 14, 280 kwa Pemba ambao
wanaendelea kupata fedha za kunusuriwa na umaskini.
Walengwa hao
wapo kwenye shehia 78, ikiwemo ya Tumbe Mashariki, ambapo tayari shilingi
bilioni 14. 4 zimeshwafikia.
‘’Mtu kama
bi Fatma ndio hasa malengo ya TASAF ya kumtoa mwananchi katika unyonge, na
kumleta kwenye taa, ili nae aishi maisha mazuri,’’anasema Mratibu.
“TASAF
inaorodha ya zaidi ya walengwa 50,000 kutoka wastani wa walengwa 15 kila
shehia, kati ya shehia 78, ambao wamenzisha miradi ya kujikwamua.
“Mtu kama bi
Fatma wa Tumbe, Amina wa Mgogoni, Mfaki wa Kwale Gongo na Maryam wa Ukunjwi
ambao hatuna shaka, hawawezi kurudi tena kwenye umaskini mzito wa kipato,
wanafikia 50,000 kwa Pemba yote,’’anaeleza.
Mratibu
Mussa anabainisha kuwa, kwa mwaka 2014/2015 walengwa hao wa kunusuru kaya
maskini, waliibua miradi ya kijamii 41, idadi iliongozeka mwaka uliofuata kwa
kufikia miradi 84.
Mwaka 2017
hadi mwaka 2018, walijukuta na miradi mengine ya kijamii 21, inayuhusisha
upandaji miti kama shehia ya Makangale, uazishwaji wa vitalu na ujenzi wa
matuta ya kinga maji ya bahari Ndagoni, Kiwani, Micheweni na Tumbe.
Achia mbali
idadi ya watu 50,000 waliojiwekeza wenyewe, vipo vikundi 942 vikizaa walengwa
12,000 vilivyoanzishwa, kuanzia mwaka 2014 hadi sasa.
WANANCHI WA KAWAIDA
Rukia Omar
Kheir, anasema fedha zilizoekezwa kunusuru kaya maskini kutoka TASAF,
zimetumika vizuri kwa vile matunda yanaoonekana kwenye shehia yake.
‘’Kama TASAF
ikiondokana inataka kuacha alama ya maendeleo, basi mfano mzuri ni kwa shehia
ya Tumbe Mashariki, ambapo sasa wanawake wameshaukimbia umaskini kwa
vitendo,’’anasema.
Hata Aisha
Issa Hassan na mwenzake Is-mail Haroun Juma wanasema, kilichobakia kwa sasa ni
tasisi nyingine kuvilea vikundi kama hivyo.
WATEJA WAO
Omar Haji Issa na mwenzake Khadija Bakar Juma wanasema, sasa hawafuti tena huduma za nguo na viatu Wete mjini (kilimo 30) baada ya ushirika huo kuweka duka.
Mwisho
Comments
Post a Comment