NA ZUHURA JUMA, PEMBA:::-
MAHAKAMA ya Mkoa
Wete imemuhukumu kijana Ali Sharif Ali miaka 19 mkaazi wa Pandani, kwenda kutumikia
chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 20 na kulipa fidia ya shilingi 100,000 baada
ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto mwenye miaka 15.
Akisoma hukumu hiyo hakimu wa mahakama ya Mkoa B Wete Ali
Abrahman Ali amesema, mahakama imemtia hatiani kijana huyo baada ya kupatikana
na kosa hilo.
Alisema kuwa, mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande
wa mashitaka, kwani wamethibitisha shitaka pasi na kuacha chembe ya shaka na
ndio maana mahakama imemuamuru kwenda kutumikia chuo cha mafunzo miaka 20
pamoja na kulipa fidia ya shilingi 100,000.
“Tumemtia hatiani mshitakiwa huyo chini ya kifungu 220 cha Sheria
ya Mwenendo wa Jinai nambari 7 ya mwaka 2018 sambamba na kifungu cha 115 (1)
cha Sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, Sheria za Zanzibar”, alisema
hakimu huyo.
Mapema upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Juma Mussa
kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, uliiomba mahakama hiyo, kutoa adhabu
stahiki kama ilivyoelezwa kwenye Sheria, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine
wenye tabia kama hiyo.
Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, mshitakiwa alipewa fursa ya
kujitetea, ambapo aliiomba mahakama impunguzie adhabu, ombi ambalo limekataliwa
na mahakama.
Awali mshitakiwa huyo ilibainika kuwa alitenda kosa hilo Disemba
11 mwaka jana, majira ya saa 1:30 usiku eneo la Kijuki Pandani, Wilaya ya Wete
Mkoa wa Kaskazini Pemba, alimlawiti mtoto menye umri wa miaka 15, jambo ambalo
ni kosa kisheria.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 115 (1) Sheria ya Adhabu
nambari 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzibar.
Kesi hiyo yenye kumbu kumbu namba RM 2/ 2022 kwa mara ya
kwanza, ilianza kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa B Wete Januari 13 mwaka
jana, ambapo jumla ya mashahidi 6, walifika mahakamani na kutoa ushahidi
kuhusiana na kesi hiyo akiwemo mtoto mwenyewe.
MWISHO.
Comments
Post a Comment