NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::-
MKUU
wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema ameridhishwa na
matayarisho ya awali, yaliyofanywa na wajumbe wa Kamati maalum ya maadhimisho
ya siku ya mtoto wa Afrika, kisiwani humo.
Alisema, kamati hiyo imeibua jambo kubwa la kutaka
kufanya maadhimisho hayo, na kujipanga kwa kufanya shughuli mbali mbali, kabla
na wakati wa kilele chenyewe ambacho ni Juni 16, mwaka huu.
Alisema ameridhishwa na mpango huo wa maadhimisho na
kuahidi kushirikiana nao, hadi kukamilika kwake siku ya kilele hicho
kinachotarajiwa kufanyika uwanja wa Gombani.
Mkuu huyo wa mkoa aliyasema hayo Juni 11, 2022 ofisini
kwake Chake chake, wakati akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, waliofika
ofisini kwake, kuwasilisha mpango pendekezwa wa kilele hicho.
Alisema, suala la kuwashirikisha watoto ambao ni
wanafunzi na kuwaandalia michezo mbali mbali kama ushindani kwenye elimu, ni
jambo linalofaa kuungwa mkono.
‘’Kwanza niwapongeze wajumbe wa kamati hii, kwa uamuzi wao wa kutaka kushirikiana na kuiunga mkono serikali yetu, katika kutetea na kulinda
haki za mtoto,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa, aliitaka kamati
hiyo, wawasiliana nae kila wakati, na ikiwa kuna jambo limekwa, kuona njia gani
ya kulitatua.
‘’Kwenye usafiri, majukwaa na hata kikundi cha brass band
na gharama nyingine, nitaangalia uwezekano wa kushirikiana na wenzangu
kuzitekeleza,’’alifafanua.
Mwenyekiti wa muda wa kamati hiyo Nassor Bilali Ali,
alimpongeza mkuu huyo wa mkoa, kwa uamuzi wake, wa kuzibeba gharama za
utekelezaji wa sherehe hizo.
‘’Kwa niaba ya wajumbe wa kamati, tunakupongeza kwa hatua
zako na kuona sherehe hii ya kutetea haki za mtoto zinafanyika kwa ufanisi,’’alieleza.
Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, Mwanaisha Ali Massoud,
alisema mfano wa viongozi kama Mkuu wa mkoa, ndio ambao wanaweza kufanikisha
mambo kadhaa.
‘’Kwa hakika ilionekana dhahiri tumeshakwa kuiadhimisha
siku hii, lakini kutokana na umahiri, utayari na kuumwa kwake na haki za
watoto, ndio maana ameamua kusaidia eneo kubwa,’’alieleza.
Wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Siti Habib Mohamed kutoka
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, alisema watoto lazima waandaliwe
zawadi maalum.
‘’Kwa vile tumeamua kuweka michezo kama ya kuokota
mbatata, kuvuta kamba, mbio za magunia, masuali ya papo kwa papo, ni vyema
washindi wakatunzwa,’’alipendekeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tumaini Jipya
Pemba TUJIPE, Tatu Abdalla Msellem, alisema moja ya changamoto zinawazowakabili
watoto, ni janga la udhalilishaji.
‘’Hivyo kama tumepanga tutakua na masuali ya papo kwa
papo, basi hata kuwauliza nini maana ya udhalilishaji, hatua gani utazichukua
ukimkuta aliyedhalilisha na mengine yanayofanana na hayo,’’alishauri.
Awali Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali,
aliitaka kamati hiyo, kuyafanya maadhimisho hayo kuwa ya kitaifa kisiwani Pemba
badala ya kuadhimishwa kiwilaya.
Kamati hiyo inaundwa na Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar ZLSC, Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Pemba ‘JUWASPE, Jumuiya ya
Tumaini Jipya Pemba TUJIPE, na Zanzibar Social Workers Association ZASWA.
MWISHO
Comments
Post a Comment