NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
Ni takribani dakika 25, kutoka katika ufukwe
kwa bandari ya Tumbe, hadi kufikia kwenye kisiwa cha Ndege ‘Khamis’ kilichopo
katika eneo la Tumbe ndani ya bahari ya Hindi.
Ilikuwa majira ya
saa 3:00 asubuhi, boti iliyobeba maafisa wa wizara ya utalii na mambo ya kale, ikiwasili
katika kisiwa Ndege kinachojulikana kwa jina la (kisiwa khamis).
Hali ya hewa
ilikuwa ni ya mawingu mawingu, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku mzima
wa kuamkia siku hiyo, boti hiyo aina ya mashua, ilibeba takribani ya watu 30.
Katika msafara
huo, jemedari wa Wilaya hiyo Mgeni Khatib Yahya amekiongozana na mwenye dhamana
ya Wizara ya utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni Othman, na maafisa
wengine.
Safari hiyo,
haikubeba maafisa hao, tu bali ilikua na watu ambao wanaipasha jamii habari,
kutoka vyombo mbali mbali vya habari.
Ziara hiyo, iliyofanywa
na Wizara ya Utalii, ilikua na lengo la kutembelea kisiwa hicho, kukitangaza
rasmi kiutalii, kikiwa ni kivutio kipya.
Kwani, kwa miaka
zaidi ya miaka 70 iliyopita, hakikuwemo kwenye orodha ya vivutio, ambavyo
vimetambuliwa Kisiwani Pemba.
Kilipo kisiwa ‘Khamis’
ni takribani ya kilomita 3, hadi ilipo bandari ya Tumbe Wilaya ya Micheweni
Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kisiwa hicho
chenye urefu wa wastani wa viwanja viwili vya mpira wa miguu ‘mita 230’ kikiwa
na upana wa kiwanja kimoja na nusu cha mpira wa miguu ‘mita 160’.
Miti mirefu
mchanganyiko, iliyotawala ubichi iliyojengeka kwa vichaka na hali ya hewa
mwanana, huku ukikaribishwa na miito ya ndege aina 12, ndio mandhari
inayowavutia wageni na wenyeji.
AINA YA NDEGE WALIOPO KISIWA KHAMIS
Aina hii ya ndege
12 waliopo katika kisiwa hicho, wala sio rahisi hata kidogo kuwakuta ndani eneo
jengine pasi na kisiwa hicho.
IDARA YA MAKUMBUSHO NA MAMBO YA KALE PEMBA
Khamis Ali Juma, ambae
ndie Mratibu wa Idara hiyo, anakiri kuwa, upya wa ugunduzi wa kisiwa hicho,
bado ni mapema kuelezea sababu ya kuitwa kisiwa ‘Khamis’.
Ijapo kuwa
wakaazi wa eneo la Tumbe na hasa wavuvi walikipachika jina la ‘Kisiwa ndege’
kutokana na kuzagaa kwa idadi kubwa ya ndege.
Mratibu Khamis
anasema, ugunduzi wa kisiwa hicho ni kuelekea kuengeza idadi ya vivutio vya
utalii Kisiwani Pemba.
‘’Ni mwaka huu wa
2022 tu, ndio tumekigundua kisiwa hichi, na rasmi sasa tumeshakiingiza kama ni
kivutio kipya cha kiutalii Kisiwa Pemba,’’ anasema.
Anaainisha kuwa,
kuwa juhudi zikiendelea za ugunduzi wa vivutio vya utalii kama ‘kisiwa ndege’
ni ile dhana ya kuongeza idadi ya utalii Pemba, haitokua mbadala.
Historia ya Pemba,
imeanza kukatika kutoka kisiwa cha Bara zaidi ya miaka milioni 5 iliyopita,
ilijigawa na kupatikana visiwa vidogo vidogo ikiwemo cha Pemba.
Kisiwa cha Pemba nacho,
kimeanza kukatika na kutengeneza visiwa vidogo vidogo kama vile Mkumbuu.
Ingawa kuna nguvu
iliyotumika ya kujengwa daraja la kuungaisha mto uliopita, vyenginevyo eneo
hilo lingekua tayari ni kisiwa.
“Licha ya daraja
na mto uliopo, lakini kutokana na mazingira yaliyopo baada ya miaka kadhaa,
Mkumbuu wilaya ya Chake chake, itakuwa kisiwa ambacho kitajitegemea,’’anasema.
Hili Mratibu huyo
anasema, kwani sasa hivi tayari kuna mito miwili inayoingiliana baina ya upande
mmoja na mwengine.
ASILI YA KISIWA NDEGE
Ni ndege wa aina
tofauti, ambao wanaingia na kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Eneo moja ni kama
vile Ulaya na kwenda kuishi kwa muda ndani ya kisiwa hicho na kuondoka.
“Kuna ndege wa
pwani, wao wanatumia bahari kwa kutafuta chakula chao, kuna ndege aina ya Yangeyange,
Makoho, Kunguru, Vijafara, Membe pamoja na Njiwa ambao wanakipamba kisiwa hichi”,
anasema.
Ndege aina ya
Membe ni ndege ambao wanalia kuashiria maji kutoka na kuingia, na mara nyingi
wavuvi wanawatumia kujua maji yanapoingia au kutoka.
WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE
‘’Ndege ni sehemu
ya utalii, wapo wageni ambao ni wanafanya utafiti, ambao hupenda kuona ndege au
kuwinja, ndipo wizara ilipoamua kutembelea, ili kukitangaza kisiwa hicho,’’
anasema.
Anasema kuwa, ndege
waliopo katika kisiwa hicho hawapatikani kwengine popote duniani, ambapo hilo
ni jambo la kujivunia.
Licha ya
rasilimali ya ndege iliyopo kwenye kisiwa hicho, lakini pia ardhi yake ni ya
mwamba wa mawe na udongo wa aina ya tifu tifu.
Kwa upande wa
wizara, imejipanga vyema kwa kukiimarisha kisiwa hicho, ili kiweze kuleta faida kubwa
kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
MKUU WA WILAYA
Mkuu wa Wilaya ya
Micheweni Mgeni Khatib Yahya, aliwataka wananchi kukitunza kisiwa hicho, kwa
kurejesha msitu ambao ulikuwepo awali.
Anasema, kisiwa
hicho ni moja kati ya vivutio muhimu cha utalii kwa Wilaya hiyo, hivyo
aliwataka wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo, kulima kilimo
kinachoendana na mabadiliko ya tabia nchi.
Anaeleza, kisiwa
hicho endapo jamii itashindwa kukitunza, kitaathirika na ndege ambao wanaishi
humo, wataondoka na kupoteza historia.
‘’Mandhari, uzuri
na utamu wa kisiwa ndege ni kuwepo kwa ndege aina 12, kama ilivyo sasa, endapo
shughuli za binaadamu zitawakimbiza ni kupunguza utamu wa historia,’’ anaeleza.
Binafis alifarajika
kukitembelea kisiwa hicho, ambacho kina mandhari nzuri na haiba ya kuvutia, na
kina mazalio ya ndege tofauti.
Mkuu huyo, aliwataka
wananchi wa Pemba kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo ya kihistoria, ili kujifunza
na kujionea utalii ambao upo ndani ya kisiwa chao.
AFISA MAZINGIRA WILAYA YA MICHEWENI
Afisa Mazingira
Wilaya ya Micheweni Salum Mjaka Ali anasema, kisiwa hicho kwa sasa, kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi kimeathiriwa na shughuli za kibinaadamu.
"Hichi
kisiwa kama tutaendelea kukitunza kitaendelea kubakia kutumika kwa shughuli za
kiutalii, tutakapofanya uharibifu tunajiharibia maisha yetu,’’ anaeleza.
Aliwashauri
wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo ndani ya kisiwa hicho, kufanya
kilimo endelevu ambacho kitaimarisha hali ya kisiwa hicho kwa kupanda miti
itakayodumu kwa muda mrefu.
Kisiwa Khamis
(kisiwa ndege) kipo upande wa Mashariki wa bandari ya Tumbe, kikiwa ni moja ya
visiwa vidogo vidogo vinavyomegeka siku hadi siku kutokana na mabadiliko ya
tabia nchi kwa zaidi ya miaka milioni 5 iliyopita.
MWELEKEO WA UTEKELEZAJI BATIKU KUU YA WIZARA 2022/2023
Akiwasilisha hutuba ya bajeti ya wizara ya Utalii na Mambo ya Kale waziri wa wizara hiyo Simai Mohamed Said, alisema kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, wizara imepangiwa jumla ya shilingi zaidi ya shilingi bilioni 17.289.
Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 7.500 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Maeneo ya Kihistoria mfano wa kisiwa Khamis (kisiwa ndege).
MWISHO.
Comments
Post a Comment