UMEWAHI
kuwaza maisha bila kuona, kusikia, kusema au kusimama.
Basi hayo
ndio maisha ya kila siku ya watu, wenye ulemavu, aidha wa viungo, uoni, uziwi
na aina nyengine.
Lakini watu
wenye ulemavu ni sawa na watu wengine, wanahaki zote za msingi, kama ilivyo kwa
wengine.
Miongoni mwa
haki hizo ni kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kama ilivyoelezwa katika
mikataba na sheria mbalimbali.
Mkataba wa
kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu wa 2006, ambao ibara yake ya 27 (f)
inasisitiza ushiriki na ushirikishwaji wao kiuchumi.
“Nchi
wanachama wakuze fursa za watu wenye ulemavu kujiajiri, kuanzisha na kuendesha
shughuli za ujasiamali, vyama vya ushirika na mtu binafsi kuanzisha biashara
zake”, inaeleza sehemu ya mkataba huo.
Sheria ya
watu wenye ulemavu ya Zanzibar nambari 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (e)
inaeleza, watu wenye ulemavu wanastahiki haki zote za msingi za
kibinaadamu sawa nawatu wengine ikiwemo kujitegemea na kujumuishwa katika
shughuli za kijamii.
Katika hili
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua ikifanya juhudi, katika kuwaendeza
watu hao, hasa kupitia vikundi vyao vya ushirika na hata mtu mmoja mmoja.
Ikiwa ni kwa
kuwapatia mikopo na mafunzo ya ujasiriamali, pamoja na kutetea haki zao za
msingi kwa kuitaka jamii iwashirikishe katika fursa ambazo wanaziweza.
Hili
limeonekana kwa wanaushirika wa kikundi cha watu wenye ulemavu wa aina mbali
mbali kilichopo Tibirinzi Chake chake Pemba, kilicho wakusanya wenye ulemavu wa
viungo, wasioona na Alibino.
Ambao kwa
pamoja mwaka 2021, walijikusanya na kufikia idadi ya watu 23 na kujiita “Nguvu
moja”.
Safari yao
ilianza kwa kuwekeza kwenye kilimo cha migomba, ambapo walimiliki shamba yenye
wastani wa migomba 600.
Wahenga
walisema ‘Ng’ombe wa maskini hazai’, wakiwa na maana mtu, asiyenacho anaweza
kutumia nguvu kutafuta na hata akipata alichotafuta hakidumu.
Kwani migomba
yao hiyo, ilikumbwa na changamoto ya kuungua mithili ya iliochomwa moto na
kupelekea kupungua uzalishaji.
Makamu
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Fatma Hafidh Suleiman anasema, hali hiyo iliwapa
wakati mgumu kiuzalishaji na walipowafikia wataalamu wa kilimo waliwashauri,
kuachana na kilimo hicho na badala yake waanzishe kilimo cha Mua, jambo
lililowawia ugumu.
“Tulianza
kwa kikilimo cha migomba tukapanda wastani wa migomba 600, ingawa ikaathiriwa
na joto kali, ikawa kama ilioungua, wataalamu wakatushauri kubadilisha kilimo
chengine, ila ilikuwa ngumu kwetu”, anahadithia.
Hapo ndipo
upepo ulipobadilika, kutoka kwenye kilimo cha migomba na kuanza biashara ya nguo, viatu, haliudi na mikoba ya
kike.
Anaeleza
walianza kwa mtaji wa Shilling 300,000 zilizotokana na uuzwaji wa ndizi, ambayo
ilikuwa ni biashara yao tegemezi, tokea mwanzo.
Baadae
ziliwazalishia hadi 500,000 kila baada ya mauzo, jambo lililowatia moyo na
kuongeza, juhudi zaidi ya upambanaji.
Mjumbe wa
kikundi hicho Zaitun Bakar Shante anasema, juhudi zao, ziliungwa mkono na
serikali kupitia mkopo wa shilling milioni 2, kutoka Wakala wa uwezeshaji
wananchi kiuchumi ‘ZEEA’, zilizo wawezesha kuongeza wingi wa bidhaa na kutanua
soko lao.
“Baada ya
ule mtaji wetu wa shilingi 300,000 tulikuwa tunazalisha wastani wa shilingi
500,000 kila baada ya mauzo, hapo ndipo ‘ZEEA’ wakatushika mkono kwa kutupatia
mkopo wa shilingi million 2,” anaeleza.
Mshika fedha
wao Raya Mohamed Nassor anasema, fedha hizo, walizitumia kwa kuongezea mtaji
wao, ili kukuza biashara yao, kwani ilikuwa ni tegemeo lao kubwa katika
kujiinua.
MAFANIKIO
Katibu
Faidha Said Kassim, anaeleza moja ya mafanikio walioyapata ni kupata fedha za
kujikimu kimaisha, jambo ambalo halikuwepo kabla.
Jingine
anasema wamefanikiwa kupata kushiriki na kushirikishwa katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi.
Anaeleza
walifanikiwa kuongeza mtaji, ambapo wamefika shilling million 1.5,
iliowawezesha kupata wastani wa shilling million 2, kila baada ya mauzo.
Anafahamisha
kati ya hizo hutoa pesa za mtaji, kulipa mkopo ‘ZEEA’, huweka hakiba kwa ajili
ya uendeshaji shughuli za kikundi na nyingine kwa kujikimu.
“Mafanikio
tulioyapata ni kupata fedha za kujikimu kimaisha, kupata kushiriki na
kushirikishwa katika shughuli za kiuchumi na kuongeza mtaji wetu”, anaeleza.
Anasisitiza
mafanikio hayo hayakuja kwa bahati mbaya, bali ni kwa uungwaji mkono wa
serikali na wadau wa kupigania haki za watu wenye ulemavu, kwa kupatiwa mkopo
wa shilling million 2.
Faidha
mwenye ulemavu wa uoni anasema, kutokana na hatua waliopiga, walishapata mlango
wa duka ambao unawawezesha kuuza bidhaa zao kwa utulivu.
CHANGAMOTO WASIOISAHAU HII HAPA
Ghafla mambo
yakabadika baada mtu asie thamini nguvu na juhudi za wengine, kubadilisha mzigo
wenye bidhaa zao za biashara kama nguo, viatu na mikoba na kuacha mzigo wenye
nafaka.
Kwakuwa
wanaushirika hao wote ni wenye ulemavu na huchukua bidhaa zao nje ya kisiwa cha
Pemba, walimchagua mmoja wa wanakikundi, kuwa ni mnunuaji bidhaa hizo.
Ambae ni
Aisha Ali Abdallah na yeye ni mwenye ulemavu wa uoni, hufanya safari ya kwenda
kuchukuwa bidhaa hizo kila pale inapo hitajika.
Aisha
anaeleza siku moja, akiwa katika harakati hizo
mzigo wao wenye bidhaa zenye thamani ya shilling million 1.5 akiwa ndani
ya meli, ulibadilishwa.
Anahadithia
kwakuwa ni mwenye ulemavu wa uoni wakati msaidizi wake, kashamuingizia kwenye
meli anarudi Pemba, alibadilishiwa mzigo wake na kupewa mzigo mwengine wenye
nafaka.
“Siku moja wakati narudi Dar-es-Salam kuchukua
bidhaa za mauzo wakati wa kupakia bidhaa kwenye gari, nilibadilishiwa mzigo, ambapo sikugundua hadi
nilipofika nyumbani, hii ilitokea kwa kutokuwa na uwezo wa kuona,” anahadithia.
Anasema hili
limesababisha kupoteza fedha zao za mtaji na biashara yao kuporomoka na
maendeleo ya kikundi kwa ujumla.
Wanakikundi
hao ambao ni wenye ulemavu kwa pamoja wanaomba wadau mbalimbali, kuwasaidia
kutatua changamoto yao hiyo, kwa kuwapatia mtaji utakao wawezesha kuanza tena
upya biashara yao.
Wanaeleza
kwa sasa, hawana tena pakushika ni kama kibatali walichokitegemea kimezimika,
kwani biashara yao hiyo, iliwasaidia kulipa mkopo uliobakia kuweka pamoja na kujikwamua kiuchumi.
Wanafahamisha
lengo la kuanzisha kikundi hicho, ni kujitengenezea mazingira ya kujipatia
kipato, kujikwamua kiuchumi, ili kuepuka utegemezi.
Wanasisitiza
kitendo hicho kimewarudisha nyuma kimaendeleo, hivyo wanaomba msaada zaidi ili
kuanza upya.
ZEEA
Wakala wa
uwezeshaji wananchi kiuchumi ndio yenye jukumu la kuwawezesha wananchi kiuchumi
kwa kuwapatia mikopo ya kujiendeleza.
Afisa habari
wake Abdi Juma Suleimani anasema, kwa mujibu wa taratibu za ‘ZEEA’ watu wenye
ulemavu wanahaki ya kupatiwa mkopo, kama ilivyo kwa wengine.
Ndio maana
ZEEA kupitia program yake ya 4,4,2 ilishawapatia wajasiriamali wa kikundi hicho
mkopo wa shilingi million 2, kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu
wa hutuba ya bajeti ya wizra ya vijana kazi na uwekezaji kwa mwaka wa fedha
2024/2025 kupitia ‘ZEEA’ shilling 6,616, 166, 637.o3 zimetolewa kwa ajili ya
wajasiriamali, ambapo kati ya hizo shillingi 1699, 288, 637 ni kwa
wajasiriamali 969 wa Pemba.
Huku hutuba
ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2025/2026 ikileza vipo
vikundi 380 ambapo Unguja ni 256 na Pemba 124, vilivyopata mikopo kwa ajili ya kujiendeleza
vikiwemo vya watu wenye ulemavu.
Aidha hutuba
hiyo imeeleza Serikali kupitia ZEEA imetumia Shilling 12, 779, 637, 967,
kuwawezesha wajasiriamali 6,135, ambapo shilling 1,581310, 263 zimetolewa kwa
wajasiriamali wa Pemba pekee.
WADAU WA
WATU WENYE ULEMAVU
Mratibu
Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Pemba Mashavu Juma Mabrouk anasema, bado
kuna changamoto za watu wenye ulemavu kwenye eneo la kiuchumi.
Anahimiza
uungwaji mkono kwa watu hao, katika masuala ya kiuchumi, ili waweze
kujitegemea.
Anasisitiza
elimu ya ujasiriamali pamoja na mikopo yenye masharti nafuu, ni suala muhimu
katika kuhakikisha wanapata fursa za kujiendeleza kiuchumi, kama ilivyo kwa
watu wengine.
Afisa watu
wenye ulemavu Pemba wa “UWZ” Maryam Mohamed Salum anasema, jamii iungemkono juhudi za serikali na watu
wenye ulemavu za kujiendeleza kiuchumi, ili kuondoa utofauti wa kiuchumi
uliopo.
TAMWA-Zanzibar
inasisitiza jamii kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo visivyo vya
kiungwana kwa watu wenye ulemavu, huku wakihimiza kuwaunga mkono katika
mapambano yao ya kichumi.
MWISHO

.jpg)
.jpg)


Comments
Post a Comment