NA NAFDA HINDI, ZANZIBAR
JUMLA ya kazi 529 za waandishi wa habari zimewasilishwa TAMWA kwa ajili ya kuwania tuzo za umahiri za uandishi wa habari za takwimu za wanawake na uongozi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya
habari Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
Zanzibar, (TAMWA – ZNZ), Dkt. Mzuri Issa,amesema miongoni mwa kazi hizo ni
pamoja na vipindi vya redio, televisheni, makala za magazeti na kutoka katika
mitandao ya kijamii zilizoandikwa na kurushwa katika vyombo vya habari kuanzia
mwezi Januari hadi Disemba 31, 2023.
Dk Mzuri amesema lengo la tuzo
hizo ni kuhimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao na vyombo vya habari
kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa masuala ya wanawake katika uongozi na
kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
“Kazi hizo zinaonesha ni jinsi
gani waandishi wamekuza mwamko wa kuandika habari za uongozi kwa wanawake
ambapo zinashajihisha wanawake na vijana wakike kujiamini zaidi na kuwa na
matumaini ya kupata nafasi mbali mbali za uongozi lakini pia zinaielimisha
jamii kuhusu umuhimu wa wanawake katika uongozi,” amesema.
Hii ni mara ya tatu kwa
TAMWA, ZNZ kutoa tunzo hizo hapa Zanzibar na kwa mwaka huu zinatarajiwa
kufanyika mapema mwezi Machi, 2024.
Tuzo za umahiri za uandishi wa
habari za takwimu za wanawake na uongozi zinaandaliwa kwa pamoja na Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, (TAMWA – ZNZ),
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya inayojihusisha
na Mazingira, Usawa wa Kijinsia, na Utetezi Pemba (PEGAO), kwa kushirikiana na
Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Comments
Post a Comment