Na Faki Mjaka-AMM-ZANZIBAR@@@@
Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga Makame amewaomba wananchi wenye Malalamiko na kadhia mbali mbali kuandika malalamiko hayo na kuyawasilisha katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu ili kusaidiwa kupata ufumbuzi.
Amesema katika Afisi yao lipo Faili maalum kwa ajili ya malalamiko ya Mwananchi yeyote ili pale anapoyawasilisha, Afisi iweze kuyafanyia kazi malamiko hayo.
Wakili Hamisa amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Mangapawani Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati Afisi ya Mwanasheria Mkuu ilipoenda kutoa elimu ya masuala mbali mbali ya kisheria kwa wananchi hao ikiwa ni shamra shamra ya wiki ya sheria Zanzibar.
Amefahamisha kuwa, pale Mwananchi atakapoandika malalamiko yake dhidi ya Taasisi yoyote ya kiserikali, Afisi ya Mwanasheria Mkuu huchukua jukumu la kuwaita walalamikiwa kwa lengo la kutafuta suluhu dhidi ya malalamiko hayo.
“Mwananchi anapoandika malalamiko yake, sisi tunampa ushauri wa kitaalam, ikiwa anailalamikia taasisi yoyote ya kiserikali tunachukua jukumu la kuitaarifu taasisi hiyo kwa lengo la kumsaidia mwananchi huyo kupa ufumbuzi” alibainisha Wakili Hamisa.
Mmoja ya wananchi hao Jafar Said Khamis amesema Shehia yao imegubikwa na changamoto nyingi ikiwemo maswala ya udhalilishaji na migogoro ya ardhi hivyo ni vyema Afisi ya mwanasheria Mkuu kuendelea kutoa elimu ili kupambana na changamoto hizo.
“Kwa kweli elimu inahitajika sana. Hapa kuna matatizo mengi, tunaomba kila baada ya miezi mitatu Maafisa muje mutoe elimu na kufanya tathmini ya maendeleo yetu kuliko kuja mara moja kwa mwaka” alishauri Jafar
Kwa upande wake Ali Juma Nuru ameomba kujengwa Kituo cha Polisi kutokana na Shehia yao kuwa kubwa na kutawaliwa na harakati nyingi zinazochochea makosa mbali mbali ikiwemo wizi, udhalilishaji na madawa ya kulevya.
Amesema kituo cha Polisi kipo masafa ya mbali na hata pale inapotokea kufanyika uhalifu, wananchi hushindwa kumpaleka muhalifu kituoni kutokana na kuwa mbali.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Mangapwani Abbas Khamis Maalim ameishukuru Afisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kuamua kuja katika Shehia yake kutoa elimu ya kisheria ambayo imewanufaisha kwa kiasi kikubwa.
Awali, Wakili wa Serikali Mkuu, kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Said Salim Said (Bakhresa) wakati akitoa mada ya udhalilishaji aliwaomba wananchi hao kutoa ushirikiano ikiwemo ushahidi pale zinapopelekwa kesi za udhalilishaji mahkamani.
Aidha Wakili Said aliwashauri wananchi hao kuzijenga familia katika malezi na maadili mema ili watoto weweze kuwa Wachamungu ambao watajiepusha na makosa mbali mbali ikiwemo ya wizi, udhalilishaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Kila ifikapo mwanzoni mwa mwezi Februari ya kila mwaka, Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar huungana na Taasisi nyengine za kisheria kutoa msaada wa kisheria kwa jamii (outreach program) ikiwa ni moja ya maadhimisho ya wiki ya sheria Zanzibar.
Comments
Post a Comment