Skip to main content

DONGO MSANII MWENYE NDOTO ZA KUFIKA MBALI KWENYE FANI YA UIGIZAJI

 





-Asema, changamoto ya kifedha inawarudisha nyuma kwenye kazi zao


NA ZUHURA JUMA, PEMBA 

 

KHAMIS Ali Omar (32), umaarufu ‘dongo’, ni mkaazi wa Kambini Kichokochwe wilaya ya Wete Pemba.

 

Yeye ni msanii wa kizazi kipya mwenye ndoto za kufika mbali kwenye uigizaji wake.

 

Alianza fani hiyo mwaka 2017, wakati huo haikuwa moyoni mwake, wala haikuwa katika malengo yake aliyojiwekwea kwenye maisha.

 

Kipindi hicho alikuwa kwenye kikundi cha mchezo wa sarakasi cha 'Kambini Art Group', hivyo kulikuwa na maonyesho yanayofanyika kila mwezi wa mwisho kabla ya kuingia kwenye funga, kijijini kwao, ambapo walikutana na vikundi mbalimbali ikiwemo vya uigizaji.

 

"Hapa kwetu kila mwaka mwezi wa ‘mrisho’, (siku moja kabla ya ramadhan), kulikuwa kunafanyika onesho 'show', hivyo vikundi mbalimbali vya burudani vilialikwa na kuonyesha vipaji vyetu," anaeleza Dongo.

 

Wakati wapo kwenye sarakasi, mmoja wao alizaa wazo la kutaka kuigiza, ambalo halikupingwa kwenye kikundi chao, wakati huo akiwa ni Katibu wa kikundi hicho.

 

Baadae ya kukubaliana, kwa mara ya kwanza waliigiza mchezo unaoitwa 'Haidar' ambapo yeye ndie aliebeba uhusika mkuu aliekuwa akiitwa 'Haidar'.

 

Walicheza vizuri filamu hiyo, kiasi ambacho kiliwapatia umaarufu kikundi chao hicho na yeye mwenyewe binafsi.

 

Anafafanua, walitoa kazi mbili na ya tatu iliharibika, ambapo aliekuwa akiwatungia maudhui hayo ni mwalimu Mussa Hamad Said, ambae fani yake hasa ni daktari wa binadamu.

 

Walizowea kumwita mwalimu, kutokana na kuwafundisha kwake, hivyo wakampa heshima hiyo kubwa.

 

Dongo anaeleza, waigizaji wengi maarufu na wakongwe walianza kuwatafuta ili kuunganisha nguvu za pamoja, na kuona wanakuwa vizuri katika soko la filamu.

 

Anahadithia kuwa, hata muigizaji maarufu anaejulikana kwa jina la 'Mau Mpemba' alipoona filamu zao hizo, alifika kisiwani Pemba kuwaunga mkono, ambapo walianza kuigiza klipu ya samaki ya vichekesho.

 

"Mau’ baada ya kutuona vijana wa kwao tunaigiza, wakati huo yeye ameshasonga mbele kiuigizaji, aliamua kuja kutuunga mkono, tulifurahia sana hatua hii," anasimulia Dongo.

 


Kwa sasa Mau akiwahitaji katika kazi zake anawaita Unguja kusaidiana, hivyo hawakupitia changamoto kubwa ya kupata umaarufu wala kujijengea jina.

 

Kutokana na vipaji vyao kuwa vizuri na kuivutia jamii, pia walifuatwa na kikundi cha 'Jufe Film' ili waunganishe nguvu za pamoja, zitakazowafikisha mbali katika soko la uigizaji.

 

"Na kweli tumefika mbali kidogo, ingawa sipo tunapopataka, lakini tumesogea mbele, hivyo tunaendelea kupambana ili kutimiza lengo letu," anafafanua.

 

Akiwa kwenye kikundi cha 'Jufe Film', kwa mara ya kwanza Dongo, aliigiza kwenye filamu ya 'Mwizi wa Futari' ambayo ilipata mashabiki wengi na kuendelea kupata umaarufu.

 

Walifanya kazi nyengine ambayo iliharibika na haikutoka, jambo ambalo liliwatia hasara ya zaidi ya shilingi 400,000.

 

"Lakini tulichukulia ni jambo la kawaida, kwani hakuna kazi inayokosa changamoto, kwa sababu kuna baadhi yetu walikata tamaa kabisa," anasema.

 


Anasema, changamoto haikuwa ndogo sana kwa sababu pesa hiyo ilikuwa ni ya wapigaji picha tu, kwani mambo mengine wanafanya wenyewe zaidi kwa kujitolea.

 

Baada ya kuharibika filamu hiyo, waigizaji wengi kwenye kikundi chao cha mwanzo, waliondoka kwenye sanaa, na kubakia yeye, Naomba, Goro na marehemu Bikidecha.

 

Filamu nyengine na clipu walizoigiza ni pamoja na Nyumba moja, Skujua, Wahuni si watu wazuri, Mke wa ngomani, Mume wa mjini, Figo, Marejeo na kwa nini Ramadhani.

 

Kuna mafanikio mengi aliyoyapata katika fani ya uigizaji, ikiwa ni pamoja na kupata heshima na kujuana na watu mbalimbali, hali ambayo inamsaidia kufanya kazi zake kwa urahisi.

 

Pia wanapata mahitaji ya familia ingawa hayakidhi haja, lakini sio kama kukosa moja kwa moja, hivyo anajishugulisha na kazi nyengine ili kujipatia kipato.

 

Kwenye jamii asilimia kubwa ya wananchi inamkubali Dongo, isipokuwa changamoto kidogo ni kwa wasanii wenzao wakike, kwa sababu mwanzo walipata shida sana kwa kuonekana wahuni na wasio na heshima.

 


"Changamoto zinazotukabili ni kutokuungwa mkono (support) kwa sababu zamani tulikuwa tunatoa ‘CD’ lakini kwa sasa hazinunuliwi, lazima tutumie mitandao ya kijamii," anaeleza.

 

Tena jambo hilo inawapa shida kwa sababu ili wapate malipo kidogo wanatakiwa kuwa na ‘subscribe’ nyingi na kutuma kazi zao kila siku, jambo ambalo ni ngumu kwani hawana fedha za kutengeneza.

 

Ukosefu wa vitendea kazi, hivyo wanalazimika kukodi vifaa, hali ambayo inazidi kuwaongezea gharama kila wanapoigiza.

 

"Wadhamini wanajitokeza kiasi, wakati mwengine tukiona kimya sana tunawafuata wao, hali ambayo inasababisha kuwa kama wametununua,’’anasema.

 

Anaomba waungwe mkono kwenye kazi yao, ili wapate soko kama wasanii wenzao wa Bara, kwani hawaumizi vichwa sana kutokana na soko lao ni zuri.

 

Dongo anaiomba serikali iwasaidie kupeleka kazi yao katika chombo cha habari cha jamii (ZBC), kwani juhudi zao ziligonga mwamba walipokwenda kutafuta msaada.

 

"Ikiwa tutaungwa mkono basi itakuwa na sisi tumejiajiri vizuri, kwa sababu tutapata pesa ya mahitaji yetu angalau ya muhimu," anahadithia.

 

Anasema, wameona kwamba, Shirika hilo kwa sasa limeboreshwa na kwa vile filamu zao zinapendwa sana, basi ikiwa zitarushwa hata watazamaji wataongezeka.

 

"Kutengeneza filamu mpaka kumaliza ni gharama kubwa, kwa sababu, lazima tuweka kambi, kula, usafiri, hivyo kwa vile ni wenyewe kwa wenyewe tunabebana tu," anaeleza.

 

Hivyo kwa vile ni wao wenyewe, filamu moja hutumia zisizopungua shilingi milioni saba kwa kujibana.

 

Wakati mwengine inawalazimu watafute wasanii nje ya Zanzibar, hivyo wanatumia gharama kubwa zaidi mpaka kumaliza.

 

Hivi karibuni waliongeza nguvu na wasanii wa Bara, ambapo walitumia mwezi mmoja na hawajamaliza, hivyo walitumia gharama za shilingi milioni nane.

 

"Hiyo ni ya ‘episode’, kwa hiyo tumeiacha uporo kwa sababu hatuna pesa ya kuendeleza, na tulicheza kisiwani Unguja kutokana na kuwa tungewaleta Pemba gharama ingezidi," anaeleza.

 

Waliipeleka kazi yao hiyo kwenye kituo cha AZAM TV ili wapate gharama, angalau nusu kwa ajili ya kwenda kumalizia, ingawa waliambiwa wamalizie kwanza ndipo waipeleke.

 

"Walituambia siku hizi hawapokei tena kazi nusu kwa sababu, baadhi ya vikundi wakishakupewa pesa tu wanakimbia, hivyo wameshaibiwa sana," anasema.

 

Anaeleza kuwa, wanaendelea kutafuta wadhamini ili wamalizie kazi yao, ambapo wangepata pesa ndani ya miezi miwili wangemaliza yote.

 

Na wao pia wamekuwa wakichukuliwa kwenda kuongeza nguvu kwenye filamu za Bara, ambapo hivi karibuni walikwenda Lushoto na walitumia mwezi mmoja kwa episode 20.

 

‘’Tupo tuliosomea fani mbalimbali lakini hatuna ajira rasmi, hivyo kupata fedha ya kuendeleza shughuli zetu za uigizaji ni ngumu sana, tunahitaji msaada," anaeleza.


Mdogo wake Dongo mkaazi wa Kambini, Said Ali Omar (Goro) anamuelezea kaka yake kwenye fani ya uigizaji kwamba, ni kijana anaefanya vizuri ambae anashirikiana na waigizaji wenzake vizuri na hata kwenye jamii.

 


‘’Yeye ni mkarimu sana kwa sababu hata akitafutwa na wanafunzi wa skuli kutaka waigize nae hapingi, bali anashirikiana nao na wanafanya vizuri, hivyo jamii inampenda sana,’’ anaeleza.

 

Anasema kuwa, familia yake wanampa ushirikiano huku wakimnasihi kwamba aendelee kupambana kwani hakuna mafanikio yanayokuja kwa urahisi.

 

‘’Kila jambo mwanzo unakuwa mgumu, hivyo na yeye ipo siku atavuna matunda mazuri, muhimu asirudi nyuma kwa changamoto anazopitia,’ anaeleza.

 

Amina Hamad Ali (Naomba) mkaazi wa Ole ambae ni msanii mwenzake anasema, anamfahamu Dongo kwamba ni mpambanaji na ni msanii asie na shida, hivyo kila mmoja yupo karibu nae.

 

Anasema kuwa, yeye alimkuta katika fani hiyo ya uigizaji kwa sababu aliingia mwazo, ingawa mashirikiano anayoyapata anafarijika sana, kwani yanamjenga kuwa bora kila siku zinaposonga mbele.

 

‘’Dongo namfahamu sana kwa sababu nimekuwa nae kwa muda mrefu sasa kwenye uigizaji, anapambania kazi zake vizuri, hana shida na mtu, na anajitolea sana kwa wenzake,’’ anasema Naomba.

 

Mwenyekiti na Mwanzilishi wa kikundi cha Uigizaji cha ‘Jufe Film’ Pemba, Mohamed Yussuf Hemed anasema, alimjua msanii huyo tangu akiwa bado hajawa maarufu sana kwenye fani ya uigizaji.

 

Anaeleza kwamba, baada ya kumuona kwenye filamu ya Haidar, walimfuata na kuja kusajili rasmi kwenye kikundi chao na kuanza kufanya nae kazi.

 

‘’Kwa kweli Dongo ni mzuri sana kwenye kazi kwa sababu anaipenda sana kazi yake na ukimpangia sini yeyote anacheza bila kusita,’’ anaeleza.

 

Anahadithia kwa, msanii huyo yupo tayari muda wowote kwa kazi, hivyo anapopigiwa simu anakuja haraka na anashirikiana na wenzake kwa kila jambo.

 

‘’Kwa kweli siwezi kuyamaliza kuyataja mazuri yake kwa sababu, sio mvivu na yupo tayari kwa chochote kwenye uzalishaji (production), hata umwambie afanye kazi gani anafanya na kubeba vifaa, hajali kuwa amekuja kwa uigizaji tu,’’ anasema.

 

Msanii huyo ana mke na watoto watatu, ambae alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya Mchangamdogo na kumalizia kidato cha nne katika skuli ya Sekondari Mchangamdogo.

 

Dongo hakuwa nyuma kujiendeleza na elimu ya juu ambapo alisomea fani ya umeme katika chuo cha Elimu Amali Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Pemba.

 

MASHABIKI WA DONGO

 

Asha Khamis Hamad mkaazi wa Wete anasema, yeye anapenda sana filamu anazoigiza Dongo, hasa za vichekesho kwani anapoziangalia hata kama ana msongo wa mawazo, hunaondoka.

 

‘’Kwa kweli kipaji chake ni kizuri, kwa sababu anaigiza kwenye vichekesho na kawaida, hivyo inaoneshea anaweza kuigiza katika hali yeyote ile,’’ anasema.

 

Amina Makame wa Kiuyu Minungwini anamsifia sana Dongo, katika uigizaji wake kwamba, anafurahisha hasa pale anapovaa mavazi ambayo yanachekesha.

 

Bakar Hamad Juma mkaazi wa Kambini anamtaja kuwa ni muigizaji mzuri, anaeweza kufika mbali kwenye sanaa ya filamu, kwani kipaji chake ni cha kiwango cha juu.

 

‘’Tuna kipaji kizuri pale, lakini kinachouwa vipaji vya wasanii Pemba, ni kukosa fedha za kufanyia sanaa yao, maana, ili uwekeze fedha, badi uwe nazo,’’ anasema.  

 

WIZARA INAFANYA NINI KUWASAIDIA WASANII

 

Mratibu wa Baraza la Sanaa Pemba Seif Salim Mussa anasema, kuna fungu maalumu la kuwasaidia wasanii, kwa kuwapatia elimu, vifaa na kuwatafitia fursa mbalimbali ikiwemo wadhamini.

 

‘’Wakifuata taratibu za Baraza ketum kazi zao zinaonekana, kwa sababu ni lazima wawe na leseni, kwani vikundi vya Sanaa, vinatakiwa vitambulike kwa kuwa na usajili pamoja na kuhakiki kazi zao kwetu,’’ anafafanua.

 

Anasema, wanamipango mingi, kuhakikisha wasanii hao wanaweza kujitegemea, hivyo wameandaa ‘ubunifu wa kimkakati’ ambao unategemewa kuzinduliwa mwaka huu.

 

Katika ubunifu huo wa kimkakati, wasanii wanatakiwa kutengeneza muongozo ‘script’ zao, na baada ya kutoka tangazo la wizara, wanatakiwa waipeleke kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

 

Anafafanua, lakini pia walilishajiihisha ‘ZBC’ wachukue kazi za wasanii, angalau zioneshwe kwenye kipindi maalumu cha sanaa, ili kukuza vipaji vyao.

 

‘’Ipo taasisi moja inayohusika na kukuza vipaji Zanzibar, tulizungumza nayo na wakasema kuwa watawasaidia na kuwachukua kwenye mashindano ya sanaa (ZIFF), na tumewaunganisha wasanii,’’anafafanua.

 

                            MWISHO.

 

 





Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

Vikausha damu vya mjamzito hivi hapa, umo mchele, udongo, mkaa, chaki Uwezekano wa kuzaliwa watoto wenye udumavu, utapiamlo ni mkubwa

  NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@ ‘’KILA ninapobeba mimba nimezoea kula mchele kwa wingi naweza kusamehe pilau au biriani,’’ ndio maneno ya mwanzao ya Bahati Mohamed Ali (sio jina lake halisi). Nilimfuma akiwa barazani kwake, mjini Ole wilaya ya Chake chake, pembeni yake akiwa na kibakuli cha mwazi, kwa umbali utaona amejaza chakula aina ya pepe, kumbe ni mchele wa Mbeya. Hujichotea kidogo kidogo na kuushindilia mdomoni mwake, huku akiendela kupiga storia na wenzake, bila ya kujali kuwa ujauzito alionayo na mchele huo hauna mwisho mwema. Kawaida yake akiwa mjamzito, kila anapoamka asubuhi anaroweka mchele upatao robo kilo hivi…na baada ya kumaliza kupika, yeye huchukua mchele wake kutafuna (kula). Wakati mwenza wake na watoto wao, wanakula chakula cha mchana, Bahati yeye hukaa pembeni na kibakuli chake cha mchele akiendelea kubahatisha afya yake. ‘’Mimba nyengine hupenda sana kutafuna mchele wa Mbea na nyengine hupenda mchele wa mapembe, kwa kweli huwa nina hamu (kileo), kwan...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...