UNAPOZUNGUMZIA juhudi za serikali,
katika kuiletea Pemba maendeleo ya kiuchumi, huwezi kuacha uimarishaji miundombinu
ya bandari ya Mkoani Pemba.
Bandari ambayo ni sehemu muhimu katika uchumi wa watu
wa kusini Pemba na kisiwa kizima kwa ujumla.
Kutokana na umuhimu wa bandari hiyo, serikali imekuwa
ikiimarisha kwa kuifanya kuwa ya kisasa zaidi, ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwani kumekuwa na maboresho makubwa, yanayo husisha gati
ya kisasa, ujenzi wa jengo la abiria, njia ya kupitia abiria na kuongezwa kwa eneo
la bandari kavu, kwa kuwekwa eneo maalumu la kutunzia makontena ya mizigo.
Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Pemba Abdalla Salim
Abdalla, anasema bandani ya Mkoani ni ya pili kwa ukubwa visiwani humo, ikipokea
meli kubwa za mizigo kutoka nchi mbalimbali na kukuza uchumi wa kisiwa hicho.
Kwakuona umuhimu wa Bandari hii, serikali imewekeza kiasi
cha Dola za Marekani milioni1, kwa maboresho ya gati pekee.
Ambapo kumbe lengo ni kuziwezesha meli za kisasa za mwendokasim
kuegesha kwa urahisi na usalama, ili kurahisisha safari za boti baina miji ya Unguja,
Pemba na Tanga.
Tena kati ya hizo, zimo meli za abiria, za makontena
pamoja na mizigo kutoka miji ya Mombasa na Uturuki na majahazi kutoka mkoa wa Tanga.
Maana kabla maboresho hayo, uingiaji wa meli na
majahazi ulikuwa mdogo, kwani kwa mwezi hazikufika hata meli 30.
Hii inathibitisha kwamba, maboresho hayo ni mapinduzi
makubwa ya sekta ya bandari, ambayo ni miongo ni mwa sekta muhimu inayo waunganisha
raia kutoka sehemu moja kwenda nyengine.
Kwani wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi,
imesema kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, mamlaka imehudumia abiria 2,108,239.
Amba hao ni wale wanao safiri kupitia bandari za Unguja
na Pemba, kati ya hao 86, 442 kwa Pemba pekee.
Hii inaonyesha umuhimu wa sekta ya bandari katika kurahisisha safari za wananchi wa Unguja
na Pemba na maeneo mengine.
Ali Abudu Mzee ni Mwenyekiti bodi ya Shirika la
bandari, anafahamisha maboresho hayo ya gati hiyo, pia yalienda sambamba na maboresho
ya njia ya kupitia abiria, yenye urefu wa mita 150 na upana wa mita 2.5.
Kwani njia hiyo iliowekwa mabati juu na uzio pembeni,
inalenga kuongeza usalama wa abiria, wakati wanapokwenda kupanda meli ama boti
kwa safari zao mbalimbali.
Wananchi wanaotumia bandari hiyo kusafiria
wanaeleza, kabla ya ukarabati huo, walitembea urefu huo wa mita 150, katika
mazingira magumu ambayo jua na mvua
viliishia mwilini mwao.
“Kabla maboresho haya, tulikuwa tukipata shida sana,
kwani tulitembea masafa katika mazingira yasio rafiki, jua na mvua vilikuwa
lazima kwetu,’’anasema Omar Haji Makame.
Aisha Hassan Hassnuu anasema maboresho mengine yaliofanywa
bandarini hapo, ni ya utanuzi wa njia ya kupitishia vitendea kazi, sasa umewapa
usalama zaidi.
Mwananchi Asha Salim Mohamed anasema bei za bidhaa kama
mchele, sabuni na vyengine zinapungua.
“Kabla maboresho ya bandari ambapo Kontena za mizigo
zilishushiwa Unguja bei za bidhaa zilikuwa juu, wafanyabiashara walililia sana
usafiri lakini kwa miaka miwili hii ni nafuu sana kwetu” anaeleza.
Nae Mwanajuma Hija Said, anaamini kuwa hayo
yaliofanywa na Dk. Mwinyi yanalenga kuimarisha usalama wao, na utoaji huduma
bora.
Kwani kwasasa bandari ya Mkoani ni sehemu muhimu ya
kuiunganisha Pemba na sehemu nyengine, hasa katika uwanja wa kiuchumi.
Aidha maboresho mengine yaliofanyika ni yale ya
utanuzi wa eneo la bandari kavu, inaosimamiwa na kampuni ya Fumba Ports,
inayojumuisha ghala la kuhifadhia kontena.
Eneo hili lenye ukubwa wa mita za mraba 420, limezungushiwa
uzio wenye mfumo wa usalama wa umeme, na lina uwezo wa kuhifadhi makontena 580 kwa
wakati mmoja.
Kazi hii iliyofanywa na serikali ya awamu ya nane, lengo
ni kurahisisha shughuli za upakiaji na upakuaji wa makontena ya mizigo, yanayo kuja
au kupelekwa nje ya nchi.
Oktavian Mbela Kilei ni Msimamizi mkuu wa shughuli
za bandari kavu, kutoka kampuni ya Fumba Ports anasema, hadi Mei 2026 makontena
930 za mizigo, imepokelewa, na kontena 793 zimesafirishwa, kati ya hizo 38 ni zilizojaa
mizigo.
“Toka kuzinduliwa rasmi sehemu hii ya kuhifadhia makontena
mwaka 2024 hadi Mei 2026 tumeshasafirisha, makontena 793 za mizigo na kontena 930
zimepokelewa kutoka nchi mbalimbali”, anaeleza.
Kumbe eneo hilo, ni kwa ajili ya meli kupakuwa mizigo,
kufanyiwa upekuzi, kupakiwa pamoja na uwekaji wa makontena.
Tena akasema michakato yote hayo huhusisha taasisi mbalimbali
za serikali ikiwemo Taasisi ya Viwango Zanzibar ‘ZBS’, Wakala wa Chakula, Dawa
na Vipodozi Zanzibar ‘ZFDA’ na nyenginezo.
Akafafanua kuwa, chakujivunia ni upakuaji mizigo hufanywa
ndani ya siku mbili hadi saba, tofauti na zamani ikichukuwa zaidi ya siku 30 mpaka
kukabidhiwa kwa wenyewe.
Msimamizi huyo kutoka Fumba Ports anaeleza, makontena
hayo mara nyingi huja na bidhaa kama sabuni, Mchele, Mafuta, Nondo na Misumari.
Anafafanua kwa upande wa upakiaji kontena hizo hupakia
bidhaa kama karafuu, mafuta ya karafuu, mwani, kombe na chaza.
Anaeleza malengo ni kuongeza uwelewa kwa wafanyabiashara
wa nchi mbali mbali, ili waweze kuitumia zaidi bandari hiyo.
Anamatumaini kwamba, jambo hilo litawezesha kuongeza
idadi ya makontena yanayoingia na kutoka, kwani lengo ni kufikia tani 10,000 kwa
mwaka.
Mfanyabiasha Suleiman Mohamed Said anaeleza kabla ya
maboresho hayo, walipata usumbufu mkubwa, wanaposafirisha bidhaa zao, kwani walisubiri
muda mrefu.
“Zamani tulikuwa tukiagiza mizigo inachukuwa siku
hadi 30 kuupata, wakati mwengine bidhaa zinaharibika, ingawa sasa siku mbili,
kontena zinapakuliwa kwa kuchelewa siku saba, ni faida kwetu,’’anaeleza.
Stadi Seif Haji ndie Msimamizi kitengo cha Marine
bandari ya Mkoani Pemba anasema, kabla kuwepo kwa mradi wa ’contena Yard’
kisiwani Pemba, mizigo ilipakiwa katika meli za abiria.
Akizitaja kama vile za Azam sealink na Ikram sealine,
kupelekwa Unguja kwa ajili ya kufanyiwa upakiaji na kusafirishwa.
“Kwa sasa huduma za usafirishaji zimeimarika Pemba,
michakato ya upakiaji na usafirishaji hufanyika hapa bandari ya Mkoani na
bidhaa kusafirishwa moja kwa moja, katika nchi ilio kusudiwa sio kama zamani”, anafafanua.
Mbali na manufaa ya kiuchumi, sasa bandari ya Mkoani,
imesaidia kutoa ajira kwa wazawa, kwa asilimia 75 ya wafanyakazi katika eneo
hilo ni wa Pemba wenyewe.
Hii inaonyesha kufanikiwa kwa lengo la serikali ya
kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira zilizopo katika maeneo yao.
Mitandao ya kijamii, inaripoti kuwa, tafiti zinaonyesha
nchi zinazoendelea, zinatazama bandari kama chanzo muhimu cha kipato na maendeleo
ya nchi.
Wakati bandari kubwa ulimwenguni zinapakia na kupakuwa
hadi tani milion 744 za shehena kwa mwaka.
Ilifahamika kuwa, kwa Zanzibar kwenye hutuba ya bajeti
ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar ya 2026/2027, imebainisha kuwa, shehena
za mizigo mchanganyiko 802,584 ziliingia nchini kwa kipindi cha Julai mwaka 2024
hadi Machi jana.
Huku ikifahamika kuwa, shehena 1,452, 665 zikiingia
Zanzibar kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, sawa na ongezeko la
asilimia 81.
Aidha makontena 65,476 yalioingia Zanzibar kwa
kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, huku makontena 73,450 kwa kipindi cha
Julai 2025 hadi Machi 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia12.2.
Vile vile hutuba hiyo inaeleza utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa bandari ya Mkoani umefikia asilimia 73 ya kazi zote, zilizopangwa na
hadi kufikia Machi 2026 na zaidi ya
shilingi bilioni 3.094 zimetumika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Hussein Ali Mwinyi ndie aliezindua meli ya kwanza ya makontena, bandarini
hapo na kuwataka wafanyabiashara, kutumia fursa hiyo.
Septemba 2024 meli ya Lamu Shipping Limited, ilishuhudiwa
na wazanzibari ikishusha kwa mara ya kwanza makontena kwenye Bandari ya Mkoani.
Mbali ya maboresho ya bandari ya Mkoani, pia Pemba kuna
ujenzi wa bandari ya mizigo ya Wesha na bandari ya abiria ya Shumba mjini, itakayo
waunganisha wananchi wa kisiwani humo na nchi jirani ya Kenya.
MWISHO.

Comments
Post a Comment