NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia za Mtemani, Njuguni, Sizini na Mtemani wilaya ya Micheweni, wamesifu ujio wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kupata uwelewa wa mambo kadhaa ya kisheria.
Hayo yameyasema leo Juni 2, 2025 kwenye mikutano tofauti ya wazi, iliyofanyika skuli za Sizini na Wingwi, ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Suluh.
Juma Haji Juma wa Kilindini, alisema sasa amepata ufahamu wa njia za kufuata, ikiwa atabaini cheti chake au cha mtoto wake, kimekosewa herufi.
Nae Aisha Juma Makame wa shehia ya Mtemani, amesema kwa sasa amaelewa njia tano za kuimiliki ardhi, jambo ambalo hapo awali, hakuwa anafahamu.
‘’Ilikuwa sielewi kuwa, hata ukivunja pori baada ya miaka kadhaa, kama hajatokea mwenyewe, ardhi hiyo unaweza kuimboa hati za matumizi,’’alieleza.
Kwa upande wake Asha Makame Haji, amesema alichofaidika yeye, ni kupata ufahamu juu haki na wajibu wa watoto.
‘’Sasa najua kuwa, hata kumpa mtoto jina zuri, kumpeleka masomoni na matibabu ni haki zake kwa mujibu wa sheria,’’alifafanua.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo, Afisa sheria kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu Pemba, Massoud Nassor Mohamed, alisema sheria ni jambo pana, ingawa kupitia kampeni hiyo, inawasaidia wananchi kupata ufahamu japo mdogo.
Afisa Usajili wa Matukio ya Kijamii wilaya ya Micheweni, Almas Massoud Hamad, aliwasisitiza wananchi kutokubali kughilibiwa na baadhi ya watu, wakati wanapotafuta vyeti.
‘’Itumieni ofisi yetu kutafuta vyeti vya kuzaliwa, ama kurekebisha makosa, na msiwatumie watu wa nje maana, madhara yake ni makubwa,’’alifafanua.
Mapema Mkuu wa Idara ya Upimaji na Ramani Pemba, Salim Khamis Haji, aliwakumbusha wananchi, wanapotaka kurithi ardhi zao kupitia serikalini, ili kupata nyaraka halisi.
‘’Unapokwenda Kamisheni ya wakfu kwa ajili ya kurithishwa, faida yake kubwa kwanza ni kupata nyaraka, ambazo ni njia moja wapo ya kujiepusha na migogoro,’’alifafanua.
Akifungua mkutano uliofanyika skuli ya Sizini, Sheha wa hiyo Suleiman Shaame Hamad, aliwapongeza watendaji wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria kwa kuisimamia kampeni hiyo.
‘’Nguvu za utendaji kazi, lazima tuipongeze Idara husika ambayo imesababisha leo, kutufikia katika shehia yangu, na sasa ni wajibu kwa wananchi, kuuliza na kutaka ufafanuzi,’’alifafanua.
Kampeni ya kitaifa na msaada wa kisheria ya Mama Samia Suluhu, kwa upande wa wilaya ya Micheweni itaendelea tena kesho katika skuli, madrassa, vyuo na mikutano ya ana kwa ana na wananchi.
mwisho
Comments
Post a Comment