NA HAJI NASSOR PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia za Msuka mashariki, magharibi, Kifundi, Konde na Kinowe wilaya ya Micheweni, wamekumbushwa kufuatilia haki ya cheti cha kuzaliwa kwa watoto wao, kwani kwa sasa ni jambo la lazima, kwa maisha ya sasa na baadae.
Ushauri huo umetolewa leo Juni 4, 2025 na Afisa Usajili wa Matukio ya kijamii wilayani humo, Alamas Massoud Hamad alipokuwa akizungumza na wananchi hao, kwenye mikutano ya muendelezo wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
Alisema hakuna namna kwa mzazi suala la kufuatilia cheti cha kuzaliwa kwa mtoto wake, kwani ni haki yake ya msingi kama ilivyo haki nyingine.
Alifahamisha kuwa, wajawazito wanapaswa kuhakikisha kwanza wanajifungulia hospitalini, ili iwe rahisi kuandikishwa na kukabidhiwa kipande chenye jina la mtoto husika.
Afisa huyo alieleza kuwa, uandikishwaji huo kisheria unapaswa kufanywa ndani ya siku 42 baada ya mtoto kuzaliwa na ikizidi hapo bado nafasi ipo ingawa tozo lake huongezeka.
"Hapa inaonesha kuna umuhimu mkubwa wa kujifungulia hospitalini, na kwa wale ambao wamebahatika kujifungulia nyumbani, wawaandikishe watoto wao kwa masheha husika,"alifafanua.
Kwa upande wake Inspekta wa Polisi kutoka mkoa wa kusini Pemba, Salehe Makame Ame, amewakumbusha wananchi hao, kuashirikiana na jeshi la Polisi, ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.
Alieleza kuwa sio rahisi kwa vyombo vya sheria pekee kumaliza vitendo hivyo, pasi na wananchi kuongeza ushirikiano wao.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Micheweni Bizume Haji Zume, aliwataka watoto kuwaripoti watu wote wanaowanyemelea kutaka kuwadhalilisha.
Baadhi ya wananchi wa shehia za Msuka Mashariki akiwemo Ali Hassan Faki, alishauri kuwa mikutano kama hiyo iwe endelevu kwa siku nyingine.
Nae Issa Omar alisema wakati umefika sasa, eneo la Konde kuwepo kwa ofisi ndogo kwa ajili ya kupokelea nyaraka mbali mbali, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, ili kupungua masafa ya kwenda Micheweni.
Nae Fatma Hamad Ali alilalamikia mapokezi yasio mazuri katika baadhi ya taasisi za umma, jambo ambalo linaweza kuwarejesha nyumna kufuatilia haki zao.
Ziara za wataalam wa masuala ya sheria kwenye kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, kwa wilaya ya Micheweni itaendelea tena kesho kwa shehia za Makangale na Mkiang'ombe.
Mwisho
|
Comments
Post a Comment