NA HAJI NASSOR, PEMBA::
‘’Kamati yangu inawajumbe tisa, saba ni wanawake sawa na asilimia 77.77
na wawili ni wanaume wakiwa asilimia 22.22, na kazi zangu zinafanikiwa ,’’ndio maneno ya mwanzo ya sheha wa shehia ya Jadida Wete, Juma Ali Juma.
Awali alikuwa na kamati ya wajumbe 12, wanawake wakiwa
wawili na wanaume 10, ingawa kuanzia mwaka 2020, aliivunja kamati hiyo baada ya
kuona maagizo anayoyatoa, hayafanikiwi.
Mwaka 2019, alihudhuria mkutano wa ulioandaliwa na Chama
cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar, Gombani Chake chake,
na kuelezwa kua wanawake wana haki sawa ya kuongoza kama walivyo wanaume.
‘’Mimi dhana hiyo niliijaribu kwenye shehia yangu, na
kweli sasa wanawake ndio ninaowategemea pale ninapotoa maagizo kwa ajili ya
kuwafikishia wananachi,’’anasema.
Anasema, hawajahi kushindwa kwenye shehia yake, kwa kuwa
na idadi kubwa ya wajumbe wanawake, na anafikiria kuwapunguza tena idadi ya
wajumbe wanaume.
‘Wajumbe wanaume wazito kufika kwa muda kwenye
vikao na mikutano, pili fedha wameweka kipaumbele, lakini hata unapowapa kazi, nao huwapa watu
wengine wazifanye, lakini kwa wanawake ni tofauti,’’anasema.
Kumbe sio shehia ya Jadida pekee, ambako masheha
wanaume wanawaamini wajumbe wanawake, hata shehia ya Mtemani ina wajumbe 13,
wanawake ni tisa, sawa asilimia 63.23 na wanaume wanne wakiwa asilimia 30.76.
Sheha wa shehia hiyo Mrisho Juma Mtwana, alisema
sababu ya kuongeza idadi ya wanawake, ni baada ya kuona shehia ya Jadida
inafanikiwa kikazi.
‘’Nilimfuata sheha mwenzangu wa Jadida, nikamuuliza
siri ya mafanikio, kwa mfano kupata watu wengi kwenye mikutano ya jioni,
akaniambia ni kuwapunguza wajumbe wanaume,’’anasema.
Sasa kuanzia mwanzoni mwaka 2021, aliamua kwanza
kupunguza wajumbe kutoka 15 wa zamani, na kuwa na wajumbe 13 na wanawake
kuwaweka tisa (9).
Tokea afanye mabadiliko hayo, kuanzia sasa anafurahia utendaji
wa kazi, na hasa anafurahishwa zaidi, anapokuwa na mikutano ya nyakati ya jioni, jinsi
wajumbe wake wanawake wanavyotumia mbinu ya kukusanya wananchi.
‘’Kama kuna sheha anamatatizo kwenye shehia yake, aangalie
uwezekano wa kuwaweka wajumbe wengi wanawake kwenye kamati, kama hana tatizo
binfsi, anaweza kufanikwa kama nilivyo mimi,’’anasema.
WAJUMBE WA SHEHIA HIZO
Wanasema, kamati ya sheha yenye wajumbe wengi wanaume
imekuwa ikikosa ufanisi, kutokana na kuwaburuza wanawake, hata kwa jambo lililo
wazi.
Asha Mussa Idd na mwenzake Maimuna Ali Khamis wajumbe
wa kamati ya shehia ya Jadida, wanasema licha ya kuwa sheha wao ni mwanamme,
lakini wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
‘’Kwa mfano suala la utoro kwa wanafunzi, tulizungumza
na wanawake wenzetu kwa kutumia maneno yetu, walitifahamu na kwa mwaka 2022 pekee
wanafunzi 13 walirudishwa skuli,’’wanasema.
Lakini hata wajumbe wa kamati ya shehia ya Mtemani
Sauda Issa Haji na Asha Issa Ali, wanasema sheha amekuwa akiwaamini kutokana na
kujituma kwao.
‘’Sisi sheha akitupa kazi huwa hailali, maana tunajiuliza,
kwa nini wameachwa wanaume tena walio na elimu, nafasi hii tukapewa sisi, inabidi
tufanye kazi kwa bidii,’’wanasema.
Lakini mjumbe wa kamati hiyo, Ali Makame Mkubwa
anasema, pamoja na na kuwa idadi ya wajumbe wanawake ni kubwa, lakini inamamtiki
katika utendaji wa kazi zao.
WANANCHI WA SHEHIA HIZO
Khadija Ussi Haji na mwenzake Asiya Sharif Hassan wa
shehia ya Jadida na wenzao wa shehia za Mtemani, Nussra Mohamed Omar na Mtumwa
Ilayas Kombo, walisema kamati zao sasa ziko hai.
‘’Inafurahisha, kwa mfano tunapokuwa na kazi ya usafi wa
shehia, hawa wajumbe wa shehia zetu ambao wengi ni wanawake, huwa ndio wa
mwanzo, sasa na sisi tunahamasika,’’wanasema.
Wanasema kama kuna tasisi mfano Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania -TAMWA Zanzibar ndicho kilichowaelimisha masheha wao, na sasa kuwa na kamati zilizohai, baada ya kuingia
wanawake kwa asilimia kubwa.
‘’Kumbe wanawake wanaweza, sasa lazima kuwa na sheria
hasa iwalazimishe masheha kuwa wajumbe wawe sawa sawa baina ya wanawake na wanaume,
maana faida inaonekana,’’wanashauri.
HALI HALISI YA WILAYA YA WETE KWA WAJUMBE WANAWAKE
Wilaya ya Wete, bado hali hairidhishi sana, maana baina ya wajumbe wote 359 kutoka shehia 36 wilayani humo, wajumbe wanawake 132 sawa
na asilimia 36.76 na wanaume wakiwa ni 227, kwa asilimia 63.23.
Hili linaweza kuchangiwa kwa karibu, na uhaba wa
masheha wanawake wilayan humo, kwani wapo 10 tu sawa na asilimia 27.77 na
wanaume wakiwa 26 sawa na asilimia 72.22.
MASHEHA WANAWAKE WILAYA YA WETE
Sheha wa shehia ya Mtambwe Kaskazini, Shufaa Asaa
Muombwa, alisema anao wajumbe 11, lakini wote ni wanaume.
‘’Mara tatu nimeshateua wajumbe saba wanawake,
lakini wanazuiliwa na waume wao, na wengine hutishwa na wananchi,’’alisema.
Na ndio maana kuanzia mwaka 2021 mwishoni, aliamua kuwa na wajumbe 11, sawa na asilimia 100, kuwa wote ni wanaume, ingawa anasema
anangalia namna na kuwa na wanawake hapo baadae.
‘’Napata shida ninapo wapa maagizo hawa wajumbe wangu,
huwa wazito wazito kuyatekeleza, inabidi wakati mwengine niingie na mimi, lakini kama
wanawake wakiondolewa vikwazo, ntafanikiwa,’’anasema.
Sheha wa shehia Bopwe Ramia Said Rashid, alisema
kamati yake imeshirikisha wajumbe tisa (9), wanawake wakiwa watano sawa na asilimia
55.55 na wanaume ni wanne sawa na asilimia 44.44.
‘’Mimi nna nia ya kupunguza idadi ya wajumbe wanaume na
kuongeza ufanisi, maana zipo shehia kama za Mtemani na Jadida zinakwenda
vizuri,’’alisema sheha.
WANAHARAKATI WALISEMAJE?
Mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto Tatu
Abdalla Mselleh, alisema idadi kuwa ndogo ya wajumbe wanawake kwenye kamati za
masheha, hakun uhusiano na uchache wa masheha wanawake.
‘’Wivu wa kupindukia, masheha kutowaamini wanawake, au
mfumo wa utamaduni unaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa wanawake kutopewa nafasi
hizo au kuzikataa,’’alisema.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema
wapo wanawake hupewa nafasi ya ujumbe wa sheha, lakini kutokana na vikwazo
wanavyowekewa, huzikataa nafasi hizo.
‘’Kwa mfano mwanzoni mwa mwaka 2022 yupo mwanamke
alipewa nafasi ya usheha, lakini kwa vikwazo vya muume aliusamehe, sasa mfano kama huu,
huwakumba hata wajumbe wanawake wa kamati,’’alisema .
Sifuni Ali Haji kutoka Jumuiya mwevuli ya asasi za
kiraia Pemba ‘PACSO’ alisema bado wapo baadhi ya wanaume, wamekuwa wakitumia
vitisho, kwa wanawake na kuogopa kupewa uongozi.
‘’Hata ukija kwenye vyama, ukiweka nia ya kugombea
kama ubunge au uwakilishi, umeanza kujitengenezea adui, hivyo hata huko kwenye
wajumbe wa shehia, wanawake wanasumbuliwa,’’anasema.
Mohamed Hassan Ali, Mwenyekiti wa jumuiya za asasi za
kiraia mkoa wa kaskazini Pemba, alisema bado baadhi ya viongozi wanaume,
hawajawaamini wanawake.
‘’Kwa mfano wilaya ya Wete ina shehia 36, lakini
masheha wanawake ni 10, kwanini hapa isiwe idadi sawa, na Mkuu wa mkoa na katibu
tawala wilaya wote wanawake,’’alihoji.
VIONGOZI WA SERIKALI
Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari, alisema
masheha hawafungiki na idadi ya wajumbe wa shehia, kutokana na ukubwa wa shehia
zao.
‘’Sisi hataka kama watawachagua wanawake wote, hakuna
tatizo muhimu mambo yaende, kama ambayo maagizo yanakuja kila siku, maana
wananchi wanachotaka ni kutekelezewa shida zao,’’anasema.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk
Khatib, anasema kubwa ni kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi na kisha
kuzitendea haki.
Akizungumza kwenye kongamano la kutimiza miaka miwili
lililofanyika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi Wete, Rais wa Zanzibar
Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema mawaziri wanawake wameongoza kwa kufanya
vizuri.
‘’Na kwa siku sijazo nitaongeza idadi yao, katika nafasi
mbali mbali za uongozi iwe mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya na
mkoa,’’anasema.
Dk. Mwinyi kwa sasa, alimteuwa Katibu mkuu kiongozi
mwanake kwa mara ya kwanza, tokea Zanzibar ilipofanya Mapinduzi miaka 59 iliyopita.
KATIBA
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndani ya kifungu cha 21
(1) kimeeleza wazi wazi kwamba, kila mzanzibari anayohaki ya kushiriki katika
shughuli za utawala wa nchi.
Kifugu hicho kikazidi kufafanua kuwa iwe ni moja kwa
moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari, sasa je mbona wanawake
wamekua wakikoseshwa haki hii.
Maana leo hii wanawake wamkuwa waimbaji vigelele gele
wakubwa na kuimba nyimbo mwanana kwenye vyama vyao vya siasa, mbona
wamekuwa wakikwazwa wanapotaka kuchukua fomu na kugombea nafasi za majimboni.
Ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, kwenye Ibara ya 21, nayo imeeleza haki ya kila mtanzania
kushiriki kwenye shughuli za utawala, na pia suala la kuchagua na kuchaguliwa.
Hapa utaona kwamba, wanachama wa vyama vya siasa
wamekuwa wakiwang’ng’ania wanaume kama vile kuna kifungu ndani ya katiba za
vyama vyao au ya nchi inayowalazimisha hivyo.
ATHARI YAKE
Mwanaharakati wa haki za wanaweke, Dina Juma Makota
kutoka Jumuiya ya PEGAO wanaotekeza mradi wa miaka minne wa kuwajengea uwezo
wanawake kuadai haki, zao anasema ni kukosa kujiwakilisha.
Ali Khamis Juma mwenye ulemavu wa viungo, anasema kama
wanawake hawamo kwenye kamati za shehia, shughuli za kimaendeleo, zinaweza
kuzorota kwa kiwango kikubwa.
Sheha wa shehia ya Pembeni Saumu Ali Hamad, anasema wao
hushindwa kuyatekeleza maagizo ya wilayani, kwani baadhi ya maeneo, wanaume
hawafiki kutoa taarifa.
Mjumbe wa kamati ya shehia ya Gando, Hamisa Iddi
Kassim anasema, na masheha wanaweza kushindwa kazi, maana suati yao inaumuhimu
wake kwenye vikao.
Mwanafunzi Hassan Khatib Nassor wa Utaani, anasema
kama shehia inataka iporomoke kiutendaji, isiwashirikishe wanawake kwenye
kamati za shehia.
NINI KIFANYIKE
Masheha wanasema, ili idadi ya wajumbe wanawake
iongezeke kutoka ya sasa 132, kati ya wajumbe 359, elimu inahitajika kwa wenye
mamlaka.
Masheha wanawake, wamesema kama wanaume watawafungulia
minyororo wanawake na kuwaamini, idadi ya wajumbe wakamati za masheha itaongezeka.
Wajumbe wa shehia wanasema kama shehia nyingine
zitajenga utamaduni wa kuzitembelea shehia zilizofanikiwa, idadi ya wajumbe
wanawake itakua.
Mratibu wa TAMWA anasema wanawake waliojengewa uwezo
na kupata nafasi, wazitumie kwa moyo mmoja thabiti nafasi zao, ili kuwatia moyo
na ari, wenye mamlaka ya kuteua.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Katib Yahya, anasema
masheha waamue kuwatea wajumbe wanawake, wale wenye uwezo, ili wengine waige.
mwisho
Comments
Post a Comment