NA HANIFA SALIM, PEMBA::
‘’KIJANA ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 15 hadi miaka 35,’’ndivyo sera na sheria ya vijana Zanzibar inavyofafanua.
Lakini kwa upande
mwengine kijana ametafsiriwa kuwa ni mwanamke au mwanamme yeyote mwenye miaka
katia ya 15 hadi 24, kama sera
ya taifa ya Maendeleo na vijana ya mwaka 1996, na kama ilivyorekebishwa mwaka
2007.
Kijana ni mtu muhimu kwa taifa lolote
ulimwenguni, kwani ndio nguvu kazi ya taifa, ndio taifa la kesho kama wasemavyo
baadhi yao.
Lakini kijana ndio
tumaini la taifa na ndio mtu anayetazamiwa kwa mapana ya nchi, katika kuongoza,
kukuza uchumi na kuzima majaribio ya kihalifu.
Vijana wanakumbana
na changamoto mbali mbali katika maisha yao, na mwisho wa siku taifa
linamchukulia kama mtu aliyeshindwa na asiye na msaada wowote kwa taifa lake.
Lakini katika
umri huo wa ujana, inampasa kijana kujitambua ili aweze kuwa na muonekano
halisi, sio kwa umri tu bali matendo zaidi.
Ni lazima awe na
ushawishi katika masuala muhimu na kwa manufaa ya jamii kwa ujumla, hasa kwa
vijana wenzake, katika kushawishi ndio tunaona nguvu ya kijana na kuanza
kutengeneza taifa imara.
Hata serikalini,
vijana wengi wameaminiwa na kuonesha ushawishi mkubwa, kuwa wana uwezo wa
kufanya kazi kwa kuaminiwa na pale wanapopewa nafasi za uongozi.
Serikali imeahidi kuendelea
kuweka mazingira bora ya kuwawezesha vijana, kuzitumia fursa zinazopatikana
katika sekta ya uchumi wa buluu, kuibua fursa za ajira na kuwainua kiuchumi.
Serikali ya awamu ya nane,
inathamini juhudi mbali mbali zinazofanywa na vijana, hivyo ipo tayari
kuendelea kuwashirikisha katika kuzitumia fursa zitakazosaidia kuwainua
kiuchumi.
IDARA YA
MAENDELEO YA VIJANA
Idara ya maendeleo ya vijana, ni miongoni mwa taasisi za serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, iliyoanzishwa mwaka 1992 kwa lengo la kuratibu na kusimamia maendeleo
ya vijana Zanzibar.
Idara hii inatekeleza kazi zake kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya
vijana Zanzibar, mipango na miongozo ya Serikali.
Dhamira yake ni kukuza ustawi na maendeleo ya vijana, kuwajengea
mazingira mazuri na endelevu yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika
sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mkurugenzi wa
Idara hiyo Zanzibar Shaibu Ibrahim Mohamed anasema, juhudi mbali mbali
zinachukuliwa na serikali kuhakikisha shughuli za vijana vinatekelezwa.
Kupitia Idara
yao, imekua ikifanya vikao vya pamoja na wadau wa maendeleo ya vijana, kwa kila
robo ya tatu kuwasilisha taarifa na mpango wa utekelezaji juu ya masuala
yanayowahusu vijana.
"Vikao hivyo
pia tunapata kujua changamoto na tunapashana habari mpya, zilizopo katika sekta
ya vijana, kwani kuna miradi mingi ambayo inaibuka siku hadi siku,’’anasema.
Akitaja malengo ya Idara hiyo moja wapo ni
kuandaa, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango ya maendeleo nchini.
Jengine ni kuimarisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika
nyanja za kiuchumi na kijamii, ili wawe mfano bora wa taifa lao.
Kuratibu taasisi na asasi za maendeleo ya vijana Zanzibar, kusimamia
mipango ya malezi na makuzi ya vijana na kuimarisha ushirikiano, baina ya
taasisi za vijana ndani na nje ya nchi.
‘’Jengine ni kuhakikisha masuala ya vijana yanazingatiwa na kuingizwa
katika sera, mipango, miradi ya kitaifa, na kusimamia mipango ya uwezeshaji wa
vijana kiuchumi,’’anafafanua.
OFISI YA RAIS KAZI, UCHUMI NA UWEKEZAJI
Mratibu wa Idara
ya Ajira Pemba Said Salum Othman anasema, idara yao, inatekeleza mipango
maalumu ya kuhakikisha vijana wanawapatia mafunzo ya ujuzi.
“Mafunzo haya ni
ya miezi sita kwa vijana wa rika tofauti kuanzia miaka 15 hadi 24 kwa wenye
elimu ya msingi, sekondari na ambao hawana elimu kabisa, ili kuhakikisha vijana
wanapatiwa fursa na kuweza kujiajiri na kuajirika,” anasema.
Mafunzo hayo ya
ujuzi yanatolewa, na mwaka jana wilaya ya Wete walichukuliwa vijana wawili,
Chake watatu, Mkoani wawili na Micheweni wawili kupelekwa Unguja kwa ajili ya kusoma
utalii.
“Mwezi Novemba mwaka
2021, tulichukua vijana wa wilaya ya Wete, tunawaangalia ambao wanafaa kwa
mchujo maalumu badala yake, tunawapeleka katika vyuo maalumu vya mafunzo ya
ujuzi wa kujiajiri au kuajirika,” anasema.
Mwaka huu mwezi Machi
walichukuliwa vijana wengine kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya kutengeneza
mafriji, viyoyozi, ushoni pamoja na uchongaji.
Ambapo walichukuw
avijana 28 sawa na kila wilaya vijana saba kati ya Wilaya nne zilizopo Pemba,
wenye jinsia tofauti na uwezo usiolingana.
Hivyo sasa
inafahamika kuwa, vijana 339 wa wilaya ya Chake chake, wamenufaika wakiwemo
wanawake 14 na wanaume 325 na ajira kupitia kampuni za ujenzi wa miradi saba ya
ahuweni wa COVID 19.
Mkoani jumla ya
vijana 117 wakiwemo wanaume 72 na wanawake 45, huku Wete ikiwa na vijana 158
wanaume 141 na wanawake 17 na Micheweni vijana 772 wanaume 688 na wanawake 84
kupitia miradi hiyo.
Afisa TEHAMA
kutoka mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Pemba, Farid Hamuni Juma, anasema
serikali ya awamu ya nane, imetenga zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa ajili ya
kuwawezesha wajasiriamali.
Ambapo tayari kwa
kisiwa cha Pemba pekee, zimeshatolewa zaidi ya bilioni 2 kwa vikundi 228.
“Kati ya bilioni
2 hizo, wilaya ya Chake kuna vikundi 58 vimepatiwa zaidi ya shilingi milioni
500 na wilaya ya Mkoani vikundi 94, vyenyewe vimepatiwa zaidi ya shilingi
milioni 700,’’anaeleza.
Lakini hata
wilaya ya Wete nako kuna vikundi 38, vimeshapatiwa zaidi ya shilingi milioni
300 na wilaya ya Micheweni ina vikundi 38 vilivopatiwa zaidi ya shilingi
milioni 400.
Anasema, kati ya
bilioni hizo 80 kuna mgawanyiko ambao umewekwa asilimia 45 ni vijana, asilimia 35
ni wanawake, asilimia 12 watu wenye mahitaji maalumu, huku asilimu 5 wakiwa ni wastaafu
na asilimia 3 watu ambao wameachana na dawa ya kulevya.
WIZARA YA UCHUMI WA BULUU NA UVUVI
Ali Rashid Hamad,
kutoka ziara hiyo Pemba anasema, jamii bado uwelewa wa jamii kuhusu masuala ya
uchumi wa buluu uko chini, hivyo wameona
kuna haja ya kutoa elimu ili wafahamu.
“Tumetoa elimu
hii ya uchumi wa buluu katika shehia 25 za Pemba na ndani yake asilimia 48 ya
tuliowafikia ni vijana, tumetoa mafunzo ya kusarifu wa mwani kati ya hao vijana
walikua 26 na kutoa vifaa vya uvuvi ambapo wanufaika walikua 16 kati ya hao
asilimia 60 ni vijana,” anaeleza.
Wizara ilitoa
mafunzo ya ufugaji wa majongoo bahari, ambapo waliwafikia watu 80 asilimia 50
kati ya hao walikua ni vijana na baada ya kuwapa mafunzo waliwajengea vizimba
vitano vya kufugia.
“Lazima
tuwajengee mabanda maalumu kwa kushirikiana na watu wa ‘FIO’ tayari
wameshatenga zaidi ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya banda la kukaushia
mwani kwa wakulima wetu wakiwemo vijana,” anasema.
Anasema, sasa hivi
kuna zaidi ya shilingi bilioni 49 ambazo zimepangwa kutolewa kwa kukopeshwa
wanufaika wakiwemo wavuvi, wafugaji wa mazao ya baharini, wakulima wa mwani wakiwemo
vijana.
IDARA YA KILIMO
Afisa Kilimo
Wilaya ya Chake chake Rashid Mohamed Wema, anasema idara hiyo inafanya kazi kwa
kushirikiana na shirika la kilimo ulimwenguni ‘FAO’.
Ambalo
limewawezesha vijana 23 wa vikundi viwili vya ushika kwa wilaya ya Wete na
Mkoani.
“Katika mradi wa ‘CFP’
ambao mabwana shamba wetu wameshirikiana kwenye kilimo cha mboga mboga na
matunda kwa Wete vijana 184 wamewezeshwa kupitia vikundi 12.
Wilaya ya Chake
vijana 195 wamewezeshwa kupitia mradi huo kwa kupatiwa taaluma pembejeo, mbegu
na mbolea, Mkoani vijana 133 wamewezeshwa kupitia vikundi 13 na Micheweni
vijana 21.
WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE
Afisa Utalii na Mambo
ya Kale Pemba, Hafidh Omar Masoud anasema, wizara yao inapitia hatua mbali
mbali katika kuwawezesha vijana.
Kwa mwaka huu wa
fedha, wizara imekua ikitoa elimu bure kwa vijana ambayo inahusisha madarasa ya
vijana yanayohusiana na utalii na lugha za kigeni.
“Tunatoa elimu
hii kupitia mikoa yote miwili ya Pemba kwa upande wa kusini tuna wanafunzi 35
wakiwemo wanawake 10 na wanaume 20 na kaskazini ni wanafunzi zaidi ya 50 wa
darasa la elimu ya kigeni,” anasema.
Anasema, katika
fursa zilizopo nyingi kwa vijana ni za kiutalii ndani ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar za kuajiriwa na kujiajiri wenyewe ikiwemo kuongoza wageni au kuwa mwalimu wa lugha.
MAMLAKA YA MAFUNZO YA AMALI
Mwalimu Mkuu wa
chuo cha mafunzo ya amali Vitongoji Juma Mussa Ali anasema kwa mwaka 2020,
jumla ya wanafunzi 580 walipatiwa mafunzo ya ufundi, kupitia fani za uchongaji,
ushoni na uchomaji wa mageti ‘uashi’.
Mwaka 2021/2022
walipata vijana 400 wa kike, ambao walijiunga na masuala ya upandaji na usarifu
wa mwani, ambao walijitolea kuitumia fursa ya kilimo hicho.
Anasema, katika lengo la kuwaendeleza vijana
mamlaka imeandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana watakaotoa huduma za
kiufundi kwenye hoteli na sehemu nyengine za nje ya nchi kupitia fani ya umeme,
mafriji, viyoyozi na mafundi bomba.
BARAZA LA VIJANA
Fahim Abdalla ni
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wilaya ya Chake chake, amepongeza kwa jitihada
zake za kuwaunga mkono vijana, kupitia nyanja mbali mbali.
Anaona kazi iliyoko
mbele yao sasa kwa vijana ni kukaza buti, ili fedha na miradi iliyopo kwa ajili
yao ifikie lengo la kujiongezea kipato.
MWISHO.
Comments
Post a Comment