HABIBA
ZARALI, PEMBA:
KILA
mwanzoni mwa wiki ya mwezi wa Agosti, ya kila mwaka, dunia huwa na wiki ya
unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Lengo la wiki hii, huwa ni kusisitiza umuhimu wa
maziwa ya mama kwa watoto wachanga na wadogo, kiafya.
Afya ni kitu muhimu katika maisha ya mwanadamu na
kinyume chake, ni kuzalisha maradhi kadhaa yanayodhoofisha mwili na kiakili.
Katika kuhakikisha afya ya mwanadamu inaimarika,
msingi wake huanzia tokea mtoto anapokuwa tumboni na mara anapozaliwa, kwa
kuhakikisha anapewa mahitaji ya msingi ikiwemo maziwa ya mama.
Maziwa ya mama yana kinga kamili ikiwemo ya
vitameni A vya kutosha ambavyo huwa ni kinga ya maradhi mbalimbali kwa mtoto
mchanga.
Ingawa wapo baadhi ya akina mama hawapendi
kunyonyesha na huamuwa kumuachisha ziwa mtoto mara tu, anapojifunguwa, kwa
sababu tofauti ikiwemo kuhofia maziwa yake kuanguka, kupoteza haiba na
muonekano wake.
Katika hatuwa ya kumlisha mtoto chini ya miezi
sita kunaweza kumsababishia michubuko ndani ya utumbo na kupata gesi kutokana
na kuwa utumbo wake hauhimili kusaga vyakula hivyo.
Kunyonyesha ni njia moja wapo muafaka ya
uwekezaji muhimu na ya gharama nafuu inayoweza kufanywa na mtu yoyote mwenye
uwezo wa aina yoyote hata akiwa mlemavu ama masikini.
Taifa lolote linahitaji watu wenye afya na wenye
uwezo wa kiakili na kimwili katika kuleta maendeleo katika nyanja zote za
kiuchumi,kijamii na hata kisiasa.
Moja kati ya njia muhimu ya kupata Taifa bora ni
kupata msingi wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto wachanga.
WATAALAMU
WA AFYA WANASEMAJE?
Muuguzi wa mama na mtoto wa Hospitali ya Abdalla
Mzee Mkoani Pemba, Rabia Mohamed Ussi, anasema kushindwa kuwekeza katika
unyonyeshaji, kunachangia kuongeza magonjwa mengi yanayowakumba watoto.
Anaainisha kuwa, thari za kutonyonyesha watoto
maziwa ya mama hasa kwa watoto moja ni kudumaa akili, kupunguwa kiwango cha
ufahamu wa kujifunza na kutambua mambo mbalimbali ambapo huwapunguzia fursa ya
kiwango cha kupata elimu.
“Viwango duni vya unyonyeshaji humsababishia mama
kubeba mimba za papo kwa papo, ambapo hukosa afya mama huyo na kupunguza
kufanya kazi za kujikimu kimaisha,’’ anasema.
Daktari kutoka Wodi ya wazazi katika hospitali hiyo,
Fatma Said Mohamed, anasema unyonyeshaji unampa mtoto mwanzo mzuri wa maisha,
huku maziwa ya mama yakiwa mithili ya chanjo ya kwanza kwa mtoto wake.
Msimamizi wa kitengo cha lishe Wilaya ya Chake
Chake, Harusi Masoud Ali, anasema kufuata utaratibu wa kunyonyesha kwa akina
mama, kunawalinda watoto wachanga na maradhi kama vile maradhi ya saratani, pumu
na kuharisha.
‘’Maradhi haya kwa watoto ni mepesi kupoteza
maisha ya watoto hao, maana huwa hawana kinga ya aina yoyote,’’anafafanua.
Dokta, Munira Suleiman Khalifa, kutoka kitengo
cha lishe Chake chake anasema maziwa ya mama ni rahisi kupatikana, na wanaoamua
kuwapa maziwa ya kununua hukumbana na gharama kubwa.
WHO
Shirika la Afya Duniani ‘WHO’ linasema mtoto
mchanga ana umri wa tangu pale anapozaliwa mpaka anapotimiza mwaka mmoja,
wakati mtoto mdogo ni yule wa umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka miwili.
Kwa hiyo, unyonyeshaji maziwa ya mama unaweza
kuelezewa kwa ujumla kuwa ni njia asilia ya uzalishaji watoto wachanga na
wadogo ambao pamoja na kula maziwa hayo mtoto anapata virutubishi vingi vya
kinga ya mwili.
Vilevile kitendo cha Unyonyeshaji ni muhimu kwani
huimarisha uhusiano baina ya mama na mtoto na kumjengea mama na mwanawe
kujiamini zaidi.
MTOTO
ANATAKIWA ANYONYESHWE VIPI
Mratibu wa lishe Wilaya ya Mkoani, Mwajine Khamis
Mjaka, anasema ili mtoto aweze kufaidika na maziwa ya mama anatakiwa
kunyonyeshwa ipasavyo kila anapohitaji mtoto na sio anapohitaji mama.
Anasema mama anaponyonyesha anatakiwa kumuweka
mtoto wake vizuri kichwa kiwe juu ya mkono wa mama, tumbo la mtoto ligusane na
tumbo la mama.
‘’Nyato ya ziwa yenye rangi nyeusi ikae katika
mdomo wa mtoto, na mama aliteke vizuri ziwa lake na kuacha tabia ya kulikamata
ziwa hilo kwa kubana vidole kama mkasi,’’anafafanua.
Anasema mtoto anahitaji kupata maziwa ya mama
hata kama yuko kazini, mama huyo anapaswa kuyakamuwa maziwa yanayomtosha kwa
muda wote hadi atakaporudi.
“Wazazi wana kawaida ya kuwaacha watoto wao bila
ya kunyonya kwa muda mrefu na kumpa vyakula vyengine wakati uwezo wa kuyakamuwa
maziwa na akapewa upo hata kama mama hayupo,”anasema.
Mama yanapokamuliwa yana uwezo wa kukaa kwa saa
nane, ama yanaweza kuhifadhiwa katika friji kwa saa 24 na iwapo yatagandishwa
yanakaa hadi saa 72.
“Unapoyayeyusha maziwa ya mama yaliyoganda kwa kuyaweka
katika friji unatakiwa kuyatia katika chombo kisha kukitia katika maji ya moto
chombo hicho hadi yapate umoto unaohitajika na sio kuyateleka maziwa hayo,”alifahamisha.
UMUHIMU
WA MAZIWA YA MAMA
Mratibu wa mama na mtoto wilaya ya Mkoani Moza
Mohamed Ali anasema, licha ya maziwa ya mama kuonekana ni mepesi lakini yana
virutubisho muhimu na kiasi kikubwa cha maji ya kutosha.
‘’Maji ni kwa ajili ya kukata kiu ya mtoto,
chakula na mafuta ambapo kitaalamu inashauriwa watoto wasipewe maji wala
chakula chochote mpaka baada ya miezi sita,’’anasema.
Maziwa ya mwanzo yenye rangi ya njano, yanayotoka
kwa siku tatu baada ya kujifungua ni muhimu na lishe bora kwa watoto, kwani
yanakinga mwili kwa mtoto (immunity).
FAIDA ZA UNYONYESHAJI
Moja ni kuimarisha uhusiano baina ya mama na
mtoto, kuwaondolea watoto maradhi mbalimbali, kuzidisha ufahamu pamoja na
kuwasababisha kujiamini.
Watoto wanaonyonyeshwa kwa kipindi cha miezi sita
ya mwanzo bila ya kupewa maji hupata madini chuma ya kutosha na kukingwa na upungufu
wa wekundu wa damu kwa kipindi chote cha miezi sita.
Mama anaponyonyesha mara kwa mara usiku na mchana
mwili wake hutengeneze maziwa kwa wingi zaidi, kwani kadiri mama
anavyonyonyesha anaongeza uwezo wa kuzalisha maziwa mengi.
Mkuu wa kitengo cha lishe cha wizara ya afya
Pemba Raya Mkoko Hassan, anasema elimu duni ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama,
inachangia ongezeko la ugonjwa wa utapiamlo kwa watoto.
Kwa Zanzibar kati ya watoto 100 ni watoto
30 pekee, ndio wanaonyonyeshwa kikamilifu bila ya kupewa aina yoyote ya chakula,
70 sio rasmi.
“Ni muhimu kunyonyesha mtoto titi moja kati ya
dakika 20 hadi 30 kwa wakati mmoja, ili amalize maziwa yote kabla ya kumpa
jengine, hii itamuwezesha kushiba na kulala muda mrefu,”anasema.
JAMII
INASEMAJE
Maryam Nassor (70) wa Mkoani, anasema enzi zake
wakati akizaa utaalamu huo wa kunyonyesha mtoto miezi sita bila ya kumpa hata
maji, haukuwepo.
Anaona kwa vile wataalamu wa afya wanalihimiza
hilo, basi hakuna shaka ni jambo zuri kwa afya ya watoto na ni jema kwa wazazi
kuufuata utaratibu huo.
“Zamani maradhi kwa watoto yalikuwa mengi na vifo
vilikuwa vikitokea mara kwa mara, inawezekana ilikuwa inatokana tatizo la
kulishwa mapema,”anaeleza.
Sabiha Juma (45) wa Kiwani anasema, kati ya
watoto wake watano, ni wawili wa mwisho ndio aliowanyonyesha miezi sita bila ya kuwapa hata maji, ingawa tofauti
anaiona ikiwemo kwenye ufahamu wa kusoma.
Salma Suleiman (27) wa Uweleni anasema elimu ya unyonyeshaji anaipata
kupitia klinik ya mama na mtoto na kushauri akina mama kufuata maelekezo ya
wataalamu wa afya.
Suleiman Hamad (65) wa Mtambile anasema kila zama
zinazokuja zina utaalamu ulioboreka zaidi ya uliopita ,ni wajibu wa jamii
kusikiliza na kufanyia kazi ili mafanikio kuatikana.
Juma Saidi wa Makombeni anasema ni wajibu wa kina
baba kutowa huduma stahiki ikiwemo ya kula kwa akina mama ili waweze
kunyonyesha watoto miezi sita bila kupewa chakula.
TATHMINI
UNICEF/WHO
Tathmini iliyotolewa mwaka 2017 kwa ushirikiano
wa UNICEF, Shirika la Afya Duniani (WHO) na mradi wa kimataifa wa unyonyeshaji
inaonyesha kuwa, hakuna nchi inayokidhi kikamilifu viwango vya unyonyeshaji
vilivokuwa vimependekezwa.
Viwango vya unyonyeshaji vilivyofanyiwa tathmini
katika nchi 194, vimebaini kwamba asilimia 40 tu ya watoto walio chini ya umri
wa miezi sita, wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kitu kingine na nchi 23
pekee duniani, ndizo zenye kiwango cha unyonyeshaji pekee wa zaidi ya asilimia
60.
Aidha tathmini imebaini kuwa, uwekezaji wa dola
4.70 kwa kila mtoto mchanga unahitajika ili kuongeza kiwango cha unyonyeshaji
pekee kwa watoto walio chini ya miezi sita ili kufikia asilimia 50 ifikapo
2025.
Vifo vingi vya watoto wadogo huchangiwa kwa
kutokupata kunyonya maziwa ya mama ipasavyo jambo ambalo husababisha kukosa
kinga mwilini ikiwemo vitamin ‘A’ ambavyo ni kinga ya maradhi kwa mtoto.
Imebainika kuwa katika nchi tano kati ya hizo ni
za mataifa makubwa kiuchumi, lakini ni yenye dharura kama vile China, India, Indonesia
,Mexico, Nigeria kadiri ya watoto 236,000 hufariki kwa mwaka.
Kwa mujibu wa UNICEF na WHO “Tathimini inaonyesha
kwamba ongezeko la kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee linaweza
kuokoa maisha ya watoto 820,000 kila mwakana na hivyo kuzalisha pato zaidi la
dola bilioni 302.”
Mwisho
Comments
Post a Comment