NA
MARYAM SALUM, PEMBA:::
WALIOSEMA
‘umoja ni nguvu utengano ni udhaifu’ wala hawakukosea.
Waliaamini kuwa, watu wanapofanyakazi kwa pamoja,
maendeleo na ushindi kwa kweli hupatikana.
Sheria namba 15 ya mwaka 2018 iliundwa kwa ajili ya kuipa
nguvu sekta ya ushirika, ili iweze
kuimarika zaidi kwa nia ya kuwafanya
wananchi wapate ajira na kipato.
HISTORIA YA VYAMA VYA USHIRIKA
Sekta ya ushirika iliasisiwa hapa Zanzibar tokea miaka ya
1923 hadi mwaka 1925, ingawaje haikupewa kipaumbele kikubwa kwa wakati huo,
kutokana na ukosefu wa sera makini.
Ambapo kwa wakati huo, jamii haikuwa ikiona manufaa kwa
kuwepo kwa sekta hiyo, hali iliyotajwa kupana foleni ya ajira kubwa serikalini.
HALI YA SASA
Miaka ya hivi karibuni sekta hiyo, imepewa mkazo mkubwa
na kujengewa mazingira na kuundiwa sera madhubuti baada ya kuonekana ni fursa
mzuri kwa wananchi kuweza kupata pahala pa kujiajiri bila ya kusubiri ajira
kutoka serikalini.
Sera hiyo ilikusudia kuviimarisha vyama hivyo, ili viweze
kuwa na uwezo wa kuhimili ushindani wa kibiashara, kuongeza akiba na uwekezaji
na kuinuwa hali za maisha ya wanaushirika kiuchumi na kijamii.
Malengo ya sera ya ushirika mi kujenga vyama vya ushirika
vilivyohuru, imara, endelevu, vinavyoendeshwa kwa uwazi, vinavyoendana na
mahitaji yaliopo.
Ikitajwa vyama hivyo kuwa, vinaweza kuchangia katika
kutoa fursa za ajira, kupunguza umaskini na maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa
ujumla.
Sekta ya ushirika Zanzibar inaendelea kuimarika kwa
viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuipa msukumo mkubwa ikiwemo nyenzo
na vitendea kazi kwa wanachama ili kuona wanakuza vipato vyao kupitia sekta
hiyo.
Kutokana na umuhimu huo Serikali iliandaa sera ya
maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2014, ambayo imeweka dira, dhamira pamoja na
mikakati ya kutekeleza ili kuweza kuimarika zaidi sekta hiyo ya ushirika.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kusimamia
misingi ya kanuni za kimataifa zinazoongoza masuala ya ushirika, kwa
kuhakikisha inafuata fuata misingi na kanuni za ushirika zilizotolewa na
Shirika la kimataifa la vyama vya Ushirika (ICA-1937) na mapendekezo ya ‘ILO’
namba 193 ya mwaka 2002.
Kwa kuonekana kuwa sekta ya ushirika ni muhimu kwa
maendeleo ya taifa na hata kuinuwa kipato ilani ya Chama cha Mapinduzi ya
uchaguzi uliopita wa 2015/2020 ibara ya 85 hadi 87 iliagiza kumarishwa kwa
vyama vya ushirika kama ni taasisi muhimu .
Kutokana na hilo hadi sasa vyama vya ushirika vimekuwa ni
tegemeo kubwa kwa wananchi waliojiunga katika umoja huo na vimekuwa
vikiongezeka siku hadi siku.
Akizungumza na makala hii Msaidizi wa Idara ya vyama vya
ushirika Pemba Yussuf Saleh, anasema vyama 4,418 vimeanzishwa na kusajiliwa
ambavyo vina wanachama wa mchanganyiko wakiwemo wanawake na wanaume ingawaje
karibu asilimia 90 ni wanawake.
Vyama hivyo vinamtaji wa shilingi milioni 269.602 na
vimefanyiwa ukaguzi na mamlaka husika vinaaminika kwamba vinafanya kazi zake
kwa mujibu wa sheria za vyama hivyo.
Anasema vile sekta hiyo imekuwa ni moja ya kitu
kinachotoa ajira kwa wananchi, ambao ni wanachama wa vikundi hivyo vimetowa
ajira kwa wananchi 10,423wakiwemo wanawake 5,442 na wanaume 4,981.
Yussuf anaeleza kuwa kuimarika kwa vyama vya ushirika
kunategemea sana, kiwango cha huduma za kitaalamu zinazotolewa kwenye vyama
husika ikiwemo.
Moja ya eneo hilo ni usajili, kuvipatia ushauri wa
kitaalamu, kuvisaidia katika utatuzi wa migogoro pamoja na kusimamia masuala ya
utawala bora na ubadhirifu wa mali na fedha za vyama vya husika.
“Hili kama la ubadhirifu wa mali na fedha za vyama vya
ushirika kama halikusimamiwa vyema, kunapeplekea kufa na tumekuwa tukiwasikia
wenzetu kukumbwa na kashfa kama hizi”, alisema.
VYAMA
VYA USHIRIKA
Katibu wa kikundi cha ushirika cha ufugaji wa samaki cha
Maambani Chambani wilaya ya Mkoani, Maalim Nassor ‘Buda’ anasema kwanza
kujiunga katika kikundi cha ushirika kunatoa fursa ya kujenga umoja wa ndani na
nje.
Anaeleza kuwa kuanzishwa vikundi vya ushirika kunakuwa na
mafanikio mbali mbali ikiwemo kupata mikopo, mafunzo ya kibiashara, kuongeza
udugu na uzalishaji mkubwa wa bidhaa.
“Nawaomba wale ambao hadi sasa hawajaamua kujiunga na
vikundi kama hivi, basi waanzishe na wajiunge kwa wingi kwani sasa kunafursa
nyingi ambazo Serikali imeziweka kwa wale ambao wamejiunga na vikundi vya
ushirika,’’anasema.
Nae Katibu wa kikundi cha ushirika wa ‘Kichakaa sishangi’ unaojihusisha na
utengenezaji wa Chumvi na ufugaji wa Samaki, Shehe Bakar anasema uwepo wa
ushashirika umekuwa mkombozi mkubwa kwao.
‘’Kwa hakika hata kama ni kiasi kidogo, lakini ushirika
wetu umezaa ajira kwa wanachama, na hman hamna, lakini rizki inapatikana ya
kuendeshea maisha,’’anasema.
Anasema kama mwanachama anakuwa mjanja wa kutafuta,
kupitia vyama vya ushirika anaweza kujiendeleza na kuanzisha shughuli nyingine
mbadala ambayo atajiingiza kipato.
Hata ndani ya ushirika wao, wapo wanachama toa
wamefanikiwa kusomesha watoto hadi vyuo vikuu, kutibu wanafamilia na kujenga
nyumba za thamani, jambo ambalo halipo kwa wale ambao hadi sasa hawajaamuwa
kujiunga.
“Hii fursa ambayo ipo kwa wanaushirika, tuitumieni kwani
inafaida kubwa kwetu, sasa hivi tunapatiwa mikopo mbali mbali kwa wale ambao
tumejiunga,’’anaeleza.
Kwa upande wake Mwanakhamis Ali Haji mwanaushirika wa
kikundi cha ‘Tumpendane’ Wingwi
anasema vikundi vya ushirika, vimefanikiwa kuwatoa katika utegemezi kutoka kwa
watu wengine, kwani wanakuwa wakipata fedha za mahitaji yao mengi.
“Ilikuwa ninapokumbana na changamoto za kifamilia au
zangu binafisi, nilikuwa na hofu wapi nitapata pesa ya kujikwamuwa, lakini sasa
namshinda mfanyakazi serikalini, wakati wowote napiga hodi kikundini
nakopa,’’anaeleza.
Anawawashauri wengine kuacha kukaa bila ya kazi ni vyema
wakajitokeza kujiunga na vikundi vya ushirika, ili waweze kuwa na shughuli
ambazo zitawapatia kipato cha halali.
Mwanachama wa ushirika wa ‘Tuaminiane’ wa Pembeni wilaya ya Wete, Omar Ali anaona vyama vya
ushirika ni moja ya hatuwa muhimu katika kujinasua na umaskini wa kipato.
Anasema kwake
fursa kubwa ambayo inampa uhakika wa maisha asasa ni kuwa na sehemu ya uhakika
ya kukopa fedha hasa pale anapotokezea na shida.
“Nimeshawahi
kukopa hadi shilingi 500,000 kwangu ni fedha kubwa, maana kabla ya kujiunga na
ushirika huu na kuanzisha kikundi cha kuweka na kukopa, sikuwa na uhakika,’’anasema.
Anaeleza kuwa vikundi hivyo vya kuweka na kukopa hutumika kama ni fursa ya haraka kupata fedha
za kujinasua na matatizo ya ghafla, katika kumuwezesha mwanachama kuondowa
changamoto zao.
Kwa upande wake mwanaushirika wa ufugaji kuku Juma Omar
wa Njuguni , anaieleza makala hii kuwa Sekta ya ushirika ni moja ya jambo
ambalo limewakombowa kutokana na umaskini ingawaje sio kwa haraka sana ila
Waswahili walisema kidogo kidogo ndio mwendo.
Anasema wao wanafuga kuku wa kisasa ambapo kuku mmoja ana
uzito wa baina ya kilo tano hadi saba na wanauza kwa kilo moja kwa shilingi 10,000,
na kupata faida ya kiasia.
“Iwapo tutawezeshwa kwa kupatiwa mikopo yenye masharti
nafuu, tutapiga hatuwa kubwa, kwani hivi sasa soko lipo, ingawaje sio kubwa“, anasema.
Akizungumza
na wanachama wa vikundi vya ushirika na Saccos, ukumbi wa Samael Gombani
Pemba, katika shamra shamra za siku ya Washirika Duniani , aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya ya Wete Abeid Juma Ali, alisema Serikali imekuwa ikisaidiana na vyama
hivyo katika kuwafanya Wanachama wake waweze kufikia ndoto zao.
Anaeleza kuwa, Saccos nyingi huwa zinaonekana kupata
mafanikio makubwa, baada ya kuanzishwa, lakini hufa kidogo kidogo kutokana na
baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu .
Wakati hayo yakifanyika, moja ya eneo ambalo serikali
imeshaanza kuweka mazingira, kwa kuwepo kwa vituo vinne kwa ajili ya masoko ya
uhakika.
Ni kujenga kituo kimoja kutoka kila wilaya kisiwani Pemba
Tumbe kwa wilaya ya Micheweni, Kifumbikai wilaya ya Wete, Michakaini wilaya ya
Chake chake na Kipitacho kwa wilaya ya Mkoani, kwa sasa kazi ya ujenzi
imeshaanza.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahoro Massoud,
anasema wastani wa wajasiriamali 500 watanufaika kwa wakati mmoja kwa vituo
viwili vya Chake chake na Mkoani.
“Kumalizika kwa vituo hivyo itakuwa ni fursa kwa
wajasiriamali wetu, ambao wamekuw wakihangaika kupata eneo la uhakika la kuuza
bidhaa zao,’’anasema.
Aisha Rashid Mohamed kutoka Mkoani anaeleza kuwa ushirika
umeweza kuwasaidia na kuwakombowa wananchi wakiwemo wanawake na Vijana na kuwa
kwenye hali mzuri kimaendeleo.
Nae Hadia Hamad Makame mkaazi wa Piki anasema kuwa
Ushirika kama utakuwa na watu wanaoelewana na waaminifu ni moja ya chanzo
kikubwa cha ajira.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikiwahamasisha
wananchi kila mara kuanzisha vikundi vya ushirika, ili waweze kujinasua na
umaskini na kuondosha wimbi la watu wanaosubiri ajira serikalini.
MWISHO.
WATU WA KAWAIDA
Omar Haji Omar wa …………..anasem
Khadija Haji Mlekwa wa ………..anasema
Hasina Issa Juma wa ………………….
MWISHO.
Comments
Post a Comment