HABIBA ZARALI, PEMBA:::
LICHA ya serikali kuimarisha huduma za akina mama na watoto
mijini na vijijini, ili wajifungulie hospitali, bado jitihada hizo zinaonekana
kubezwa na baadhi ya akina mama hao.
Tayari Unguja na Pemba
serikali imesogeza karibu vituo vya afya na kutowa elimu afya ya uzazi tofauti
na zamani, wapo akina mama hujifungulia majumbani wakisaidiwa na wakunga wa
jadi.
Ni dhahir kuwa akina
mama wanapobeza maelekezo hayo na kuamuwa kubakia majumbani hadi kujifunguwa
kunaweza kuwaletea madhara yatokanayo na uzazi.
Na ndio maana serikali
kupitia wizara ya Afya, wakawataka wakunga wa jadi kuwasindikiza mama
wajawazito hadi katika vituo vya afya na sio kuwazalisha wakiwa majumbani.
Na ndio maana hata
Raisi wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi katika hutuba zake za mara kwa mara, huitaka
wizara ya Afya kutowa huduma bora na kuona kwamba kunapunguwa vifo vya mama na
mtoto.
Uchunguzi wa makala
hii umebaini kuwa bado wapo akina mama ambao wanaendelea kupatwa na matatizo
yahusuyo uzazi kwa kuamuwa kujifungulia majumbani.
MAMA WALIOJIFUNGULIA MAJUMBANI
“Bado kidogo nipoteze
maisha kutokana na kujifungulia nyumbani, hata hivyo nimepata matatizo makubwa,
kwani sijuwi kama nitaweza kubeba tena ujauzito”, hiyo ni kauli ya Fatma
Abdalla (39) mkaazi wa Mwambe Mkoani Pemba.
Mwanzoni mwa mwaka
2022, alipojifungua mimba yake ya tano na aliamua kujifungulia nyumbani,
kutokana na uzoefu kwamba ameshazoea kujifungulia hapo, ingawa kwa bahati mbaya,
mtoto alitoka vibaya na kumsababishia matatizo makubwa.
Akionekana mwenye
huzuni baada ya kukumbuka mateso aliyoyapata, anasema alikuwa kwa mkunga wa
jadi, mtoto alitangulia kutoka makalio, akakwama sehemu ya kichwa na mkono.
Anasema mkunga wa jadi
hakuwa na namna ya kuweza kumsaidia, ndipo ilipoamuliwa kupelekwa hospitali ya
Abdalla Mzee Mkoani, akiwa amechanika.
“Niliponea chupu
chupu, nilipoteza damu nyingi, nikapoteza fahamu na mguu wangu wa kushoto ukafa
ganzi kwa miezi mitatu, sikuweza kusimama,” anaeleza.
Zuwena Juma (35)
mkaazi wa Chambani anasema, bado kidogo apoteze maisha, lakini huku na huku
alimpoteza mtoto wake, baada ya kukaa nyumbani akiona ataweza kujifunguwa
mwenyewe.
Mtoto wake hakutoka kwa
hali ya kawaida, ila baada ya kufikishwa hospitali ya Abdalla Mzee, alifanyiwa
upasuwaji na maisha yake yakaokoka.
Sauda Salim (59)
mkaazi wa Chake Chake, anaeleza jinsi mkwewe alivyopata tabu, alizalia kwa
mkunga wa jadi na kusema kuwa mtoto alitoka vibaya mkunga hakuwa na uwezo tena
wa kumsaidia.
‘’Kwa hakika nilimuona
mkunga akienda huku na kule, ili kuhakikisha anaokoa maisha ya mtoto, lakini
hatimae alipoteza maisha na mimi nilikuwa hali mbaya hasa baada ya kupoteza
damu nyingi,’’anakumbuka.
MASHUHUDA
Munira Mohamed Ali
(55) Mkaazi wa Kengeja, anatoa ushuhuda kwa aliyoyaona kwa jirani yake
alivohangaika tokea majira ya saa 12:00 asubuhi, hadi saa 4:00 asubuhi, ambapo
bado zalio halikutoka.
Anasema alimuona mama
huyo akipoteza damu nyingi, ndipo walipoamua kumpeleka hospitali ya Abdalla
Mzee Mkoani, akiwa na hali mbaya.
“Mtu akisha jiona
kashazaa mimba tatu au nne hujiona mzoefu hukataa kujifungulia hospitali,
hubahatisha kwa kujifungua nyumbani, jambo ambalo ni hatari,”anasema, Munira.
Hafidh Mohamed (30)
Mkaazi wa Msuka Wilaya ya Micheweni anasema, wanaume wana jukumu la kuwahimiza
wake zao kuzalia hospitali, ili kujiepusha na matatizo.
“Mimi siwezi
kusahau tokea siku niliyomuona jirani yangu anavyoteseka, tukiwa tunamkimbiza
hospitali baada ya kukaa siku nzima, kwa mkunga wa jadi bila ya kujifunguwa na
kupoteza gharama kubwa zisizo za lazima,’’anakumbuka.
Hassina Issa Omar wa
Mtambile, ambae ni mkunga anasema, wakati mwengine huamshwa usiku kati, na
hushwindwa kuwarejesha wazazi.
‘’Tumeshaelekezwa
kuwa, mama yeyote asijifungulie nyumbani, lakini wapo wakaidi na wakati ndio
hao wanaotufikia mikononi mwetu,’’anasema.
Mohamed Kombo wa
Mwambe anasema mara nyingi ni ukaidi wa wanawake wenyewe, kwenda hospitali
mapema na hatimae hujikalia mpaka wakafikwa na matatizo.
WALIOJIFUNGULIA HOSPITAL
Awena Abdalla wa Kiwani
Mkoani, anasema moja ya jambo linalomshawishi kujifungulia hospitali ni huduma
za lazima kama kuangalia uwingi wa damu.
‘’Hii ni mimba yangu
ya nne, zote najifungulia hospitali, maana hata mume wangu na mama mzazi
hakubali wazo la kwenda kwa mkunga,’’anasema.
Siti Othman Mohamed wa
Kengeja, anasema faida anayoiyona anapojifungulia hospitali ni kupata dawa za
kuhimiza uzazi.
‘’Niliwahi mimba yangu
ya sita, kujifungulia kwa shangazi yangu, alitumia nguvu wakati nataka
kujifungua, na baadae, nilikimbizwa hospitali kwa matibabu,’’anasema.
Hata Aisha Haji
Ibrahimu wa Mtuhaliwa, anasema ushauri nasihi na huduma bila ya malipo, ndio
jambo kubwa linalomvutia kujifungulia hospitali.
‘’Lakini hata
ikitokezea unaukosefu wa damu, mtoto amekwama au umepata kifafa, wataalamu
wanakushughulikia na hayo ukiwa nyumbani ni kukikaribia kifo,’’anasema.
WATAALAMU WA AFYA WANASEMAJE
Muhudumu wa mama na
watoto, hospitali ya Abdalla Mzee Pemba, Rabia Mohamed Ussi, anasema tatizo
kubwa linalo gharimu maisha ya akina mama na watoto wakati wa kujifungua, ni
kucheleweshwa kufikishwa hospitali.
“Mama anapokuja
hospita huwa hali imesha kuwa mbaya pamoja na juhudi tunakazochukua basi
utakuta anapoteza maisha mama au mtoto na mara nyingine wote wawili, “anasema.
Kwa mwaka 2020 akina
mama 286 walijifunguwa kwa njia ya upasuaji, kati yao 27 walifanyiwa upasuaji kwa
njia ya dharua ili kuokoa maisha yao na watoto, lakini hata hivyo watoto 7 na
mama mmoja walipoteza maisha.
Kwa mwaka 2021
waliojifunguwa kwa upasuaji ni 310 kati yao 39 wamefanyiwa upasuaji wa dharura
ambapo wamama 18 wamepoteza watoto na mama wanne wamepoteza maisha.
“Kati ya hao mama
waliofanyiwa upasuaji kwa dharura walifika hospitali wakiwa wanamwaga damu
nyingi, watoto kutokeza mkono mwanzo na kodi ya mtoto kutoka nje”,alisema.
Amina Ali Mbarouk, ambaye
pia ni Muhudumu wa Mama na watoto katika hospitali hiyo, anasema licha ya kuwa
wanapewa elimu lakini bado wapo akina mama hawajaamuwa kujifungulia hospitali.
“Matatizo kama ya
kukwama kwa zalio, kuchanika msamba, yote haya husababisha mama kutokwa na damu
nyingi, mkunga wa jadi hawezi kumsaidia,”anasema, Amina.
Ofisa muuguzi wa
Wilaya ya Mkoani Pemba Moza Muhamed Ali anasema wakunga wa jadi hawaruhusiwi
kuzalisha majumbani, isipokuwa wanahimizwa kuwaongoza hadi hospitali, kwani
kuna matatizo mengi ya uzazi yanayoweza kujitokeza na hushindwa kuyakabili.
“Changamoto ambazo
wanapozalisha nyumbani hushindwa kuzikabili ni pamoja na mzazi kumwaga damu kwa
wingi, kupasuka fuko, mtoto kutanguliza makalio ,mkono ama kiungo
chochote”,anasema
Ofisa Mdhamini Wizara
ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali anawasisitiza akina mama kwenda katika vituo
vya afya mara tu wanapojigunduwa na ujauzito.
Hii anasema ni kwa ajili
ya kupata huduma za awali na elimu ili kuweza kulea mimba kwa hali ya usalama
pamoja na afya yake kwa ujumla.
Anasema, Serikali
imeamua kuwasogezea karibu huduma hiyo, kwa kuongeza vituo mbali mbali vyenye
madaraja ya pili kila wilaya, na kwa sasa Zanzibar ina Mtandao mzuri wa vituo
vya Afya.
“Kwa sasa kuna wadau
wa maendeleo ambao wamejitokeza na wanaendeleza kusaidia eneo la mama na mtoto,
ili kupata huduma ambazo ni za bora sahihi na kwa wakati,’’anafafanua.
Mdhamini Bilali
anawataja wadau kuwa ni hawa wa wanaokujana mradi wa M-mama ambao
utawanufaisha kina mama kufika hospitali mapema, kujifungulia spitali na
kupunguza vifo vya mama na mtoto.
WAKUNGA WA JADI WANASEMAJE
Wahida Mohamed Saidi
wa Mkanyageni anasema wizara ya afya imeshawapa elimu ya kuwasindikiza wazazi
hospitali kabla kuwazalisha ili kunusuru matatizo wanayoyapata.
“Akina mama wengi
hupuuza kwenda spitali mapema na kujikalia majumbani mpaka hali inapokuwa mbaya,
jambo ambalo hulazikmika kuwazalisha majumbani bila ya kutarajia,”anasema.
Siti Khamis Juma wa
Mwambe anasema juhudi kubwa wanayoifanya ya kuelimisha akina mama kwenda hospitali
mapema, ingawa bado wapo wanaokaidi.
Anasema husuburia
mpaka hali ikawa tete na wakati mwingine hufanya makusudi wala si kwa bahati
mbaya kama wanavyosingizia.
“Wapo wazazi wenye
tabia ya kutuita wakiwa hali mbaya na dalili zote za kutaka kuzaa
zimeshajionesha, ndipo kama binadaamu huona tusaidie kuzalisha lakini huku
tukijitayarisha kuwakimbiza haraka hospitali maana kuna matatizo yakiwatokezea
hatuyawezi,”alisema.
mwisho
Comments
Post a Comment