NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
RIPOTI
ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ‘UNICEF’, lile la masuala ya
wanawake, UN-Women na shirika la Plan International, inaonesha idadi ya wasichana
wanaoandikishwa skuli, kwa sasa ni kubwa kuliko wakati wowote.
Ripoti hiyo iliotolewa mwaka 2020,
inaeleza idadi ya wasichana watoro skulini tangu mwaka 1995 imepungua na sasa wasichana
wana fursa ya kusoma skuli za sekondari, kuliko wavulana.
HALI
ILIVYO NCHINI
Mitandao inaripoti, kiwango cha
wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari nchini Tanzania ina uwiano nzuri,
ambapo wasichana hufikia karibu nusu ya wanafunzi wanaosajiliwa.
Hata hivyo, kutoka elimu ya msingi hadi
sekondari kwa ujumla asilimia 56 ni ya wasichana, huku asilimia 34 pekee ndio
wanaomaliza elimu ya sekondari.
Huku mitandao ikiripoti, hata Zanzibar
kunauwiano mzuri wa wasichana wanao jiunga na masomo ya sekondari, kati yao na
wavulana.
Idadi ya wanaomaliza na kufaulu ni
pungufu ikilinganishwa na wavulana, kwa kila mwaka.
Wakati dunia ikishuhudia ongezeko la
idadi ya wasichana wengi skulini wanaoingia sekondari, inashuhudia idadi ndogo
ya wasichana wanaomaliza kwa mafanikio.
Hii inaonyesha uwepo wa vikwazo mbalimbali
vinavyowakabili wasichana, katika safari yao ya utafutaji wa elimu hasa
sekondari, ambavyo ni sababu ya kutofikia malengo yao.
Kwa mujibu wa ripoti za UNESCO na UNICEF
wasichana ni miongoni mwa waathiriwa wa unyanyasaji, ukatili wa kingono,
kimwili na kisaikolojia wanapokuwa maskulini au maeneo ya karibu.
Huku aina hizi za udhalilishaji
zikiathiri zaidi ya watoto na vijana millioni 200 ulimwenguni kote (wasichana
na wavulana).
SASA CHANGAMOTO NI ZIPI
Khansaa Ali Makame ni mwanafunzi wa
kidato cha pili skuli ya sekondari ya Mitiulaya anasema, moja ni kutembea
umbali mrefu, katika kuzifikia skuli hasa za sekondari.
Anaeleza hili, husababisha kukutana na vishawishi
vingi wanapokuwa njiani, ambavyo maranyingi, hupelekea udhalilishaji.
“Moja ya changamoto ni kutembea umbali
mrefu tunapokwenda skuli, hili baadhi ya watu huchukulia kama fursa ya kufanyiwa
vitendo vya udhalilishaji kwa kutushawishi kwa ahadi za ‘lift,’’
anaeleza.
Anasema mwisho wake husababisha ubakwaji
au mimba za umri mdogo na kupelekea kukatisha masomo na kuzima ndoto zao.
Khadija Said Mattar mwanafunzi wa kidato
cha tatu skuli ya sekondari Chasasa Wete, anaoba lugha chafu na za kukatisha
tamaam kutoka kwa watu mbalimbali, ni changamoto nyingine kwao.
Tena hata wakiwa kwenye gari, mara
nyingi watu huzungumza nao kwa lugha tofauti na abiria wingine, huku lugha hizo
zikionyesha kutokuthamini utu na heshima yao.
“Wasichana tunachangamoto nyingi katika
juhudi zetu za utafutaji elimu, binafsi nimewahi kutolewa maneno makali na yenye
kuumiza na watu tofauti kwa zaidi ya mara moja,’’ananikumbusha.
Mwanafunzi Bilha Khamis Suleiman wa
kidato cha nne skuli ya sekondari Mitiulaya, anaeleza changamoto nyengine ni wazazi
kuwatwisha wasichana majukumu ya nyumba.
Ansema imeshazoeleka msichana anapofika
sekondari wazazi wengi hubadili muelekeo, badala ya kumuandaa aelimike, huanza
kuwaandaa kuwa mamama wa nyumbani.
Mundhir Maalim Omar mwanafunzi wa kidato
cha tano skuli ya sekondari Chasasa Wete Pemba, anasema amewahi kushuhudia
mwanafunzi mwenzake, tena msichana akifanyiwa udhalilishaji kwa kuitwa jina kwa
aina ya maumbile yake.
Anasema alimshuhudia msichana huyo akipoteza
furaha na kujiamini kwake kwa siku kadhaa kila anapo kuwa darasani.
WAALIMU
WANASEMAJE
Khadija Bakari Sharifu, Msaidizi Mwalimu
Mkuu skuli ya Sekondari Mitiulaya anasema, changamoto za kifamilia, kama
utelekezwaji ni miongoni mwa changamoto inayowakabili wasichana wa sekondari kutofikia
ndoto zao.
Anaeleza kuwa, hii huwakumba baadhi ya
wanafunzi wanaotelekezwa na kulelewa na
watu wengine au mzazi mmoja.
Mwalimu Salum Ali Yussuf, anaeleza bado
wapo wazazi na walezi, ambao huona ni hasara kubwa kuwasomesha watoto wa kike,
kwa sababu wanahofia kupoteza gharama zao, jambo ambalo sio sahihi.
“Baadhi ya wazazi au walezi wanaamini
watoto wao wa kike hawana haki ya kupata elimu ya juu, hivyo huamua kuwaozesha
mapema, na hii ndio changamoto kubwa kwa wasichana,’’ anaeleza.
USTAWI
WA JAMII
Salma Saleh Hamad Afisa ustawi wa Jamii Wilaya
ya Wete, anikiri kuwa wasichana ni watu wanaopitia changamoto kadhaa, ikiwemo
za udhalilishaji.
Kumbe wakiwa sekondari, vishawishi huwa
vingi kwao na kupelekea udhalilishaji wa aina mbalimbali ikiwemo, kubakwa na
kupata mimba wasizozitarajia.
Anaongeza wasichana hasa wa sekondari
wanapaswa kuangaliwa kwa karibu na familia zao ili kupunguza hili.
Anasikitishwa na wazazi na walezi wanao
kubali suluhu za kifamilia na sio kisheria, pale watoto wao wanapopewa ujauzito
au udhalilishai mwingine.
Safia Salim Said, yeye ni Mratibu
wanawake na watoto shehia ya Kisiwani wilaya ya Wete, anasema wasichana hasa wakishafika sekondari,
hubebeshwa majukumu ya familia na kupoteza mwelekeo wa elimu ya juu.
Anasema hali hii kwa kiasi kikubwa,
hupelekea wasichana kushindwa kufanya vizuri katika masomo na wengi wao hubakia
nyumbani na kisha kuolewa.
MIKAKATI
YA KUKABILIANA NA HILI
Mwanakhamis Hafidh Juma wa Kizimbani
Wete Pemba, anasema wamekuwa wakiwasaidia wasichana jinsi ya kukabiliana na
changamoto hizo, ikiwemo ya vishawishi.
Msaidizi Mwalimu Mkuu skuli ya sekondari
Mitiulaya, Khadija Bakar Sharif anasema, wanaweka mahusiano mazuri, baina yao
na wanafunzim ili kubaini changamoto wanazopitia.
Afisa ustawi wa Jamii wilayani humo, Salma
Saleh Hamad, anasema ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau wingine, wamekuwa
wakiwaelimisha wasichana hao.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania Zanzibar -TAMWA Zan kupitia Afisa Programu wa kupambana na ukatili na unyanyasaji,
Asiya Hakim, ametahadharisha juu ya changamoto zinazo wakumba wasichana hasa
wakiwa sekondari katika kutafuta kwao elimu.
Anasema katika kupunguza athari hizo, TAMWA
imewajengea uwezo waandishi wa habari, kuripoti
matukio ya udhalilishaji, hasa kwenye sehemu ambazo hazipewi kipaumbele
ikiwemo, skuli na vyuoni.
Hili linatekelezwa kupitia Mradi wa ‘Tunaweza
Pamoja’ unaotekelezwa na UN- Women kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar, hasa
kwa wilaya za Wete na Micheweni kwa Pemba.
SERIKALI KUU INAFANYA NINI
Ofisa Mdhamini wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, anasema katika kutatua changamoto
za wasichana, wizara inajenga skuli katika maeneo ya karibu.
“Tunajenga
skuli kwenye maeneo ya karibu, ili wanafunzi wasitembee umbali wa zaidi ya kilomita
tatu au tano, ili wasipite katika maeneo hatarishi,’’anafafanua.
Anafahamisha kuwa, wizara inatoa mafunzo
ya stadi za maisha kwa wanafunzi, kuanzia darasa la sita, ili wanapofika
sekondari, wawe wamejitambua na kujielewa.
Kumbe hilo, humuwezesha mwanafunzi kujua
mabadiliko yake ya kimwili na kumjenga kuyaelewa, ili kukabiliana na changamoto
zitokanazo na mabadiliko hayo.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Mgeni
Khatibu Yahya anasema, serikali ya mkoa kupitia idara ya ustawi, imekua ikiwasaidia
wanafunzi wenye mazingira magumu, ili kuhakikisha wanaepukana na changamoto
zinazowakabili.
Eeneo jingine, Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul inasema, vipaumbele vyao kwa mwaka
2026/2027 ni pamoja na kukuza utekelezaji wa mpango wa pili wa kitaifa, wa
kupambana na ukatili na udhalilishaji.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeridhia uwepo wa sheria, kanuni na mikataba ya kikanda na kimataifa
inayotetea haki za wanawake na wasichana.
Miongoni mwao ni mkataba wa umoja wa
mataifa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake wa mwaka 1993.
TAKWIMU
Takwimu za mwaka 2024 za Shirika la Afya
Duniani (WHO), zinaonyesha mwanamke mmoja, kati ya watatu, wamewahi kufanyiwa
ukatili, katika kipindi cha maisha yake.
Kwa mujibu wa takwimu za ukatili na
udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, zilizotolewa na Ofisi ya Mtakwimu mkuu wa
serikali, mwaka 2024 kulikuwa na 1,809
ya ukatili na udhalilishaji wameripotiwa.
Takwimu hizi zinaonyesha waathirika
wengi walikua watoto ambao ni asilimia 84.3 ikifuatiwa na wanawake ambao ni
asilimia 11.7.
Aidha utafiti uliofanywa na shirika
lisilo la kiserikali, linaloendeleza usawa wa ukuaji wa kiuchumi na kijinsia
katika sekta isiyo rasmi (EFG), Tanzania 2017, unaonyesha wanawake wanakumbana
na viwango vya juu vya ukatili na udhalilishaji katika harakati zao za
kiuchumi.
MWISHO.



Comments
Post a Comment