SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha
ustawi na ulinzi wa watoto nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Zawadi Amour Nassor, wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika, leo tarehe 16 Juni 2026 katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake chake Pemba.
Alisema hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza kampeni za kupinga ukatili dhidi ya watoto, kuimarisha huduma za afya na lishe, kuhamasisha malezi chanya pamoja na kuendeleza ushiriki wa watoto katika masuala yanayowahusu.
"Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha ustawi na
ulinzi wa watoto, ikiwa
ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza kampeni za kupinga
ukatili dhidi ya watoto, kuimarisha huduma za afya na kuhamasisha
malezi chanya"
alisema.
Alieleza hatua hizo kwa pamoja
zinalenga kuimarisha ustawi wa mtoto na
jamii kwa ujumla, jambo litakalo jenga taifa bora na lenye nguvu hapo baadae.
Alisema kaulimbiu ya maadhimisho
ya mwaka huu inayosema “Linda Mtoto wa Afrika: Mpe
Afya Bora na Maisha Bila ya Udhalilishaji”, inajumuisha upatikanaji wa afya ya mwili, afya
ya akili, lishe bora, malezi yenye upendo, elimu bora, mazingira salama na
fursa za kushiriki katika masuala yanayomhusu, ambavyo kwa pamoja ni chachu ya ustawi wao.
"Kaulimbiu
hii inatukumbusha kuwa mtoto mwenye afya bora na anayeishi katika mazingira
salama yasiyo na aina yoyote ya udhalilishaji ana nafasi kubwa ya kukua,
kujifunza, kufanikiwa na kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na familia kwa
ujumla",
alisema.
Naibu Waziri huyo alendelea kueleza kua wizara kwa kushirikiana na wadau wa watoto imeona ni vyema kuwa na kaulimbiu inayoakisi masuala ya Afya na upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama, ili kuikumbusha jamii wajibu wake juu ya hili.
Aidha alisisitiza kua, maisha bila udhalilishaji yanamaanisha ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kimwili, kihisia, kingono, kutelekezwa, unyanyasaji mtandaoni, ajira za watoto na mila au desturi zinazoweza kuathiri ustawi wake.
Alieleza pamoja na mafanikio yaliyopo, kuna changamoto mbali mbali ikiwemo
ukatili na udhalilishaji wa watoto, baadhi ya watoto kukosa malezi stahiki,
afya ya akili na matumizi yasiyo salama ya teknolojia na mitandao ya kijamii,
ambapo zinazohitaji juhudi za pamoja katika kuzitatua.
Aidha alitoa mapendekezo kwa wadau
wa kulinda haki za watoto kuendelea kufanya uchambuzi wa changamoto
zinazochochea vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa Watoto na kuandaa
mikakati ya pamoja ya utatuzi
wa hayo.
Pia
aliendelea kutoa wito kwa wadau wanaotetea haki za watoto kuweka masuala ya watoto katika vipaumbele vya maendeleo ya
taifa kwa kuhakikisha sera, mipango na bajeti zinazingatia mahitaji ya watoto
katika sekta zote, na kuimarisha sheria zinazolinda haki za watoto na mipango ya udhibiti wa
haki hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Siti Abbas Ali alisema, katika kuhakikisha ustawi wa watoto,
kwa mara ya kwanza wizara imeweka bajeti ya mabaraza ya watoto, ili isaidie
kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Akiwasilisha mada ya wajibu wa
Jamii, wazazi na skuli katika upatikanaji wa maji safi na salama kwa mtoto
mkufunzi Fihim Abdalla Mohamed kutoka wizara ya Afya alisema, ni kulinda vyanzo
vya maji pamoja na kuimarisha usafi na usalama wa maji hayo majumbani.
Akizungumza kwa niaba ya watoto
walioshiriki maadhimisho hayo Mwenyekiti wa watoto bodi ya ushauri taifaKhamis
Abdallah Mbarouk ameipongeza wizara na asasi nyengine za Kiraia kwa kuandaa
maadhimisho hayo, huku akiisihi jamii iendelee kumtunza mtoto kwa ustawi wake
na maendeleo ya sasa na baadae.
Siku hii
ilianzishwa na Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mwaka
1991 kwa lengo la kuwakumbuka watoto waliopoteza maisha katika maandamano ya
Soweto nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni 1976.
Tukio lililotokea wakalipokua wakipinga mfumo wa ubaguzi wa rangi uliowanyima haki yao ya kupata elimu
bora na yenye usawa.
Kwa mwaka 2026 maadhimisho hayo
yamefanyika Kisiwani Pemba, ambapo watoto wa makundi mbali mbali, wakiwemo wenye ulemavu, wanafunzi na kutoka
mabaraza ya watoto walishiriki.
"Kwa pamoja,
tunaweza kujenga Zanzibar na Afrika ambayo kila mtoto atakuwa salama, mwenye
afya njema, mwenye furaha na mwenye uwezo wa kutimiza ndoto zake."
MWISHO




.jpg)
Comments
Post a Comment