MRADI WA ‘PAMOJA’ WABISHA HODI PEMBA, WAANZIA WILAYA YA CHAKECHAKE KWA MAJARIBIO, WANANCHI WAUFURAHIA
TAKWIMU kutoka Mtakwimu Mkuu
wa serikali Zanzibar, zinaendelea kutishia usalama wa wanawake na watoto wa
Unguja na Pemba.
Maana, kwa miaka mkitatu
iliyopita, imekusanya matukio 4,991 ya ukatili na udhalilishaji, ambao wengi wa
waathirika ni wanawake na watoto.
Ijapokuwa, namba inaonesha
kupungua kila mwaka kwa miaka hiyo, lakini kwa juhudi za serikali, washirika
wake wa maendeleo, taasisi binafsi na mtu mmoja mmoja, bado maumivu yapo.
Maana mwaka 2023,
ilikusanya matukio 1,954 ingawa mwaka uliofuata, yalishuka na kuripotiwa
matukio1,8 09, na mwaka jana, yakashuka tena na kuripotiwa matukio 1,228.
Utaona kuwa, mwaka 2023, matukio
1,954, yalioripotiwa, ingawa mwaka 2024 kulikuwa na mapungufu ya matukio 145,
maana yalikuwa 1,809 na mwaka 2025, kukiripotiwa pungufu ya 581 kati ya yale
yaliokusanywa 1,228.
Hapo sasa, ndio maana kwa
Zanzibar nzima, ukiyakusanya matukio hayo kwa kipindi kuanzia mwezi Januari
2023 hadi Disemba 2025, utabaini matukio 4,991 ya ukatili na udhalilishaji yameripotiwa.
Kwa wilaya nne za Pemba,
kwa kipindi hicho wilaya ya Chakechake, imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kila
mwaka, ukiwemo mwaka 2023 iliyorpoti matukio 108.
Wakati wilaya ya Mkoani
ikikusanya matukio 54, Wete matukio 93 na wilaya ya Micheweni iliyoko mkoa wa
kaskazini Pemba, ikiripoti matukio 43.
Mwaka 2024, wilaya ya Chakechake
ilioongoza tena, kwa kuwa na matukio 113, ikifuatiwa na Wete matukio 73, Mkoani
52 na Micheweni ikishika nafasi ya mwisho kwa Pemba, kwa matukio 46.
Takwimu zikazidi kuonesha
wilaya ya Chakechake kuwa, ndio inayoongoza kwa zile wilaya nne za Pemba, kwa
kusanya matukio 93, kwa mwaka 2025.
Wilaya ya Wete kama
kawaida, ilishika nafasi ya pili, kwa matukio 91, Micheweni nafasi ya tatu kwa
matukio 54 na Mkoani ikiwa na matukio 52.
Kwa ujumla takwimu hizo,
zinatoa sura ya kuwa, kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025, wilaya ya Chakechek
imekusanya matukio mingi zaidi, kuliko wilaya nyingine kwa Pemba, kwa 314,
wastani wa matukio 104 kwa mwaka na manane kwa mwezi.
Wilaya inayoshika nafasi ya
pili na Wete, kwa matukio 261, wastani wa matukio 87 kwa mwaka, na saba kwa mwezi.
Wilaya ya Mkoani matukio 158,
wastani wa matukio 52 kwa mwaka, na manne kwa mwezi na wilaya ya Micheweni ni
ya mwisho kwa kuripoti matukio 143, wastani wa matukio 47 kwa mwaka na matatu
kwezi.
MRADI WA ‘PAMOJA’ NA
UTAFANYA NINI CHAKECHAKE
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa
Masuala la Jinsia, kupitia Mradi wa ‘pamoja’ wa kukuza usawa wa
kijinsia Tanzania, Nyezuma Simai Issa, anasema Mradi huo, ni wa aina yake, na
utapunguza wimbi la ukatili na udhalilishaji, pindi utakapomalizika.
Kauli hii, aliitoa hivi
karibuni, ukumbi wa Samail Gombani Chakechake Pemba, wakati akielezea
muhutasiri ya utekelezaji wa mradi huo, kwa Kamati teule ya wilaya ya
Chakechake, ya utekelezaji wa mradi.
Anasema, jambo jipya ambalo
limo ndani ya mradi huo, ni ujenzi wa vituo vinane, vya makuzi na malezi ya
awali ya mtoto, ambapo kila wilaya kitajengwa kimoja.
Kumbe, lengo la kituo hicho
ni kuwapa nafasi wazazi na walezi, kujiendeleza kiuchumi, wakiwa na uhakika wa
malezi, kwa watoto wao.
‘’Kupitia mradi huu wa
miaka mitano, jambo kubwa ambalo limo pamoja na mingine mazuri, tutajenga vituo
vinane, kwa wilaya zote nane ikiwemo Chakchake, zilizopotiwa na mradi,’’anafafanua.
Jambo jingine, ni kuona
kila wilaya mradi unalikarabati jengo moja chakavu, na kwa ajili ya matumizi
kama, hayo ya awali.
‘’Mradi huu, pamoja na
kuanza kwa ujenzi wa vituo hivyo vinane, lakini pia unapanga kukarabati majengo
mingine machakavu kwa wilaya zote, ili nayo yatowe huduma za makuzi na malezi
ya awali ya watoto ikiwa yapo,’’anaeleza.
Zuri zaidi, ijapokuwa Mkoa
wa Mjini Magharibi, haumo kwenye mradi, lakini mradi utajenga kituo cha kitaifa
cha msaada wa kisaikolojia.
Maana wapo ambao, aidha
baada ya kudhalilishwa ama kufanyiwa ukatili, watazungurukwa na msongo wa mawazo,
hivyo kituo hicho kitakuwa na wataalamu wa kazi hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano
huo, Mtaalamu wa masuala ya kijamii, kupitia Mradi huo, Ali Wadi Makame,
anasema ndani ya mradi huo, utawapa mikopo wanawake, waliojikusanya kwenye
vikundi vya ushirika.
Ingawa hayo yatakuja, baada
ya kuwapa mafunzo maalum, ya jinsi ya kujikwamua na umaskini na matumizi ya
fedha hizo.
‘’Mradi huu, utawapa mikopo
ya fedha moja kwa moja wanawakwe walioanzisha vikundi vya ushirika na ambavyo
vimesajiliwa, ili sasa iwe sababu ya kukuza pato lao,’’anabainisha.
Lakini, akawageukia waanchi
wa Unguja na Pemba, na hasa ambao mradi huo unatekelezwa, kujenga ushirikiano
na maafisa wao, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi.
Kuhusu kanuni za maadili, anasema
mradi unataka wajumbe hao kuheshimiana na kujengeana nidhamu wakati wote,
wanapokua kwenye shughuli zao.
‘’Ni jambo la kawaida kwa
sisi watumishi, sasa kupitia mradi huu zitakuwepo na kisha zitasainiwa na
wajumbe wa kamati zote,’’anaeleza.
Kwa sasa mradi huo kwa
kuanzia, unatekelezwa kwa majaribio katika wilaya za Kati kwa Unguja na
Chakechake kwa Pemba.
Ingawa kisha wilaya
nyingine za Kusini, Kaskazini ‘A’ na ‘B’ kwa Unguja na wilaya za Mkoani, Wete
na Micheweni kwa Pemba zitafuata.
WANANCHI WA CHAKECHAKE
WANASEMAJE
Baadhi ya washiriki wa
mkutano huo, wanasema mradi huo ni nzuri, na umekuwa na mwelekeo wa aina ya
pekee, katika kupunguza wimbi la ukatili na udhalilishaji.
Katibu wa Kamati ya
kupambana na udhalilishaji wilaya ya Chakechake Rashid Said Nassor, anasema
bado vitendo vya udhalilishaji vinaendelea kutokea.
‘’Kwa aina ya mradi huu
ulivyolenga, utaisaidia sana wilaya ya Chakechake, ambayo kwa Pemba, ndio
kinara wa kukusanya matukio mingi ya udhalilishaji,’’anasema.
Salma Khamis Haji, anasema
kilichobakia ni kwa jamii, ni kutoa ushirikiano na watendaji walioteuliwa
kupitia mradi huo.
Hidaya Mjaka Ali, ambae ni mjumbe wa Kamati tendaji ya
Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar JUWAUZA, anasema wilaya ya Chakechake,
inaelekea kupata mwaroubaini, wa vitendo hivyo.
‘’Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia
vipo na vina athari, ingawa watu wenye ulemavu huwa mara mbili, hivyo ujio wa
mradi wa ‘pamoja’ itakuwa dawa,’’anasema.
Mkuu wa wilaya ya Chakechake Mgeni Khatib Yahya,
anasema elimu zaidi inahitajika kwa jamii, ili isiendelee kuwa kinara wa
matukio ya udhalilishaji.
Mkurugenzi wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya
Chake chake ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, anasema wako tayari, kushirikiana
kwa karibu na watekelezaji wa mradi huo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla
Hussein Mussa, anasema miradi kama hiyo ni muhimu kwa jamii, ili kujua njia za
kujiepusha na vitendo vya jinai.
Mjumbe wa baraza la watoto shehia ya Wawi wilaya ya
Chakechake Mohamed Juma Othman, anasema moja ya njia ya kupunguza matukio hayo,
ni kwa wakosaji kupewa adhabu kali.
Mradi wa kukuza usawa wa kijinsia Tanzania ‘pamoja’
umeundiwa timu kadhaa, ikiwemo za kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na
ufuatuliajia na tathmini.
Jingine lililomo ndani ya mradi huo wa miaka mitano, ni
kuwepo kwa mtaalamu wa mazingira, ukiwa na lengo la kukuza fursa za kiuchumi,
kwa wanawake na kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Mradi huu ambao unafadhiliwa na Benki ya dunia,
unatekelezwa, kwenye wilaya za Chake, Mkoani, Micheweni, Wete kwa Pemba,
Kaskazini ‘A’ na ‘B’, Kati na Kusini kwa Unguja.
Mwisho

Comments
Post a Comment