NA
MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
UKATILI
na udhalilishaji dhidi ya wanawake na wasichana unasalia kuwa kitendo cha
ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani kote.
Ambapo kila mwaka makadirio ya wanawake
milioni 316 sawa na asilimia 11 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 45, hukutana
na vitendo hivyo duniani kote, kwa mujibu wa mitandao ya kijamii.
Udhalilishaji huo unaweza kua wa
kimwili, kingono au kihisia.
Takwimu za mwaka 2024 za Shirika la Afya
Duniani (WHO), zinaonyesha mwanamke mmoja, kati ya watatu amewahi kufanyiwa
ukatili huo katika kipindi cha maisha yake.
Kwa mujibu wa takwimu za ukatili na
udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, zilizotolewa na ofisi ya Mtakwimu mkuu wa
serikali, mwaka 2024 kulikuwa na 1,809
ya ukatili na udhalilishaji wameripotiwa.
Takwimu hizi zinaonyesha waathirika
wengi walikua watoto ambao ni asilimia 84.3 ikifuatiwa na wanawake ambao ni
asilimia 11.7.
Aidha utafiti uliofanywa na shirika
lisilo la kiserikali, linaloendeleza usawa wa ukuaji wa kiuchumi na kijinsia
katika sekta isiyo rasmi (EFG),Tanzania 2017, unaonyesha wanawake wanakumbana
na viwango vya juu vya ukatili na udhalilishaji katika harakati zao za
kiuchumi.
Hasa katika sekta zisizo rasmi ikiwemo
masokoni.
Hili linaonyesha namna wanawake wanaofanyakazi
katika sekta hizo wanavyo andamwa na changamoto mbalimbali.
Changamoto ambazo kwa namna moja ama
nyengine, zinarejesha nyuma ustawi wao na taifa.
Kwani ripoti ya ofisi ya taifa ya
takwimu (NBS) ya mwaka 2017, kuhusu hali halisi ya wanaume na wanawake
wanaofanya kazi inaonyesha, idadi ya wanawake wanaofanya kazi katika sekta zisizo
rasmi, ni asilimia 51, huku walio katika mashirika na serikali ni asilimia 18 hadi 28.
Utafiti wa (EFG) pia unaonyesha hadi
asilimia 96 ya wanawake, hukumbana na ukatili, unyanyasaji na udhalilishaji,
katika maeneo ya kazi ikiwemo sokoni.
Ukatili huo unaweza kua wa kiuchumi, kimwili
na kisaikolojia, ambao mara nyingi hufanywa na wasimamizi wa masoko na wateja.
Yote hayo hutokea kwa uwiano
unaoshabihiana, katika maeneo mbalimbali,
ingawa hutofautiana, kulingana na shughuli au biashara mtu anayofanya na
eneo husika.
SIMULIZI
ZA WANAWAKE SOKONI
Mmoja ya wanawake waliowahi kukumbana na
udhalilishaji katika soko la mjini Wete, Tahiya Said Abeid, anaefanyabiashara ya
viungo, anasema, haikua rahisi kwake kuingia sokoni hapo.
Baada ya mkulima wa magimbi aliemuuzia
bidhaa hiyo, kuvamia sehemu yake ya biashara na kumchukulia tungule zake, pale
yeye aliposhindwa kumaliza kurudisha fedha walizokubaliana.
“Kwa vile sina mtaji wa kutosha kuna
siku nilichukua magimbi kwa mkulima, ili niyauze kwa shilingi 230, 000, nikamlipa
shilingi 200,000 na fedha iliyobakia, tukakubaliana avumilie kwa siku mbili,
aliporudi nikawa sijaipata, hapo akavamia sehemu yangu ya biashara na kuchukua
bidhaa zangu,’’alilalamika.
Maryam Mohamed Mgeni, mfanyabiasha soko
la Kifumbikai Wete anasema, aliwahi kutolewa maneno machafu na yakuumiza, baada
ya kuchelewa kurejesha chenji ya mteja.
Anaeleza alipokea maneno mabaya, makali,
yenye kuumiza na kukatisha tamaa na kusababisha kutokwa na machozi, mbele za wenzake.
‘’Kwa udhalilishaji nilioupata siku hiyo,
nililazimika kufunga biashara na kurudi nyumbani mapema, baada ya kujisikia
vibaya,’’anasimulia.
Wengi wa wanawake waliozungumza na
mwandishi wa habari hizi, walilalamikia hali ngumu ya uchumi, ndio inayosababisha
wao kukutana na changamoto za ukatili na udhalilishaji.
Mfanyabiashara Fatma Said Ali wa soko la
Mjini Wete anasema, uwepo wa masharti mengi ya upatikanaji mikopo, mwenendo
mrefu wa ufuatiliaji mikopo, hiyo na
watu kukataa kuwapa dhamana ya mikopo wajasiriamali wanawake, walioko masokoni
ni ukatili wa kihisia kwao.
“Ukiachia kukatishwa tamaa kwa maneno,
wakati mwingine kushikwa bila ridhaa, pia hii tabia ya watu kukataa kutupa dhamana
tukiomba mikopo, na pingamizi nyenginezo kwetu,’’anaeleza.
Fatma na wafanyabiashara wengine
wanawake sokoni hapo wanasema, wameshawahi kuunda kikundi kwa ajili ya kuomba
mikopo, ili wajiinue kiuchumi, ikashindikana kutokana na kuwepo kwa mchakato
mrefu wa upatikanaji wake.
Salum Muumini, (si jina la kerasmi)
anaeleza amewahi kushuhudia mwanamke aliekua mfanyabiashara wa soko la
Kifumbikai Wete, miaka miwili iliopita kushikwa shikwa bila ya
ridhaa yake.
‘’Hasa hawa chukuaji na watoaji mizigo
ndani ya soko, huwa wanawadhalilisha wajasiriamali wanawake, maana huwashika na
kupinga vikali,’’anasema.
Omar Haji Kassi, anasema aliwahi kushuhudia
kitendo hicho kisicho cha kiungwana, kwa mwanamke aliyekuwa akiuza samakini nae
kushikwa na kulazimika kwenda Polisi.
‘’Sikujua ile kesi iliishia vipi, lakini
yule mwanamke hapa amehama na sikia kwa sasa yuko Unguja Fungu refu kwa biashara
ya kuanika dagaa,’’anaelezea.
Ifahamike vitendo hivyo ni kinyume na
matakwa ya sheria za nchi, mikataba ya kikanda na kimataifa inayosisitiza
usalama wa mwanamke popote alipo.
Mfano mkataba wa kimataifa wa mwaka 1976
wa kupambana na aina zote za ukatili dhidi ya wanawake (CEDAW), katika
mapendekezo namba 19 na 35, unahimiza serikali kuwalinda wanawake, dhidi ya
ukatili wa kijinsia.
Ibara ya13 ya itifaki ya haki za
binaadamu wanawake barani Afrika Protocol to the African Charter on Human
and Peoples Rights of Women in African’ wa mwaka 2003 ulioanza kutumika
rasmi 2005, inasisitiza nchi wanachama kuhakikisha ulinzi na hifadhi kwa
wanawake wanaofanyakazi katika sekta zisizo rasmi.
Ifahamike kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake
ni jukumu la kila mtu, ndio maana Chama cha waandishi wa habari wanawake
Tanzania TAMWA–Zanzibar, imekuwa ikipinga kwa vitendo vitendo hivyo.
Hao
yenyewe imekuja na mradi wa “Tunaweza pamoja” unaolenga kupinga
vitendo vya ukatili kwa wanawake na wasichana.
Anasema lengo la mradi huom ni
kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuripoti
matukio hayo hasa katika maeneo yasio rasmi.
‘’Ndio maana sehemu ya mradi huu, tumeshawajengea
uwezo waandishi wa habari 40, kwa Unguja na Pemba, ili kuhakikisha wanakuwa weledi
kuchimbua matendo hayo.
SERIKALI
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Mgeni
Khatibu Yahya anasema, wanawake waungane kujilinda na vitendo hivyo, kwa
kuviripoti katika mamlaka husika.
Kwa upande wa wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto vipaumbele vyake kwenye bajeti ya 2026/2027, imedhamiria
kupambana na ukatili na udhalilishaji, dhidi ya wanawake na watoto.
Akiwasilisha bajeti hiyo waziri wa
wizara hiyo Anna Athanas Paul, anasema, wizara itawawezesha wanawake kiuchumi,
ili wajitegemee lengo likiwa ni kupunguza ukatili na udhalilishaji dhidi yao.
“Wizara inafanya juhudi za ufuatiliaji
wa majukwaa na vikundi vya wanawake kupitia mradi wa ‘PAMOJA’ na ‘Dk.
Mwinyi Boosting fund’ ambao unakusudia kutoa mikopo ya masharti nafuu,
kwa walengwa,” anaeleza.
Aidha Rais wa Zanzibar na Dk.Hussein Ali
Mwinyi, katika hutuba zake mbalimbali amekua akisisitiza kua, ukatili na
udhalilishaji ni janga la kidunia, linalohitaji nguvu ya pamoja kulishinda.
Ndipo serikali ya awamu ya nane,
ikaanzisha mahakama maalumu za kushughulikia kesi za udhalilishaji, ili
watuhumiwa wa kesi hizo, wachukuliwe hatua.
NINI ATHARI YAKE
Mfanyabiashara wa soko la Wete Haji Juma
Makame, anasema kwanza ni kudumaza uchumi wa wanawake, walioamua kujitegemea.
Mayasa Hassan Kombo wa Mtemani Wete,
anasema ni kuendelea mfumo dume katika maisha ya wanawake ya kujikuza kiuchumi.
Kaimu Mratibu TAMWA Pemba Amina Ahmed
anasema, ni kudhoofisha ndoto za wanawake kwenye kukuza pato lao.
Shiekh Said Ahmad Mohamed, anasema ni
kuendeleza udhalilishaji wa kiuchumi kwa wanawake, katika maeneo yasio maarufu.
ZIPI
NJIA KUDHIBITI HILI
Mfanyabiashara wa soko la mjini Wete
Tahiya Said Abeid anasema, ni serikali na wadau wingine wa maendeleo, kuwawezesha
wanawake waofanyabiashara masokoni, kwa mitaji yenye masharti nafuu.
Hamad Omar, ambae nae ni mfanyabiashara soko
la Kifumbikai Wete, anasema ni elimu kwa wanaume hasa waliopo masokoni, kuhusu
dhana ya udhalilishaji.
‘’Tulishazoea kuwa udhalilishaji ni ulawiti,
ubakaji, lakini hata kuangushiwa bidhaa chini, matusi, kuwashika shika wanawake
ni hatari kwao,’’anashauri.
Sadri
Mussa Said Msimamizi wa masoko na mazingira wilaya ya Wete anashauri, ni vizuri
wafanyabiashara wanawake waliopo sokoni wawatumie viongozi wao wa masoko,
kuripoti vitendo wanavyofanyiwa.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya
Kisiwani Wete, anapendekeza, serikali na washirika wa maendeleo, kuwekeza
katika harakati za kuwasaidia wanawake, kiuchumi na taaluma.
Afisa Maendeleo ya jamii wilaya ya Wete Salma
Saleh Hamad, anashauri kuwa ili wanawake waepukane na ukatili na udhalilishaji sokoni,
ni lazima waripoti vitendo hivyo badala ya kuvifumbia macho.
MWISHO



Comments
Post a Comment