Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya
Makaazi Zanzibar Rahma Kassim Ali amesitisha ujenzi wa michezo ya baharini
(Water Sports) unaojengwa na Muekezaji NJ Water sports eneo la fukwe za bahari
Matemwe Wilaya ya Kaskakazini ‘A’’ kwa madai ya kukiuka kanuni na sheria ya
Ardhi.
Agizo hilo amelitoa mara baada ya
kufanya ziara katika eneo hilo ambalo linadaiwa kuwa na mgogoro wa ardhi baina
ya Muekezaji NJ Water Sports na Matemwe Bangaloes ambapo kesi ya mgogoro huo
imeshafikishwa Mahakama ya Ardhi Gamba Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.
“Nimelazimika kusitisha ujenzi
unaoendelea ili kuweza kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo ikiwa ni msimamizi mkuu
wa masuala ya ardhi" sitoweza kuacha ujenzi uendele wakati kesi iko
mahamani alisema Waziri huyo.
Alisema Mahakama ya Ardhi Gamba imeshatoa maamuzi ya kusimamisha ujenzi wa muekezaji NJ
Water Spots ambae anadaiwa kuingia eneo la
mwekezaji mwenzake huko Matemwe.
Alifahamishwa kwamba Wizara ya
Ardhi na Maendeleo ya Makaazi haina nia mbaya ya kumuonea mtu bali inahitaji
wananchi wafuate sheria ili kuepusha migogoro ya Ardhi inayojitokeza katika
maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Aidha Waziri huyo alitoa wito kwa wageni na
wenyeji ambao wanaohitaji kuekeza ujenzi wa aina yeyote kuhakikisha wanafuata
sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kupata kibali cha ujenzi kutoka Taasisi
ya Utoaji wa vibali vya Ujenzi(DCU)
kabla ya kuanza hatua ya ujenzi huo.
Naye Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka
Kamisheni ya Ardhi Muchi Juma Ameir alifahamisha kua lengo la kuwepo kwaTaasisi
hiyo ni kuepusha migogoro ya ardhi isiyo na ulazima kwani inarudisha nyuma
jitihada za kuleta maendeleo ya nchi yetu.
‘’Kibali ambacho kinatolewa na
DCU huwa kinaonesha michoro ya ujenzi katika eneo husika na mipaka, hivyo vibali vya wawekezaji hao vitaonesha mpaka wa kila mmoja”
Alisema Muchi.
Naye Muekezaji Matemwe Bangaloes
alisema Mwekezaji NJ Water Sports amejenga ukuta katika eneo lake baada ya
kutofahamina kauli yangu ya kumtaka avunje ukuta huo kwa muda wa miezi sita ndipo alipoamua kwenda
Mahakamani kumshtaki ili apate haki yake.
Kwa upande wake Muekezaji NJ
Water Sports alisema kua alifuata taratibu zote kabla ya kuanza ujenzi huo na
yuko tayari Serikali ichukuwe hatua za kupima tena michoro ya ujenzi na endapo
atakua ameingia katika eneo la muekezaji mwenzake basi yuko tayari kuliachia
eneo ambalo limeingia upande wake au kulinunua ili aendelee na ujenzi wa michezo ya baharini.
Mgogoro huo ulianza mwezi wa June, 2022 baada ya NJ water
kujenga ukuta katika eneo linalodaiwa sio la kwake hali ambayo imepelekea
viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Ardhi, Rahma, Mkuu wa Mkoa Kaskazini,
Ayoub, Mkuu wa wilaya Sadifa, watendaji wa wizara mbali mbali kuingilia kati na
mahakama kusimamisha ujenzi huo.
Mwisho
Comments
Post a Comment