NA HAJI NASSOR, PEMBA::::
MTUHUMIWA
Bilali Hamad Kombo miaka 19, mkaazi wa Vitongoji wilaya ya Chake chake mkao wa
kusini Pemba, ameanza kuhemea rumande, akikabiliwa na tuhma za kumbaka mtoto wa
miaka 14.
Ilidaiwa mahakamani hapo na
Mwendesha mashataka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashataka Ali Amour Makame
kuwa, mtuhumiwa huyo bila ya halali na bila ya ridhaa ya wazazi wake,
alimtorosha na kisha kumbaka mtoto huyo.
Alidai kuwa, tukio la kwanza
la utoroshaji lilitokea Oktoba 29, mwaka huu, majira ya saa 1:40 asubuhi
ambapo, mtuhumiwa anadaiwa kumtorosha mtoto huyo kutoka nyumbani kwao na
kumpeleka nyumbani kwake Vitongoji wilaya ya Chake chake.
Kufanya hivyo ni kosa
kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018,
sheria ya Zanzibar.
Kosa la pili linalomkabili
mtuhumiwa huyo, ni la ubakaji, kwa mtoto huyo huyo, alilodaiwa kulitenda pia
Oktoba 29, mwaka huu, majira ya saa 2:00 asubuhi, wakati akiwa naye nyumbani
kwake.
Kufanya hivyo ni kosa
kisheria, kinyume na kifungu cha 108 (1), (2), (e) na kifungu cha 109 (1) cha
sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Mara baada kusomewa shitaka
lake, Hakimu wa mahakama hiyo maalum ya makosa ya udhalilishaji, mkoa wa kusini
Pemba, Muumini Ali Juma alimuuliza mtuhumiwa ikiwa amefahamu.
Hakimu huyo, alimtaka
mtuhumiwa ikiwa hajafahamu kusomewa tena upya, na Mwendesha mashataka ingawa
alidai ameshafahamu na kuyakana makosa yote.
‘’Mheshimiwa Hakimu nimemsikia
vyema Mwendesha mashataka na makosa yote mawili ninayotuhumiwa nayo kuyafanya,
lakini nakataa,’’alidai mtuhumiwa huyo.
Baada ya maelezo ya
mtuhumiwa huyo, Hakimu aliamuru kwenda rumande hadi Novemba 30, mwaka huu kwa vile makosa hayo hayana dhamana kisheria.
Hata hivyo Hakimu Muumini
aliutaka upande wa mashataka siku hiyo, kuwasilisha mashahidi wao, hasa kwa
vile ulidai upelelezi umeshakamilika.
Mwisho
Comments
Post a Comment