NA
HAJI NASSOR, PEMBA
WANANCHI
6,680 wa shehia ya Shumba mjini wilaya ya Micheweni Pemba, wanakabiliwa na huduma
ya maji safi na salama isiyo ya uhakika kwa mwezi mmoja sasa, unaowapelekea
baadhi yao, kutumia maji ya bahari kwa shughuli zao za kila siku.
Walisema, huduma hiyo
imekuwa ya kusua sua katika baadhi ya vijiji vyao, hali inayowanyima usingizi,
huku baadhi yao, wakinunua kwa dumu moja lenye ujazo la lita 20, kati ya
shilingi ya 500 hadi shilingi 1,000, kutoka shehia jirani.
Wananchi hao wa vijiji vya Chamboni,
Vumbini, Nduaga, Momogu, Mkunguni, Kichekwani, Tundumwe na Msasani kwa wale
wasio na uwezo wa kunua huduma hiyo, wamekiri kutumia maji ya bahari, kwa
shughuli nyingine.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi, walisema maji wanayonunua hutumia kwa ajili ya kupikia na kunywa
na kukoga tu, ambapo kwa upande wa shughuli za chooni na kukoshea vyombo,
hutumia maji ya bahari.
Mmoja kati ya wananchi hao
Hamad Ali Hamad, alisema sio wote wenye uwezo wa kununua maji kwa matumizi ya
kila kitu, hivyo baadhi yao, huenda baharini kuchota maji hayo.
‘’Ni kweli, kwa sasa
matumizi ya maji kama kukoshea vyombo, matumizi ya chooni, tumelazimika kutumia
maji ya bahari, maana haya ya ‘ZAWA’ hayapatikani kwa uhakika,’’alieleza.
Nae Kurata Bakar Said,
alisema huduma hiyo ya maji safi na salama, imekuwa adimu mno, na
imewalazimisha wengine kununua maji kutoka shehia za Majenzi na Micheweni.
Kwa upande wake Fatma
Mohamed Awadhi, alisema maji ya ‘ZAWA’ sasa imekuwa tunu kwao, na mifereji yao
imekaa kama pambo ndani ya nyumba zao.
‘’Unaweza kukaa wiki
ukasikia maji eneo fulani yanatoka, lakini ukifika unaweza kubahatika ndoo moja
au mbili, na kisha yanafungwa, hivyo kama unauwezo unaweza kununua,’’alifafanua.
Nao wananchi Omar Khamis
Kombo na Biache Mohamed Hamad walisema, walipomfuata sheha wao, aliwaeleza kuwa
tayari malalamiko hayo, ameshayafikisha kwa uongozi wa ZAWA wilaya ya Micheweni.
Sheha wa shehia ya Shumba
Mjini mjini Rahila Ramadhan Juma, alikiri kupokea mamalamiko ya wananchi wake,
juu ya ukosefu wa huduma hiyo, shehiani humo.
Alisema anaelewa kuwa, kwa zaidi
ya siku 30 sasa, baadhi ya wanachi hawaipatia kabisa huduma hiyo, na baadhi ya
maeneo yakitoka huwa ni kwa kusua sua.
‘’Kwa hakika, huduma ya maji
safi na salama ndani ya shehia yangu, imeshakuwa tatizo la muda sasa, na ni
kweli baadhi ya wananchi, wananunua na wengine kutumia maji ya bahari,’’alieleza.
Afisa wa Mamlaka ya Maji ‘ZAWA’
wilaya ya Micheweni Ali Rajab, alikiri kupokea malalamiko ya sheha huyo, juu ya
huduma hiyo kuwa ndogo, shehia ya Shumba mjini.
Alieleza kuwa, tatizo hilo
halitokani na uhaba wa huduma ya maji kwenye kisima wanachokokitegemea cha
Kijichame, bali na kupanda na kushuka kwa nishati ya umeme.
‘’Kupanda na kushuka kwa umeme,
kulikosambaa Pemba nzima, ndio sababu ya wananchi wa Shumba, mashine yao ya
kusukumia maji kukosa nguvu, nao kukosa huduma ya maji safi na salama,’’alifafanua.
Hata hivyo afisa huyo,
alisema kuwa kisima hicho ambacho kinauwezo wa kuzalisha lita 17,000 kwa saa
moja, na kuwekwa bomba lenye ujazo wa nchi tatu, kama sio tatizo la umeme
wananchi wengepata huduma ya kutosha.
Afisa Uhusiano wa ‘ZAWA’
Pemba Suleiman Anasi Massoud, alisema mashine iliyopo kwenye kisima cha
wananchokitegemea wananchi hao wa Shumba, kimekumbwa na shida ya umeme, ya
kupanda na kushuka.
‘’Mshine iliyopo kwenye
kisima hicho ni ya kisasa, hivyo kama umeme ukiwa mkubwa au ukiwa mdogo kama
ilivyo sasa, hujizima wenyewe na kukosa nguvu ya kusukuma maji,’’alieleza.
Hata hivyo, alisema
changamoto kubwa ambayo ipo kwa wananchi hao, ni ukosefu wa tenki la kuhifadhia
maji, ambapo hilo huisababishia mashine iliyopo, kufanyakazi kwa saa 24 bila ya
mapumziko.
‘’Wananchi wa Shumba mjini,
waondoe wasi wasi na waendelee na ustahamilivu, upo mradi mkuba wa usambaazaji
maji safi na salama kwa ajili yao tu, na utajenga na tenki la kuhifadhia maji
safi na salama,’’alifafanua.
Afisa Huduma kwa wawateja wa Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ Pemba Haji Khatib Haji, hivi karibuni alinukuliwa na vyombo vya habari, akisema tatizo la kupungua kwa umeme ovyo ovyo, kutokana na eneo la Tanga kupata hitilafu.
‘’Ndio mafundi wetu wamekuwa
wakishirikiana kwa karibu na mafundi wa TENESCO, ili kushughulikia tatizo hilo,
huku akiwataka wananchi, kuendelea kuwa wastahamilivu,’’alieleza.
Hivi karibuni, kwenye
kongamano la kutimiza miaka miwili ya rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi,
ilifahamika kuwa, kwa Pemba kuna vituo 27 vya huduma ya maji safi na salama na ujenzi
wa matenki matno (5), yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 1, kila moja.
Mwisho
Comments
Post a Comment