HAJI NASSOR, PEMBA::
WAZAZI na walezi wa watoto wenye ulemavu shehia
ya Vitongoji wilaya ya Chake chake Pemba, wameitaka jamii kutowabagua vijana
wao, kwani wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, ili kuanzisha familia.
Walisema, bado baadhi ya
familia zimekuwa haziwachagua watoto wao kike, kwa sababu ya ulemavu wao, jambo
ambalo wanasema ni kuwanyima haki zao masingi.
Wakizungumza kwenye mkutano
wa kuihamasisha jamii kutiii sheria na kufanyika Vitongoji, walisema wamekuwa
na watoto wa kike kwa muda mrefu, bila ya kugongewa mlango.
Mmoja kati ya wazazi hao
Omar Khamis Omar, alisema jamii haiwaoni vijana wenye ulemavu kama sehemu ya
kuanzisha familia, jambo ambalo linawatia unyonge.
Alisema imekuwa ni adimu
kuona mtu mwenye ulemavu anaolewa au wakati mwengine kukubaliwa posa yake,
jambo ambalo, linawazidishia kujiona wanyonge.
‘’Mimi nna mwanangu ana
ulemavu wa viungo, basi tulienda kupeleka posa baba mzazi akakubali, ingawa
baada ya familia kukutana, tukirejeshwa kwa sababu ya ulemavu,’’alisema.
Nae Maimuna Hamad Mjaka,
alisema mtoto wake mwenye uziwi alishapokea posa mara mbili, lakini
inapokaribia wakati wa kufanya maandalizi ya harusi, wahusika hukimbia.
‘’Mwaka jana tulishapokea
fedha za awali za mahari, na wakati wanakwenda hospitali kuchunguuza afya zao,
wakamgundua ana tataizo ya usikivu hafifu, walikataa,’’alieleza.
Aidha mzazi Mayasa Haji Issa
‘da maa’ alisema pamoja na vijana wa
kike na kiume wenye ulemavu kuwa wastahamilivu hasa wanapoingia kwenye ndao,
lakini bado kundi kubwa la watu hao wanawapiga chenga.
Mmoja kati ya vijana miaka
26 ambao aliposwa mara mbili kwa miaka miwili tofauti, alisema kwa sasa
ameshakata tamaa, juu ya kuanzisha familia.
‘’Maana wanaonikataa
wanasema kwa sababu ya kuburura kwangu mguu, sasa hili mimi sikuliomba ni kazi
yake Allah, sasa kama wachumba wananikataa kwa hili, ni milele tena,’’alieleza.
Hata hivyo alisema hajakata
tamaa, kwa vile wenzake wawili wenye ulemavu kama wa kwakwe, aliosomanao chuoni
mwaka 2017, wameshaolewa.
Mratibu wa wanawake na
watoto shehia ya Kangagani Awena Salim Kombo, alisema suala la ndoa na mtu na
ulemavu wake halina uhusiano wowote.
‘’Ulemavu wakati mwengine
unatokana na matukio ya hapa na pale mfano ajali, kuungua moto sasa kila mmoja
anaweza kupata, isiwe jambo wengine kukosa haki za ndoa,’’alishauri.
Akizungumza kwenye moja ya
mikutano ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, Mkurugenzi wa
Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar Ussi Khamis Debe, alisema
kukataa kufanda ndoa kwa sababu ya ulemavu wa mtu aliyonao ni changamoto.
‘’Hata mimi wakati sijakuwa na kazi yangu, nilipeleka posa
kila kona, lakini mwisho nikapata mchumba na kuoa, sasa ni Mkurugenzi wananijia
wenyewe,’’alifafanua.
Kwa upande wake, Mtaribu wa
Idara ya watu wenye ulemavu kisiwani Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, alisema nguvu
za ziada zinahitajika, kuielimisha jamii, mchango wa watu wenye ulemavu.
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar
‘ZLSC’ tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, alisema suala la kuwa na mwenza ni la
kibinaamu zaidi.
‘’Sio suala la kuangalia
aina ya ulemavu wa mtu bali ni haki ya kibinadamu zaidi na ambayo haihitaji
manyanyaso wala kero ndani yake,’’alieleza.
Mkataba wa kimataifa wa haki
za watu wenye ulamavu, Ibara ya 18, imezitaka nchi zilizoridhia mkataba huu, kila
mtu mwenye ulemavu ana haki na kuheshimiwa kwa ajili ya utu wake kwa misingi
sawa na wenzao.
Ibara ya 23 (a) na (b)
imesema watu wote waliofikia umri wa kufunga ndoa, na kuanzisha familia na hata
suala la kupanga idadi ya watoto wawatakao na ni kosa kufungwa kizazi maana ni
haki zao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment